MAHOJIANO MAALUMU: Safari ya maisha na mikasa mizito kwa Afande Sele

Msanii Afande Sele (kushoto) akizungumza na mwandishi wa makala hii, Imani Makongoro, nyumbani kwake Kata ya Mazimbu mkoani Morogoro. Picha na Elizabeth Joachim.

Sikumfahamu, nilimuona ni mwanamke tu amekaa sebuleni, nilimsalimia na kuendelea na shughuli zangu naye aliniangalia bila kusema chochote, hivyo ndivyo nilivyokutana na mama yangu mzazi kwa mara ya kwanza,” anaanza kusimulia Afande Sele katika mahojiano maalumu na gazeti hili akiwa nyumbani kwake kata ya Mazimbu, mjini Morogoro.

Afande Sele, ambaye jina lake halisi ni Seleman Msindi, kwa hisia kali zenye maumivu anakumbuka namna alivyojilea mtaani, akiwa na umri mdogo akipambana na changamoto za dunia kabla ya mafanikio yake kufunguka kupitia kipaji chake cha muziki hadi kuwa mfalme wa Rhymes 2004.

“Yalikuwa ni maisha mabaya sana kwangu, japo kuna wakati huwa nahisi yalinitokea kwa sababu, labda Mwenyezi Mungu alikuwa na mipango haya yanitokee,” anasema Afande Sele.

Staa huyo wa Bongofleva na baba wa watoto wawili, Tundajema na Asantesanaa, mabinti aliolazimika kuwalea mwenyewe baada ya kifo cha mkewe, Asha (Mama Tunda), kilichotokea miaka tisa iliyopita anasema alipambana ili binti zake hao wasije kuishi maisha kama aliyopitia yeye.

“Tulikuwa na malengo mengi sana na Mama Tunda, nakumbuka Mwenyezi Mungu alipomchukua, Tunda alikuwa kidato cha pili na Asantesanaa alikuwa na mwaka mmoja na miezi kadhaa, sikufahamu nitawalea vipi hawa binti zangu, lakini nilisema sitoruhusu wapitie maisha kama yangu,” anasimulia.


Safari ngumu ya makuzi yake

Anasema baba yake alifariki akiwa na miaka minne, hakuwa akifahamu chochote kuhusu kifo na hakuna ndugu upande wa mama yake mzazi wala mama yake aliyehudhuria mazishi ya baba yake, hawakujua anaishi vipi baada ya kifo cha baba yake.

“Mama na baba walitengana nikiwa mdogo, mama akaenda kuanzisha maisha mengine, sikuwa na kumbukumbu hata na sura ya mama yangu, hata alipofariki baba, mama na ndugu zake hawakuja kwenye msiba.

“Kwa baba yangu nilizaliwa peke yangu, sikuwa na kaka wala dada, kwa kuwa nilikuwa mdogo, nikalazimika kulelewa na mashangazi.

“Nikiwa na umri mdogo, kuna shangazi yangu mmoja ambaye yeye ndiye alijimilikisha mali za familia, aliniambia mama yangu ameshafariki, kwa umri wangu wakati huo sikuwa hata na uwezo wa kusema niende nikatafute kaburi alipozikwa,” anasimulia Afande Sele.

Baada ya kifo cha baba, Afande Sele anasema maisha yalianza kuwa magumu kwake, licha ya kuachwa kwa shangazi yake, lakini hakupata uangalizi wowote wa malezi kama ilivyo kwa watoto wengine.

“Nilijilea mwenyewe, sikuwa na mtu japo hata wa kufuatilia mwenendo wangu shuleni, nikienda sawa, nisipokwenda pia ni sawa, ilikuwa ni juu yangu, hakuna aliyejali nimekula au la, kulala pia ilikuwa ni kwa shida sana,” anasema Afande Sele na kuongeza;

“Nikalazimika katika umri mdogo kuanza kujilea mwenyewe, kuanzia niko darasa la kwanza hadi nafika la sita, sikuwahi kuwa na uangalizi kama watoto wengine, hata kula yangu ilikuwa ni juu yangu mwenyewe.

