Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mbinu za kumfundisha mtoto kusoma akiwa nyumbani

Muktasari:

  • Mhadhiri wa masuala ya mitalaa, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge, Bahiya Abdi anasema kuna mambo kadhaa ya kuangalia tunapozungumzia uwezo wa mtoto kusoma.

Katika utafiti uliofanywa na prrogramu ya Uwezo iliyo chini ya shirika la Twaweza, zaidi ya nusu ya watoto wa darasa la nne na tano katika nchi za Afrika Mashariki hawana uwezo wa kusoma na kuandika

Mhadhiri wa masuala ya mitalaa, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge, Bahiya Abdi anasema kuna mambo kadhaa ya kuangalia tunapozungumzia uwezo wa mtoto kusoma.

‘’Mbali na mtoto kutambua herufi, lazima awe na uwezo wa kusoma kwa haraka. Lakini pia, uwezo wa kusoma unapimwa kwa kiwango cha kuelewa kile anachokisoma. Kama mtoto anaweza kusoma tu lakini hawezi kupata ujumbe vizuri, hapo tunaweza kusema uwezo wake uko chini ya kiwango,” anasema.

Kwa mujibu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) mtoto wa darasa la kwanza na la pili anatarajiwa kutambua na kusoma kwa ufasaha maneno 50 yenye maana kwa dakika na maneno 40 yasiyo na maana kwa dakika.

Kadhalika, anatarajiwa kuandika kwa ufasaha herufi kubwa na ndogo, na kufanya hesabu za kujumlisha na kutoa sambamba na kutambua herufi zinazokosekana.

Suala la watoto wetu kushindwa kusoma na kuandika kwa kiwango kinachotakiwa, limekuwa mjadala mrefu katika majukwaa mbalimbali ya elimu. Sababu zinazotajwa ni nyingi.

Moja, mazingira yasiyo rafiki katika shule zetu yanayowanyima watoto fursa ya kujifunza kwa ufasaha. Mazingira ni pamoja na vifaa vya kujifunzia pamoja na walimu wenye sifa na ari ya kufundisha.

Lakini pili, ni mrundikano wa masomo mengi katika madarasa ya awali. Mtoto mdogo ambaye kimsingi bado anakua kiufahamu , anapolazimika kusoma mambo mengi kwa wakati mmoja, inakuwa vigumu kuelekeza nguvu zake kwenye kukuza uwezo wa kusoma na kuandika.

Mbali na sababu hizo, ipo nyingine ya wazazi kutokuweka mazingira yanayomwezesha mtoto kujifunza akiwa bado nyumbani.

“Mazingira ya nyumbani yana nafasi kubwa ya kumwezesha mtoto kusoma, kuandika na hata kuhesabu. Mzazi akitambua nafasi yake, kazi ya mwalimu atakayekutana na mtoto shuleni itakuwa rahisi sana,” anaeleza.

Katika makala haya tunajadili maeneo matano yanayoweza kukuza uwezo wa mtoto kujifunza kusoma, kuandika na kuhesabu katika mazingira ya nyumbani.

Picha za irabu

Jema Karume, mkufunzi wa Chuo cha Ualimu Singachini nje kidogo ya mji wa Moshi, anashauri wazazi kuwapa watoto vifaa vinavyowasaidia kutambua irabu.

Anasema, “Hatua ya kwanza kujifunza kusoma na kuandika ni kutambua irabu na tarakimu. Hapa mzazi anahitajika kumnunulia mtoto mabango (poster) yenye irabu na tarakimu. Mtoto ataanza kuzoea zile irabu na huo ndio mwanzo wa kujifunza kusoma na kuandika.”

INAENDELEA UK 14

INATOKA UK 13

Ushauri huu wa kitaalam ni wa msingi kwa wazazi wanaotamani kuona watoto wao wanajifunza kusoma mapema. Badala ya kumnunulia mtoto midoli isiyomsaidia kujifunza, mtafutie mtoto vifaa vinavyohusianisha picha na maneno. Unapopata nafasi, mwelekeze. Hatua kwa hatua mtoto atajifunza kusoma.

