Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hanifa: Kutoka kuwa yaya hadi mwanafunzi mahiri darasani

Muktasari:

Hanifa ni miongoni mwa maelfu ya watoto wa kike hapa nchini Tanzania ambao kwa sababu mbalimbali wamekuwa wakikosa fursa ya kupata elimu.

Siyo kwamba Hanifa Shaban hakuwa na ndoto, la hasha, ndoto yake ni kuwa daktari ama mwalimu. Lakini kilichokosekana pengine ni matumaini ya kufikia ndoto hiyo.

Hanifa ni miongoni mwa maelfu ya watoto wa kike hapa nchini Tanzania ambao kwa sababu mbalimbali wamekuwa wakikosa fursa ya kupata elimu.

Akiwa na miaka 15 hakuwahi kwenda shule, wazazi wake walidai ni kutokana na shule kuwa mbali. Kwa kuwa alikuwa ‘yupoyupo’ tu nyumbani, akachukuliwa na dada yake na kumpeleka Mpanda mkoani Katavi kwa minajili ya kumsaidia kazi za nyumbani ikiwamo kulea mtoto.

 

Matumaini yarejea

Siku moja, Hanifa bila kujua aliamka mapema alfajiri kama ilivyokuwa ada yake na pengine aliiona siku hiyo kama siku tu ya kawaida.

Hakujua kuwa saa chache baadaye siku ile ingerejesha matumaini ya kuelekea kwenye ndoto yake. Aliendelea na majukumu yake ya kila siku, akianza na usafi wa nyumba na kuandaa chakula cha mtoto.

Kabla siku haijaisha wageni akiwamo Hawa Kamizula waliwasili kwenye nyumba yao. Huyu ni mtathmini wa majaribio ya Uwezo iliyo chini ya asasi ya Twaweza aliyefika nyumbani hapo kuwapima watoto wenye miaka 7-16 uwezo wao wa kusoma na kufanya hesabu rahisi za kiwango cha darasa la pili; ndipo bahati ikamwangukia Hanifa.

Hawa, alimwangalia Hanifa na kuona kitu ambacho wenzake hawakukiona. Ndipo aliposhawishika kumpima ili kuona kama anaweza kusoma.

Baada ya zoezi hilo ndipo ikagundulika kuwa Hanifa hakujua kusoma. Jitihada zikafanyika na hatimaye Hanifa akaingizwa moja kwa moja kwenye programu maalumu inayosimamiwa na watathmini wa kujitolea wa mpango wa Uwezo katika Halmashauri ya Mpanda Mjini, wakisimamiwa na kuratibiwa na shirika liliso la kiserikali la Kawodeo.

 

Aanza shule

Wakati anaanza mafunzo hayo hakuweza hata kusoma herufi a, e, i, o u lakini baada ya wiki mbili tu Hanifa alianza kusoma na kuandika maneno kama “baba”, “mama” na mengineyo ya namna hiyo. Ilikuwa ni ushindi mkubwa kwa Hanifa ambaye hakuwahi kuwaza kwamba siku moja angeweza kukamata kalamu na kuandika!

Jitihada zake hazikuishia tu katika muda wa mafunzo hata wakati wa usiku ambapo ndiyo mara nyingi hupata muda aliendelea kujifunza kwa bidii zote.

Baada ya miezi miwili tangu Hanifa aanze kujifunza kusoma kuandika na kuhesabu katika madarasa ya ya kujitolea, aliwashangaza watu wengi baada ya kuweza kusoma kwa ufasaha hadithi ya Kiswahili ya kiwango cha darasa la pili pamoja na kujibu maswali yaliyoambatana na hadithi hiyo.

Vilevile aliweza kufanya hesabu rahisi za kujumlisha na kusoma maneno rahisi ya Kiingereza. Huu ulikuwa ni ushindi mkubwa kwa Hanifa ambaye sasa hamasa ya kujifunza zaidi ndiyo imepamba moto, lakini je, nani wa kumsaidia ili aweze kusonga mbele?

