Je wajua kulala kifudifudi ni salamu ya heshima Nigeria

Muktasari:

  • Atlas of Ethnographic Societies waelezea tamaduni ambazo zinashangaza licha ya jamii husika kuziona ni za kawaida, ikiwemo tamaduni inayopatikana nchini Ugiriki ambapo bibi harusi hutemewa mate kama ishara ya kumtakia heri na kumuondolea mikosi na mabaya.

Jambo moja linalowatofautisha binadamu na ulimwengu wa wanyama ni tabia ya kukuza mila na desturi katika kila kitu kinacho wazunguka kuanzia urembo wa kimila hadi tabia.

Kwa mujibu wa mtandao wa ncbi.nlm ‘National Center for Biotechnology Information’ ulionukuu Price 'Atlas of Ethnographic Societies, nakueleza kwamba kuna tamaduni zaidi ya 3800 duniani za kipekee ambazo zipo zilizozoeleka na hazionekani kama za kushangaza lakini zipo ambazo ukizisikia zitakushangaza.

Kwa jamii husika inayosimamia na kufuata tamaduni hizo inajivunia uwepo wa tamaduni wanazoziamini, wanaziheshimu, kuzithamini na kuziendeleza kutoka vizazi na vizazi.

Hivyo pamoja na uwepo wa tamaduni nyingi, zipo za kushangaza zaidi ulimwenguni, miongoni mwa hizo ni,

Tamaduni ya kubarizi kwenye makaburi huko nchini Denmark, wakati makaburi ni sehemu ya kuogopwa katika nchini nyingi, Wadenmark wao wanaona inafaa kubadili makaburi yao kuwa maeneo ya kujumuika na kubarizi.

Makaburi yao yamepambwa vizuri na hutembelewa na wengi wakati hali ya hewa inapoanza kuwa joto.

Sehemu ya makaburi ya Assistens Cemetery iliyopo katika mji mkuu wa nchi hiyo, Copenhagen ni mfano mzuri wa makaburi hayo ambapo kubarizi hapa utakuwa unashiriki pamoja na wadenmark wengi maarufu waliozikwa hapo akiwemo Christian Andersen.

Kulala kifudifudi kama heshima nchini Nigeria, kwa watu wa jamii ya Yoruba, kabila ambalo limechukua sehemu kubwa nchini Nigeria, mila ya kulala kama salamu inachukuliwa kwa uzito mkubwa hasa wakati wa kusalimia wazee ama watu wazima.

Imezoeleka upigaji wa magoti mila iliyo maarufu Afrika, Lakini kwa Yoruba, kijana kulala chini kabisa na kuweka uso chini ni ishara ya utii kwa wakubwa.

Kuwatemea mate mabibi harusi, mila hii ilipata umaarufu mwaka 2002 kupitia filamu ya 'My big fat greek wedding'.

Kutemea mate katika tamaduni za Kigiriki ni namna ya mtu kukutakia heri na kusaidia kuondoa mikosi na mabaya.

Kwa miaka ya sasa desturi hiyo imebadilika na kuwa kitendo cha ishara zaidi ambapo wageni hutamka kwa nguvu "ftou ftou ftou." Na kutema mate nchini Ugiriki.

Salamu za mabusu, kupiga busu ni jambo kama la kawaida katika jamii nyingi hasa za Magharibi, lakini kupiga busu kila mtu na kwa idadi zaidi ya mara moja na kila wakati ni utamaduni uliozoeleka sana nchini Ufaransa.

Katika kila utamaduni kuna namna yake ya kusalimiana. Ufaransa ili uonekanae umethamini mtu na kumsabahi ni muhimu kumpiga busu, na unavyompiga busu mara nyingi zaidi ni kuonyesha thamani yake na namna unavyomuheshimu zaidi.