“Niliishi kupitia shamba ambalo liliachwa na babu na baba yangu kule Kichangani. Mzee alikuwa na eneo kubwa ambalo alipanda miti mingi sana ya matunda, kulikuwa na miembe zaidi ya 40, michungwa, michenza na matunda mengine mengi, mbogamboga na mazao mengine,” anasema.

Anasema shamba lile ndilo lilimlea, kwani alipokuwa akihisi njaa, alikwenda shambani na kukwanyua ndizi na kuzichemsha kwa chumvi na kula, au atachuma mchicha pori na kupika na chumvi kwa kutumia kuni alizookota humohumo shambani kwao, hivyo alianza kujipikia akiwa darasa la kwanza.

“Nikihitaji kitu cha shule, nitaingia shambani, nitaangua matunda yatakayokuwepo kwa wakati huo na kwenda kuuza, shuleni nilikuwa maarufu kwa kuwauzia walimu maembe, machungwa, nazi na mazao mengine.

“Jirani na kwetu kulikuwa na stesheni, hivyo wakati mwingine jioni nakwenda kuuza matunda pale stesheni kwa abiria wanaosafiri na treni na kupata pesa ya kujikimu.

“Nilikuwa na umri mdogo, lakini sikuwa na uangalizi wa mlezi yeyote, niliishi maisha ya mtaani, hakuna aliyejali kuhusu mimi, hata shangazi ambaye ndiye alijimilikisha kunilea hakuwa na muda na mimi,” anasema.


Aambiwa mama alikufa

Afande Sele anasema kuna siku alimuuliza shangazi yake kuhusu mama yake baada ya kuona kila kitu kinakuwa kigumu kwenye maisha yake.

“Alinijibu, mama yako alikufa siku nyingi, kwa kuwa nilikuwa mdogo na hata sikuwahi kufahamu kuhusu yeye, niliamini ni kweli amefariki dunia na nikaendelea na maisha mengine nikiwa nimekata tamaa, nikiamini wazazi wangu wote wamefariki japo kwa mama sikuwahi kuliona hata kaburi lake,” anasema.

Anakumbuka akiwa ndio ameingia darasa la saba, siku hiyo nyumbani kwao walitembelewa na mgeni, ambaye alizungumza na shangazi yake kisha akaitwa.

“Yule mgeni mbele ya shangazi aliniambia yeye ni mjomba wangu, akitoka kuzaliwa mama yangu anafuata yeye, amehamishiwa kikazi hapa Morogoro. Aliniambia katumwa na mama yangu aje anitafute, pale Kichangani ukoo wetu ulikuwa ni maarufu, hivyo hakupata tabu kufika kwa maelekezo ya dada yake (mama yake Sele) aliyewahi kuishi kule kabla ya kutengana na baba nikiwa mdogo sana.

“Siku hiyo ilikuwa ni mshangao, tena mbele ya shangazi yangu yuleyule aliyeniambia mama amefariki, mjomba akaniambia mama yuko hai na anaishi Moshi, amemtuma afuatilie na kujua ninaendeleaje, japo naye alikuwa na wasiwasi wa namna nitakavyompokea kutokana na ukweli, dada yake aliniacha mdogo, hakuna aliyejali kuhusu mimi hata baada ya baba yangu kufariki.

“Mazingira aliyonikuta nayo pale alilazimika kunichukua na kwenda kuishi nami kwake kambini Mzinga alipokuwa akiishi.”

Anasema aliyafurahia maisha aliyokutana nayo kwa mjomba yake, kwani mwanzo Kichangani alikuwa na maisha ya hovyo, kule kwa mjomba mambo yakabadilika.

