Nguvu ya lugha kama chombo cha mawasiliano-1
Muktasari:
Kuna mambo mengi ya muhimu katika sauti za lugha ambayo hayawezi kuwasilishwa vyema kwa kutumia maandishi. Mambo hayo ni kama, kiimbo, toni, mkazo, kidatu.
Mawasiliano ni mchakato wa kuhawilisha taarifa kwa njia ya kubadilishana mawazo au hisia kupitia mazungumzo, ishara na maandishi.
Lugha inaweza kuwa ya maandishi na ishara ili kufanikisha ubadilishanaji wa taarifa unaoleta maana baina ya pande mbili au zaidi na walengwa wake, hasa ni viumbe hai. Pia wanaowasiliana lazima wawe na akili timamu ili kuweza kufikisha ujumbe uliokusudiwa.
Ndiyo maana lugha nMawasiliano ni mchakato wa kuhawilisha taarifa kwa njia ya kubadilishana mawazo au hisia kupitia mazungumzo, ishara na maandishi.i nyenzo muhimu katika mawasiliano ya binadamu. Ni nyenzo inayomwezesha katika kujipatia maendeleo kwa kuwa inamsaidia kuwasiliana na watu wengine ulimwenguni na kufanikisha katika elimu, diplomasia, biashara, sayansi na teknolojia.
Hivyo lugha ya mwanadamu imeundwa katika mifumo ya sauti na maana. Lugha huundwa kwa sauti ambazo huunganishwa kuunda neno au sehemu ya neno. Maneno nayo huungana kuunda miundo mikubwa zaidi yenye maana kama virai, vishazi, sentensi na aya. Huu ndiyo hasa msingi wa mawasiliano. Aghalabu leo hii watu wanawasiliana kupitia mitandao ya kijamii kwa maandishi wengine kwa ujumbe wa sauti ili kukidhi haja ya mawasiliano. Kwa maana hiyo, lugha ya mwanadamu ni mfumo wenye kanuni, sheria na taratibu ambazo zikikiukwa basi mawasiliano yanaweza kukwama.
Kanuni hizi zinazotawala katika lugha ndizo zinazowawezesha watumiaji wa lugha fulani kuelewana. Lugha ni chombo cha mawasiliano ambacho binadamu anakitumia. Hii ina maana kuwa kuna sifa fulani za lugha za binadamu ambazo hazipatikani kwa kiumbe mwingine yeyote. Ingawa ndege na wanyama wanaweza kuwasiliana, mawasiliano yao huwa ni ya sauti au ishara ambazo kimsingi siyo lugha, pia huwa yanadhibitiwa na hisia tu kama hofu, njaa na ishara za kutoa taarifa. Binadamu ana uwezo wa kujifunza lugha nyinginezo na kuzitumia katika mazingira yake.
Uishara wa lugha unamaanisha kuwa maneno huambatanishwa au huhusishwa na vitu, matendo, mawazo au hisia kwa makubaliano ya unasibu tu. Vilevile, yale tunayoyasoma katika maandishi ni ishara tu, maana zake lazima zipatikane katika muktadha wa mawasiliano.
Hivyo basi, tunapojifunza lugha lazima tufahamu mfumo wa alama za lugha hiyo na kuelewa uhusiano uliopo kati ya ishara na vitu vinavyowakilishwa. Sifa kuu ya lugha ni kutumia sauti ambazo hutengenezwa na ala za sauti. Pamoja na maendeleo ambayo mwanadamu ameyafikia kwa sasa katika uandishi na uwasilishaji wa taarifa kwa kutumia lugha, sauti ndiyo msingi wa kila kitu.
Kuna mambo mengi ya muhimu katika sauti za lugha ambayo hayawezi kuwasilishwa vyema kwa kutumia maandishi. Mambo hayo ni kama, kiimbo, toni, mkazo, kidatu. Haya ni muhimu katika mawasiliano lakini hayawezi kuwasilishwa kisawasawa kwa kutumia maandishi.
Kwa kutumia lugha, binadamu anaweza kufanya vitu ambavyo viumbe wengine hawawezi kuvifanya. Mathalan lugha hutuwezesha binadamu kuelezea hisia zetu, kucheza, kufanya kazi na mengineyo. Yote haya yanawezekana kwakuwa tunayo lugha ambayo ndiyo nyenzo kuu ya mawasiliano.
Hivyo, kuwa lugha ni mfumo inamaanisha kuwa lugha ina muundo unaohusisha viambajengo mbalimbali. Vipashio hivi ni sauti, neno na sentensi. Kwa pamoja, vipashio hivi hushirikiana kuunda tungo zenye maana na kama tungo hizo hazina maana au kama haziwasilishi ujumbe wowote, basi tunasema haziwi lugha. Itaendelea Jumanne ijayo.
Mwandishi ni mhakiki wa lugha wa gazeti hili