Vifaa vya kuandikia

Upendo Zakaria, mkufunzi wa Chuo cha Ualimu Singachini, naye anashauri wazazi wawape watoto vifaa vya kuandikia.

Anasema, “Unaweza kumpatia mtoto kalamu na penseli akajifunza namna ya kuishika.”

Katika hatua za ukuaji wa mtoto, kwa kawaida mtoto anaweza kuanza kushika kitu vizuri kwa vidole vyake katika umri wa miaka mitatu. Kwa nini ni muhimu mtoto aanze kuzoeshwa kushika kalamu mapema?

Mkufunzi Upendo anajibu: “Kushika kalamu ni mazoezi ya kukomaza misuli ya mikono na vidole. Mtoto hawezi kuandika kama misuli yake miepesi (smooth muscles) haijakomaa vizuri.”

Desturi ya kusoma nyumbani

Doris Lyimo, mhadhiri wa lugha Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge, anafikiri ni muhimu kujenga desturi ya kusoma katika mazingira ya nyumbani.

Anasema: “Mtoto huiga kwa mzazi kama anayo desturi ya kusoma. Lazima mzazi amwongoze mtoto kusoma kwa kuhakikisha si tu na yeye anaonekana akisoma, bali nyumba ina vitabu na magazeti ya kusoma”

Pia kuna suala la maagizo tunayowapa watoto wetu kama anavyofafanua Jema Karume, anayeandaa walimu wa shule za msingi: “Mzazi ampe mtoto maagizo yanayochochea kufikiri na kuhesabu. Mfano, unamwambia mtoto niletee vijiko viwili. Hapo unamlazimisha kujifunza kuhesabu vitu.”

Vitabu vya hadithi

Bahiya ambaye pia amekuwa akifanya tafiti kadhaa za kubaini mazingira yanayorahisisha kusoma na kuandika, anashauri wazazi wawapatie watoto vitabu vya hadithi fupifupi.

Anasema: “Nunua vitabu kwa ajili ya mwanao. Mtafutie vile vitabu vya hadithi fupi fupi za kusisimua ajenge mazoea ya kusoma. Wewe kama mzazi msikilize wakati anasoma na kisha muulize maswali ajibu.”

Utaratibu kama huu ukifanyika mara kwa mara una nafasi kubwa ya kumjengea mtoto hamasa ya kujifunza kusoma kwa umahiri zaidi. Mbali na kumfundisha kusoma, mtoto anakuwa na uwezo wa kuelewa kile anachokisoma kwa ufasaha zaidi.

Je, hadithi zinawafaa wale wanaojua kusoma pekee? Mhadhiri Bahiya anasema: “Vitabu vinawafaa hata watoto wasiojua kusoma. Kama mtoto bado hajui kusoma, msomee hadithi na yeye asikilize. Ukishamsomea ni muhimu umpe nafasi aulize maswali yanayohusu hadithi hiyo.”

Michezo

Mhadhiri Bahiya anafikiri michezo nayo ina nafasi muhimu katika kumwandaa mtoto kusoma na kuhesabu.

Anasema, “Wazazi wanatakiwa kuwahamasisha watoto kucheza michezo inayowasaidia kujifunza kusoma, kuandika na kuhesabu. Mfano, mchezo wa kuruka kamba ilihali wakihesabu.”

Karume naye anaungana na ushauri huo wa Bahiya kwa kusema: “Wazazi wasichukulie michezo kama kupoteza muda. Kupitia michezo mtoto atajifunza kuhesabu vitu vingi. Muhimu tu iratibiwe vizuri na ifanyike kwa muda muafaka.”

Tunafahamu watoto hucheza kwa makundi. Wanapojigawanya kwa makundi ya ushindani, watahesabu idadi yao kwa kila kundi.

Mambo hayo kwa hakika yana nafasi ya kuwa darasa lisilo rasmi linalowajengea watoto ujuzi wa hesabu kabla hata hawajaandikishwa kwenda shule.