“Nimefanya mitihani yangu ya kuhitimu darasa la saba nikiwa kwenye maisha mazuri, nilipohamia kwa mjomba kwa mara ya kwanza hata chai nilianza kunywa, unatoka shule unakuta chakula, jambo ambalo nikiwa mdogo sikuwahi kukutana nalo kabisa,” anakumbuka.

Anaeleza siku alipokutana na mama yake, alikuwa amerejea kutoka shuleni, ilikuwa ni kipindi anakaribia kufanya mitihani yake ya kuhitimu darasa la saba.

“Nilitoka shuleni nikamkuta amekaa sebuleni pale kwa mjomba, nilimuona tu ni mtu, alikuwa anakula, sikumfahamu ni nani, nilimsalimia na kuendelea na mambo yangu, mke wa mjomba akanifuata na kuniambia unamuona yule mwanamke aliyekaa pale, huyo ndiyo mama yako mzazi.

“Wakati huo tayari nilishakuwa na moyo fulani hivi mgumu kutokana na mazingira niliyopitia, moyo wangu ulishakuwa na ganzi, sikuhisi chochote, nilimuangalia tu, nikajisikia huzuni sana,” anasema Afande Sele na kuongeza;

“Wakati huo alikwishatoka kwenye ajira amerudi kijijini kule Moshi, mama yangu ni Mchaga, hivyo alikuwa anahitaji sasa kukaa na watoto wake, hata hivyo sikuwa na namna maana ndiye mama yangu na nimekutanishwa naye japo nilifadhaika sana nilipomuona,” anasema.

Anasema, alipomaliza mitihani yake ya mwisho, kwa mara ya kwanza sasa alikwenda Moshi, ambako alikutana na mjomba wake mwingine akamchukua.

“Ni kama walihitaji kujisafisha kutokana na mazingira waliyoniacha tangu utoto, yule mjomba wangu naye alikuwa vizuri kiuchumi, aliamua kunisomesha.

“Aliniambia siku nyingi sikuwa nao na maisha yangu ya awali tayari walishayajua yalivyokuwa magumu, dada yao aliondoka miaka miwili baadaye baba yangu akafariki, mama yangu wala ndugu yake yeyote hawakuja kwenye msiba wala kujua naishije baada ya kifo cha baba, hivyo ni kama nafsi ziliwasuta, wakawa wanataka kuonyesha walikosea.”

Anasema alipata shule nzuri na kuanza kidato cha kwanza kule Moshi, lakini hakuyafaidi hayo maisha muda mfupi baada ya kumfahamu mama yake.

“Shangazi yangu yule aliyejimilikisha mali za familia na kunichukua mwanzo alileta shida, alitaka nirudi Kichangani, kwenye maisha yangu ya zamani,” anasema kwa sauti ya simanzi kidogo na kuendelea; “Ni kama alitaka tu kuniharibia, vilianza vitisho ikaonekana mimi nikibaki Moshi basi nakaribia kufa, alizungumza vitu vingi akihusisha na mambo ya kishirikina ambayo kule uchagani hayakuwepo kabisa.”

Anasema mama yake, licha ya kuwa mlokole, alikuwa mwoga, alilazimika kumuachia Afande Sele arudi upande wa baba yake baada ya kupewa vitisho.

“Mama alikuwa mcha Mungu, lakini aliamini ushirikina upo, wakati akiwa na baba Kichangani, aliniambia kuna vitu alikuwa akiviona, hivyo baada ya kauli ya shangazi akitaka nirudi akawa na hofu ukizingatia na namna alivyoishi nao awali, alikuwa akiona vitu vingi ajabuajabu, aliwaambia kaka zake waniache nirudi kwetu.

“Iliniumiza sana, lakini mama mwenyewe amelazimika iwe hivyo nafanyaje? Nikarudi kwenye maisha yangu ya awali kule Kichangani,” anasema.

Itaendelea kesho...