Hivi ndivyo tunavyoweza kuwekeza kwa walimu

Muktasari:
Waandishi Ashby Hobson na Vileges A waliainisha maeneo matatu yanayotakiwa kuzingatiwa katika suala zima la mafunzo ya ualimu ambayo ni mafunzo ya awali wakiwa vyuoni, mafunzo wakati wa kipindi cha mwanzo cha kufundisha na mafunzo ya kumwendeleza mwalimu.
Mwaka 2002, jarida la Journal of Teacher Education lilitoa kwa ufasaha maana ya mafunzo ya ualimu.
Waandishi Ashby Hobson na Vileges A waliainisha maeneo matatu yanayotakiwa kuzingatiwa katika suala zima la mafunzo ya ualimu ambayo ni mafunzo ya awali wakiwa vyuoni, mafunzo wakati wa kipindi cha mwanzo cha kufundisha na mafunzo ya kumwendeleza mwalimu.
Mtindo huu wa kumwandaa mwalimu kikamilifu kwa kupitia hatua hizi zote, ulikuwapo enzi ya ukoloni, lakini ukaja kufa kifo cha mende miaka michache baada ya uhuru.
Mambo yaliyozingatiwa katika mfumo huu ni kwamba mwanachuo alipata mafunzo chuoni kwa kipindi cha miaka miwili. Katika kipindi hicho mwanachuo alifundishwa kwa nadharia na vitendo.
Alipofaulu mitihani yake ya nadharia na vitendo alipelekwa shuleni kuanza kazi. Wakati yuko kazini alikaguliwa na baada ya kuona kuwa anafaa kuwa mwalimu bora alipewa hati ya leseni ya kufundisha
Hati hii alidumu kwa miaka miwili hadi alipokaguliwa tena, na kama alionekana anafaa alipewa hati ya kudumu ya kufundisha kisha kusajiliwa katika daftari la kudumu la walimu. Wale wasiofaa waliachishwa kazi.
Ni vyema Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ikatambua kuwa huu ndiyo utaratibu unaotumika kwa sasa hata katika nchi zilizoendelea kama Marekani.
Wizara haina budi kutambua kuwa suala la elimu ni kipaumbele cha kwanza kwa maendeleo ya nchini, ndio maana bajeti ya mwaka huu imeiweka elimu kuwa kipaumbele cha pili na kuitengea Sh4.77 trilioni.
Mafunzo kwa walimu
Hatua ya kwanza ya mafunzo kwa walimu, huhusisha uteuzi wa watu wanaofaa kujiunga kwa mafunzo hayo.
Wakati wa ukoloni, waliochaguliwa kujiunga na mafunzo ya ualimu daraja la A walikuwa na sifa za kuwa na ufaulu wa juu wa daraja la kwanza na la pili. Ushahidi wa hili upo. Waliopata daraja la tatu walisomea mafunzo ya daraja B.
Lengo la utaratibu huu lilikuwa ni kuona kuwa walimu wetu wanatakiwa wawe na kiwango cha juu cha ufaulu ili waweze kumudu kufundisha masomo yao vizuri.
Baada ya uhuru sifa za uchaguzi wa wakurufunzi wa daraja la A ulibadilika ili taifa lipate walimu wengi. Hapo ndipo wahitimu wa daraja la tatu na hata la nne walipochaguliwa na kujiunga na ualimu.
Walioamua hivyo walikuwa na nia nzuri lakini walipotosha ukweli kuwa wingi si hoja. La msingi ni uhakika wa taaluma. Tukubali kuzingatia viwango vya ufaulu tukiamini kuwa elimu bora inatokana na walimu bora.
Vitendo na nadharia
Kimsingi mafunzo ya ualimu yanatakiwa yawe ni ya vitendo na nadharia. Vitendo inajumuisha kufanya mazoezi ya kufundisha kwa kipindi kifupi yanayojulikana kama ‘Single Lesson Teaching Practice” (SLTP).
Hapa wanachuo wanakwenda kufanya mazoezi ya kufundisha katika shule za karibu na ndiyo maana kila chuo kuna shule ya msingi iliyo katika eneo la chuo inayojulikana kama ‘Practicing school’ na kusimamiwa na chuo husika.
