Elimu yetu inatuelekeza kwenye uchumi wa viwanda?
Muktasari:
- Itakuwa ni vigumu kufikia uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025 bila ya kuwa na msingi imara wa elimu.
Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuitoa Tanzania kutoka kwenye uchumi duni unaotegemea zaidi kilimo na mazao ya kilimo, kufikia ule wa nchi zenye kipato cha kati unaotegemea zaidi viwanda ifikapo mwaka 2025. Uchumi huo unatarajiwa kuwa na sifa muhimu zifuatazo:
Kwanza, utakuwa ni uchumi mseto wa nusu ya kilimo na sekta kubwa ya viwanda inayofanana na nchi za kipato cha kati. Pili, kiwango chake cha ukuaji kitakua kwa asilimia nane kwa mwaka au zaidi.
Aidha, Tanzania itaanza kuwa mshiriki mwenye nguvu na ushindani katika masoko ya kikanda na duniani, ikiwa na uwezo wa kuelezea, kutetea na kukuza maslahi ya kitaifa.
Ili kuiwezesha Tanzania kufikia kipato cha kati na kuondokana na umaskini uliokithiri ifikapo mwaka 2025, Serikali ilianzisha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 iliyoanza kutekelezwa mwaka 2000 yenye malengo makuu matano ambayo ni kuboresha hali ya maisha ya Watanzania; kuwepo kwa mazingira ya amani, usalama na umoja na kujenga utawala bora.
Mengine ni kuwepo jamii iliyoelimika vyema na inayopenda kujielimisha na kujenga uchumi imara unaoweza kukabiliana na ushindani kutoka nchi nyingine.
Utekelezaji wa dira
Utekelezaji wa dira hii unafanyika kwa vipindi vitatu vya muda wa miaka mitano mitano. Ili kufikia malengo haya Serikali imeweka vipaumbele vitano vya msingi katika uwekezaji.
Kwanza, ni uwekezaji katika sekta ya miundombinu ya nishati, usafirishaji, Tehama, maji na umwagiliaji; Pili, ni uwekezaji katika sekta ya kilimo ikijumuisha mazao ya chakula na biashara, ufugaji, uvuvi na misitu.
Tatu, ni uwekezaji katika viwanda, hasa vinavyotumia malighafi ya ndani kwa maana ya kuongeza thamani, viwanda vikubwa vya mbolea na saruji, kielektroniki na vifaa vya Tehama.
Nne, ni maendeleo ya rasilimali watu, hasa kuinua stadi za kazi hususani katika masomo ya sayansi, teknolojia na ubunifu. Mwisho, mkazo utawekwa katika kuimarisha mafanikio yaliyopatikana katika utoaji wa huduma za jamii.
Ili kuwa nchi ya kipato cha aina hii ifikapo mwaka 2025, Tanzania itahitaji kuwa na idadi kubwa ya wafanyakazi wenye ujuzi na stadi katika nyanja mbalimbali. Aidha, kunahitajika kuwe na ongezeko kubwa la idadi ya wahitimu wanaotoka katika vyuo vyetu hususani katika masomo ya uhandisi na sayansi. ^Tutafikia lengo?
Mwaka huu tumebakiza miaka isiyozidi saba kuwa tumefikia malengo haya. Kwa hiyo ni vizuri kujitathmini kama kasi na mikakati tunayochukua kuubadili uchumi wetu ni sahihi au tunapaswa kubadili mbinu.
Tujiulize ni namna gani haya maudhui yaliyomo kwenye dira na mikakati iliyopo inachagizwa kwenye elimu ili kuleta maendeleo yanayokusudiwa?
Mwaka 2014, Tume ya Mipango ilipima mahitaji ya ujuzi ambao Tanzania ilikuwa inauhitaji ili kufikia hali ya kipato cha kati.Katika sekta ya uhandisi, viwanda na ujenzi, utafiti ulionyesha kuwa idadi ya wataalamu katika sekta hiyo ilikuwa 17,600 mwaka 2015/16 ingawa wanapaswa kuwa 148,800 ifikapo mwaka 2024/25!
Aidha, idadi ya wataalamu katika sekta ya kilimo ilikuwa 4,175 tu mwaka 2015/16 wakati mahitaji yanapaswa kuwa 15,130 ifikapo mwaka 2024/25.
Vilevile, katika masomo ya sayansi kwa ujumla, idadi ilikadiriwa kuwa 20,920 mwaka 2015/16; lakini watahitajika wanasayansi wasiopungua 87,100 ifikapo 2024/25 ili kukidhi mahitaji ya uchumi wa kati.
Takwimu hizi zinaonyesha kwamba mahitaji kwa sekta za elimu, ili kufikia malengo ya uchumi wa kati ni makubwa.
Jambo jingine linalotilia mashaka utayari wetu kufikia malengo ya uchumi wa kati si idadi ya wasomi tulio nao pekee, bali hususani ubora wa elimu waipatayo shuleni au vyuoni.
Ingawa Tanzania imefanikiwa kuandikisha watoto shuleni, tatizo kubwa limebaki katika ubora wa elimu waipatayo katika ngazi zote za elimu kuanzia msingi, sekondari, hadi vyuoni.
Tafiti za Uwezo zimekuwa zikionyesha matokeo ya kujifunza hayajafikia kiwango stahiki ukilinganisha na matarajio ya mitalaa katika masomo ya Kiswahili, Kiingereza, na Hisabati.
Mathalani, utafiti wa mwaka 2017, ulionyesha wanafunzi wa darasa la tatu na la saba walioweza kusoma hadithi ya Kiswahili ya darasa la tatu walikuwa ni asilimia 56, ilhali darasa la saba walikuwa asilimia 89.
Walioweza kusoma hadithi ya Kiingereza darasa la tatu walikuwa ni asilimia 13 na wale wa darasa la saba walikuwa asilimia 48. Walioweza kufanya hesabu za kuzidisha darasa la tatu walikuwa asilimia 35, ilhali wale wa darasa la saba walikuwa asilimia 78.
Kwa matokeo haya, ni dhahiri kuwa watoto wetu hawajifunzi. Aidha, kwa mujibu wa waajiri, wafanyakazi wa Tanzania kwa wastani wana sifa nzuri za elimu, lakini wana viwango duni vya ujuzi au stadi muhimu kama za mawasiliano, kufanya kazi katika timu na kutatua matatizo.
Tuwe wakweli. Itakuwa ni vigumu kufikia uchumi wa viwanda ifikapo 2025 bila ya kuwa na msingi imara wa elimu.
Elimu ndiyo itakayowapa wananchi maarifa, ufundi na stadi stahiki zitakazowawezesha kuwa na tija zaidi na kupambana katika ulimwengu uliozidi kuunganishwa.
Robert Mihayo ni mratibu wa uthibiti ubora katika shirika la HakiElimu. Anapatikana kupitia [email protected]