Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wadau: Tuondoe vikwazo mtoto wa kike asome

Muktasari:

  • Miongoni mwa vikwazo hivyo ni ndoa katika umri mdogo, ubakaji, mila na desturi kandamizi ikiwamo ukeketaji, vishawishi, mazingira magumu sambamba na umaskini.

Kila mtoto anayo haki ya kupata elimu. Hata hivyo watoto wengi wa kike wanazongwa vikwazo vingi vinavyowafanya washindwe kutimiza ndoto zao za kielimu.

Miongoni mwa vikwazo hivyo ni ndoa katika umri mdogo, ubakaji, mila na desturi kandamizi ikiwamo ukeketaji, vishawishi, mazingira magumu sambamba na umaskini.

Hali yalisi ya mtoto wa kike

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la HakiElimu, John Kalage anasema zipo changamoto nyingi zinazomkabili mtoto wa kike ambazo zimekuwa kikwazo kikubwa cha kufikia ndoto zake kielimu.

Anasema bila kutatuliwa kwa changamoto hizo, mtoto wa kike ataendelea kuwa kwenye mazingira magumu yatakayoendelea kumuweka nyuma kielimu.

Ripoti ya ‘Human Right Watch’ ya mwaka 2017 imebainisha changamoto lukuki kwa mtoto wa kike ikiwamo walimu kuwataka wanafunzi kimapenzi na kuwatishia kuwaadhibu wanapokataa kufanya nao mapenzi.

Kalage anasema yapo madhara makubwa ya kisaikolojia wanayoyapata watoto wa kike kutokana na unyanyasaji huo na hivyo kuwafanya washindwe kuzingatia elimu hiyo wawapo shuleni.

Meneja wa idara ya ujenzi wa nguvu ya pamoja katika Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Grace Kisetu, anasema ukatili wa kingono ikiwamo ubakaji, kwa watoto wote wakiwamo wa kike ni mkubwa na kwamba, unaathiri makuzi ya mtoto na kumfanya ashindwe kutimiza ndoto zake kimaisha.

“Ukatili wa kingono kwa mtoto ni mkubwa na tatizo hili linapaswa kuchukuliwa kwa uzito mkubwa kwa sababu, watoto ni nusu ya Watanzania wote na hawa ndiyo taifa la kesho hivyo lazima walindwe na kuandaliwa vizuri,”anasema.

Anaongeza asilimia nane ya watoto nchini wamekeketwa na wengi wao wameingia kwenye ndoa za utotoni jambo ambalo ni baya zaidi.

“Mtoto wa kike akikeketwa anaandaliwa kuolewa hivyo watoto wengi wanaingia kwenye ndoa wakiwa na umri mdogo kwa sababu ya mila,”anasema.

Mwenyekiti wa Mtandao wa Kutokomeza Ndoa za Utotoni Tanzania unaojumuisha zaidi ya mashirika 30 nchini, Valerie Msoka anasema kuna ongezeko kubwa la mimba za utotoni hasa maeneo ya vijijini ikilinganishwa na mijini.

Msoka anasema katika utafiti uliofanywa na shirika hilo, asilimia 27 ya wasichana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 19, wamepata ujauzito kuanzi mwaka 2015 hadi 2016.

“Kiwango hiki ni kikubwa ikilinganishwa na ripoti ya mwaka 2010 ambapo, takwimu zilionyesha kuwa asilimia 23 ya watoto walipata mimba,” anasema.

Ukosefu wa mabweni na changamoto za umbali

Kalage anasema uhaba wa mabweni na changamoto za usafiri, vimekuwa vikiwaathiri wanafunzi hasa wa sekondari huku shule nyingi hasa za kata zikiwa mbali na makazi ya watu.

Kwa mujibu wa ripoti ya ‘Human Right Watch ya mwaka 2017, changamoto za usafiri huwa zinawalazimisha wasichana kufanya mapenzi na madereva wa bodaboda na daadala, ili wapate urahisi wa usafiri na mwishowe kujikuta wakipata mimba.