Jitihada hizi za wadau hawa zilikuwa ni majaribio ya muda mfupi tu wa miezi mitatu na ndiyo zimefikia ukingoni.

Hata hivyo, mkasa na uwezo wa Hanifa ulimvutia Hartson Kyejo ambaye ni ofisa mkaguzi wa mahesabu Manispaa ya Mpanda, aliyeahidi kuhakikisha anajiunga na shule ya msingi.

Matone machache ya machozi aliyodondosha Hanifa yalionyesha dhahiri shauku kubwa aliyonayo juu ya maisha yake mapya ya kielimu anayotarajia kuyaanza, safari ambayo inaonyesha kufufua ndoto zake.

Hivi sasa Hanifa ni mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Mkapa wilayani Mpanda kama alivyoahidiwa na Kyejo.

Sababu iliyochangia Hanifa kuvushwa mpaka darasa la tatu ni kutokana na umri wake lakini kikubwa zaidi ni uwezo wake wa kusoma, kuandika na kufanya hesabu za kiwango cha darasa la pili.

Pamoja na kumsaidia Hanifa kyejo anatoa wito kwa Watanzania kwa kusema: “Naomba Watanzania wengine wenye uwezo wamsaidie kuhakikisha anapata mahitaji yake muhimu ya shule, maana kuna wakati majukumu yanaweza kunibana nikashindwa kuendelea kumsaidia” Hanifa anaendelea kuishi na dada yake ambaye naye anaona faraja kwa mdogo wake kupata nafasi hiyo.

Alipoulizwa kwa nini baada ya kumchukua Hanifa hakufanya jitihada za kumtafutia Hanifa shule, akajibu: “Kusema kweli sikujua kama katika umri wa Hanifa anaweza kukubalika shule, nafarijika kumwona akienda shule na imani ndoto zake zitatimia.”

Kwa furaha kubwa na hamasa ya kusonga mbele, Hanifa anasisitiza kuwa lengo lake ni kuwa daktari ama mwalimu. Hatimaye kibatari kilichozimwa kimeanza kuwaka tena. Lakini ni wangapi hapa nchini ambao vibatari vyao huzimwa milele?

Ni kina Hanifa wangapi Taifa linawakosa kwa kuwa tu hawajabainika licha ya kuwa wana uwezo mkubwa wa kuja kuisaidia nchi yao?

 

Programu za Uwezo

Uwezo chini ya Twaweza imekuwa ikifanya tathmini ya kuwapima watoto wenye umri wa miaka 7-16 katika stadi za kusoma na kuhesabu kwa kutumia majaribio ya kiwango cha darasa la pili.

Ripoti zote za matokeo ya tathmini ya Uwezo zinaonyesha kuwa watoto hawapati stadi hizo muhimu na hatimaye wengi wao huhitimu darasa la saba bila kuwa na uwezo wa kusoma na kufanya hesabu.

Kutokana na hali hiyo Uwezo ikawapa changamoto wadau wake kuona nini wanaweza kufanya katika jamii zao baada ya tathmini ili kusaidia watoto wasiojua kusoma na kufanya hesabu

Huo ndio ukawa mwanzo wa kuanzishwa programu ya majaribio ya miezi mitatu ya kuwasaidia watoto wenye umi wa miaka 7- 16 ambao hawana uwezo wa kusoma na kuhesabu.

Hanifa akawa miongoni mwa matunda ya program hiyo ya kupigiwa mfano.

Programu hii imefanyika katika wilaya 9 walipo wadau wa Uwezo. Katika kila wilaya, vijiji viwili vilichaguliwa na katika kila kijiji watoto zaidi ya 10 ambao hawajui kusoma na kuhesabu walichaguliwa.

Walimu wanaowafundisha watoto hawa ni vijana wa kujitolea katika jamii waliohitimu kidato cha nne na kuendelea, ambao hutumika kwenye tathmini za Uwezo.

Makala haya yameandaliwa kwa hisani ya asasi isiyo ya kiserikali ya Twaweza