Kila mwanachuo anayejiunga na mafunzo ya ualimu anapaswa kufundisha kwa vitendo na hufanyiwa tathmini na wakufunzi na kupata maelekezo ya kumudu somo darasani kama vile namna ya kuzungumza, kuandika ubaoni, kueleza jambo, kuuliza maswali na kumudu nidhamu darasani.
Wakurufunzi pia wanapelekwa kufundisha katika shule zilizo mbali na chuo ili kujiunga na walimu wa shule hizo. Hii ni hatua inayowawezesha wakurufunzi kuzama katika taaluma ya ualimu kwa kufanya kazi na walimu wazoefu. Mfumo huu wa ufundishaji unajulikana kama ‘Block Teaching Practice’ (BTP).
Kwa bahati mbaya mafunzo nje ya darasa (SLTP na BTP) hayafuatwi kikamilifu kutokana ka upungufu wa fedha.
Mafunzo ya nadharia darasani kwa walimu ni masomo kama falsafa ya elimu, historia ya elimu, saikolojia na sosiolojia ya elimu, misingi ya ualimu, mbinu za ufundishaji, namna ya kumudu masomo darasani kama vile uwasilishaji wa mada na mengineyo.
Kabla mwalimu hajaenda darasani kufundisha anatakiwa ajiandae kwa kuangalia mihutasari inayotayarishwa na Taasisi ya Elimu Tanzania, kusoma vitabu vya kiada na ziada na hapo hutayarisha somo lake.
Baada ya uwasilishaji wa somo, mwalimu anatakiwa atoe mazoezi baada ya kuwasilisha mada na baadaye atasahihisha maswali na kutoa mrejesho kwa wanafunzi.
Kwa bahati mbaya, utaratibu mzima wa kuona kama walimu wanatekeleza majukumu yao haufuatiliwi na walimu wakuu wa shule kikamilifu.
Ualimu na maadili
Hivi sasa walimu nchini wanasikitisha, hawafuati kabisa maadili ya kazi yao hii adhimu. Kwa mfano, mwonekano wao hauleti picha ya unadhifu kama hapo nyuma. Baadhi ya walimu hawavai inavyostahili.
Utakuta mwalimu wa kiume anafuga ndevu, ana sharafa na sharubu na hata nywele hazichanwi. Hii ni aibu. Upi wajibu wa mwalimu mkuu kuhusu hili?
Walimu wengine wanavaa mashati yanayoning’inia nje ya suruali zao kama vijana wa kihuni barabarani. Wengine nguo zao hazinyooshwi na zina makunjo kama wauza nyanya gengeni. Hili ni kosa la kinidhamu kwa taaluma nzima ya ualimu.
Mwalimu anatakiwa kuwa mfano wa kuigwa mtaani. Anatakiwa ashiriki katika masuala ya maendeleo kama kufanya usafi, kupanda miti kama wafanyavyo wananchi wengine.
Haiba ya ualimu na uchapakazi unapokuwapo, sasa ni haki ya mwajiri kumlipa mwalimu stahiki zake zote hasa mshahara unaokidhi mahitaji yake.
Stahiki nyingine ni kumwezesha kufanya kazi katika mazingira ya kuridhisha, kuwa na nyumba bora na iliyo karibu na shule ili kumpunguzia masafa marefu ya kusafiri kwenda na kurudi nyumbani.
Pia, awezeshwe vifaa vya kutosha vya kufundishia kama vitabu, daftari, vielelezo kama ramani na picha za kufundishia.
Tatizo lililopo nchini mara nyingi ni madai kuwa Serikali haina fedha ya kutekeleza haya, ndio maana kila siku nchi imekuwa ikikumbwa na migogoro isiyokwisha kati ya walimu na Serikali kama mwajiri mkuu wa walimu.
Mwandishi ni mwalimu mstaafu [email protected]
Kwa taarifa zaidi nunua gazeti lako la Mwananchi au soma mtandaoni kupitia www.epaper.mcl.co.tz