“Wasichana huwa wanaacha shule kwa sababu ya umbali kutokana na uchovu wa kutembea kila siku kwenda na kurudi shule na wengi wao wapo kwenye hatari ya kubakwa,” anasema.

Ofisa wa kitengo cha jinsia wa Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Godfrida Jola anasema mazingira hatarishi yanayomzunguka mtoto wa kike, yanachangia kwa kiasi kikubwa ashindwe kutimiza ndoto zake.

“Mtoto anabakwa, hana matunzo, anakabiliwa na njaa, mazingira yake ya kusoma ni magumu mwishowe yote ni mimba utotoni,”anasema na kuongeza;

“Fikiria kutoka nyumbani hadi shuleni ni kilometa 10 akiwa njiani anakutana na bodaboda anayempakia kila siku, mwisho anaingia kwenye vishawishi na kupoteza mwelekeo mzima wa maisha yake,”.

Mazingira ya kujifunzia na kufundishia

Kalage anasema kwa kiwango kikubwa mazingira ya kujifunzia na kufundishia sio rafiki kwa mtoto wa kike.

“Kuna uhaba mkubwa wa maji, matundu ya vyoo. Ukosefu huu unawaweka katika hatari ya kupata magonjwa yatokanayo na uchafu,”anasema.

Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TENMET), Catherine Sekwao anasema mtoto wa kike anahitaji mazingira bora yatakayomwezesha kumudu elimu yake.

“Shule zinapaswa kuwa na maji safi, vyoo bora na chumba cha kujisitiri anapotakiwa kubadlisha taulo kutokana na hali yake ya mwili wakati anapoingia hedhi,”anasema.

Mwanafunzi Suzan Thomas (sio jina halisi)anasema huwa analazimika kukaa nyumbani siku tatu anazokuwa hedhi kutokana na mazingira magumu shuleni.

“Huwa tumbo linauma na natokwa na damu nyingi hivyo kwa kuwa sina taulo natumia za kienyeji inabidi nibaki nyumbani hadi ninapomaliza,”anasema.

Sekwao anasema mtoto wa kike ana mahitaji maalumu zaidi na kwamba, ikiwa mazingira yake yataboreshwa, anaweza kufikia ndoto zake.

Kwa mujibu wa takwimu za elimu msingi (BEST), wasichana 700,000 hadi 750,000 wa darasa la saba hawahudhurii shuleni kati ya siku nne hadi tano kila mwezi ili kujisitiri kwa aibu.

Sekwao anasema lazima kuwe na utaratibu utakaosaidia kushughulikia maumbile ya watoto wa kike, ili wamudu masomo yao kama ilivyo kwa watoto wa kiume.

Hali ya uandikishaji na upatikanaji wa fursa kielimu

Kalage anasema japo hali ya uwiano katika uandikishaji wa wanafunzi kwa shule za msingi ni 1:1, kwa sekondari hasa kidato cha tano na sita, idadi ya wasichana huwa ndogo na kufikia 1:2.

Anasema kuwa hiyo ina maana kuwa nusu ya wasichana huwa wameachwa nyuma kutokana na changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Mchambuzi wa masuala ya jinsia, Dk John Frank anasema lazima wasichana waandaliwe mazingira mazuri ili uwiano wao shuleni usipungue kama hali inavyoonyesha.

“Wasichana wengi wameishia hapo katikati kwenye ndoa za utotoni, mimba za utotoni, kubakwa, kulawitiwa, kuacha shule na mambo mengine mengi. Lazima watoto wa kike wasaidiwe,” anasema.

Tunawezaje kumsaidia mtoto wa kike?

Kalage anasema lazima Serikali ijikite kwenye kutoa elimu kwa usawa kwa kuhakikisha kuwa inatatua changamoto zinazomkabili mtoto, ikiwamo mazingira magumu ya kujifunzia na kufanikiwa kuwapo kwa elimu jumuishi.

Anasema ipo haja ya kutoa elimu kwa umma na watoto wa kike, namna ya kumlinda mtoto wa kike dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia na athari ya vitendo vya ngono zembe.