Magharibi walivyoandika kuhusu kifo cha Nyerere
Muktasari:
Jarida linalozungumzia watu maarufu duniani lijulikanalo kama Forbes, baada ya kifo cha Mwalimu liliandika hivi “The death of Julius Nyerere, African independence leader and longtime dictator of Tanzania, evoked a flood of encomiums worldwide. The praise is misplaced. Nyerere’s approach devastated much of postcolonial Africa (Forbes, 1999).
Wakati Watanzania tukimkumbuka Mwalimu, nimeona nirejee nyuma hadi mwaka 1999 ili kuangalia majarida ya magharibi yalivyoandika mara baada ya kifo chake. Kufanya hivi ni kukumbuka mabaya yaliyozungumzwa kuhusu Mwalimu ili tuyajadili madai haya na kutufanya tuyaenzi mazuri yake.
Jarida linalozungumzia watu maarufu duniani lijulikanalo kama Forbes, baada ya kifo cha Mwalimu liliandika hivi “The death of Julius Nyerere, African independence leader and longtime dictator of Tanzania, evoked a flood of encomiums worldwide. The praise is misplaced. Nyerere’s approach devastated much of postcolonial Africa (Forbes, 1999).
Kwa tafsiri isiyo rasmi, kifo cha Julius Nyerere, kiongozi wa uhuru wa Afrika na dikteta wa muda mrefu wa Tanzania, kimesababisha mafuriko ya rambirambi duniani kote. Sifa anazopewa si mahali pake. Mtazamo wa Nyerere ulijulikana sehemu kubwa ya Afrika baada ya ukoloni.
Tukiijadili kauli hii ya Forbes, kwanza tunatambua Forbes ni akina nani, ni mabwana wakubwa wa dunia ambao Mwalimu aliwaita “wakubwa”. Watu wenye uchu wa kunyonya rasilimali za Bara la Afrika na watu wake, kitu ambacho Mwalimu alisimama kidete kukipinga kipindi chote cha uhai wake akiwa Rais wa Tanzania na hata baada ya kung’atuka madarakani.
Forbes ndiyo wanaofuatilia utajiri wa watu matajiri duniani bila kujali utajiri wao waliupataje. Kwa hiyo si jambo la ajabu kwao kuiona misimamo ya Mwalimu kutetea rasilimali za Afrika hususan Tanzania, zisiwanufaishe wakubwa hao kwa sababu misimamo hiyo iliyanyima mataifa tajiri kuchota utajiri wa Tanzania.
Forbes wanamuita Mwalimu “dikteta wa muda mrefu wa Tanzania”. Kitu wanachosahau ni kwamba takriban kipindi chote cha utawala wa Mwalimu, dunia ilikuwa katika kile kiitwacho “vita baridi” kati ya nchi za kibepari na zile za kisoshalisti. Mwalimu aliamua kuiweka Tanzania katikati ya nchi hizo kupitia kile kilichojulikana kama Umoja wa Nchi zisizofungamana na upande wowote.
Mwalimu alikataa taifa lolote kuwachagulia Watanzania rafiki. Ujerumani ya Magharibi ilipotishia kukata misaada yake kwa Tanzania kupinga Ujerumani ya Mashariki kufungua ubalozi wake Zanzibar, Mwalimu aliiambia Ujerumani Magharibi waondoe misaada yao yote ili kulinda heshima ya Tanzania.
Pia, Mwalimu alisema maneno ambayo yanapaswa kuandikwa kwa wino wa dhahabu “we would not allow our friends to choose enemies for us” yaani hatuwezi kuwaruhusu marafiki zetu watuchagulie maadui. Huyu ndiye Mwalimu ambaye awamagharibi, ingawa si wote, wanamsema kwamba misimamo yake ilizitia katika umaskini nchi za Afrika. Alikubali kukosa misaada ya “wakubwa” kulinda heshima ya Waafrika.
Wakati taasisi ya kimarekani ya Millenium Challenge Corporation (MCC) ilipositisha msaada wake kwa Tanzania kwa sababu za nchi yetu kutokuheshimu demokrasia, Rais John Magufuli alinikumbusha msimamo huu wa Mwalimu kwa Ujerumani Magharibi pale aliposema “ni heri kula muhogo kuliko mkate wa masimango”.
Ninachokizungumzia hapa siyo kuhalalisha mapungufu ya kidemokrasia yaliyofuatia kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar wa Oktoba 25, 2015 jambo lililofanyika kinyume cha demokrasia. Ninajaribu tu kuoanisha msimamo ule wa Mwalimu na kauli ya Rais Magufuli.
Siyo kuhusu mabilioni ya MCC tu, Rais Magufuli ameonesha msimamo hata kuhusu mkataba wa kibiashara kati ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya (EPA). Hata baada ya Kenya na nchi nyingine kumgeuka na kukubaliana na mkataba huo, Tanzania imeshikilia msimamo kuwa mkataba huo utakwamisha juhudi za kujenga uchumi wa viwanda nchini.
Rais Maguful ameanza kufuata nyayo za Mwalimu kwa mbali kutokana na hatua anazochukua kulinda heshima ya Mtanzania, ikiwamo kukataa nchi kutegemea misaada kutoka nje wakati ni tajiri.
Jarida la Forbes lilipomuita Mwalimu dikteta, tukumbuke kuwa zama za vita baridi nchi zilichagua ama siasa ya vyama vingi au chama kimoja. Nchi nyingi za Afrika zilichagua siasa ya chama kimoja kutokan ana mazingira ya uadui kutoka nje. Kama katika hali ya uchanga wa nchi hizo vyama vingi vingeruhusiwa, maadui wangetumia vyama kuzivuruga.
Kwa nchi za magharibi za kibepari, mfumo tofauti na ule wa vyama vingi unaoendana na siasa zao za kibepari kwao ulikuwa udikteta. Kwa hiyo udikteta anatuhumiwa nao Mwalimu ni kwa mtazamo wa nchi hizo ambako jarida la Forbes ndiko liliko. Nalo jarida la Newsweek la Marekani, kuhusu kifo cha Nyerere liliandika “How does a leader wreck a country’s economy yet die a national hero? Julius Nyerere’s inefficient leadership dried Tanzania of funds, but his personality was irresistible {Newsweek, Oktoba 25, 1999).
Wakiwa na maana inakuwaje kiongozi auwe uchumi wa nchi na bado afe akiwa shujaa wa taifa? Uongozi usio na ufanisi wa Julius Nyerere ulikausha fedha za Tanzania lakini heshima yake haikuweza kupingika. Ukweli ni kwamba wazungu waloweka mfumo wa uchumi na biashara duniani usiozingatia usawa ndiyo sababu ya umaskini wa nchi za Afrika Tanzania ikiwemo.
Lakini, sehemu kubwa ni usaliti wa mataifa makubwa dhidi ya nchi changa kupitia upangaji wa bei za bidhaa zetu, ndiyo mambo yaliyochangia tusifanikiwe.
Mikopo ya Benki ya Dunia na sera za Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ndizo zilikuwa kikwazo cha uchumi wa mataifa machanga kama Tanzania chini ya Mwalimu, kiasi cha kushindwa kufurukuta na hatimaye wanakuja kutulaumu kuwa Waafrika ni wavivu na hawana akili.