Mkakati wa kuongeza thamani ya alizeti, Tanzania itajitegemea kwa mafuta ya kula

Muktasari:
Kwa kuangalia historia, bila shaka hilo linawezekana.
Kwa mujibu wa wadau wa kilimo, kabla ya uhuru nchi za Afrika Mashariki zilizalisha mafuta ya kula ya kutosheleza na hatimaye kuziuzia Rwanda, DRC (Zaire kipindi hicho), Malawi pamoja na kusafirisha nje ya Afrika.
Hivi inawezekana Tanzania kuacha au kupunguza uagizaji wa mafuta ya kula na badala yake kuzalisha bidhaa hiyo hapahapa kutokana na alizeti hadi kuuza nje ya nchi?
Kwa kuangalia historia, bila shaka hilo linawezekana.
Kwa mujibu wa wadau wa kilimo, kabla ya uhuru nchi za Afrika Mashariki zilizalisha mafuta ya kula ya kutosheleza na hatimaye kuziuzia Rwanda, DRC (Zaire kipindi hicho), Malawi pamoja na kusafirisha nje ya Afrika.
Kwa Tanzania, mambo yaliharibika miaka ya 1980 baada ya kampuni zilizokuwa zinajishughulisha na mbegu za mafuta kufunga biashara baada ya Serikali kuondoa kodi kwenye mafuta yaliyoagizwa kutoka nje.
Hali hiyo iliua kabisa uzalishaji wa mbegu zinazozalisha mafuta.
Malaysia na Indonesia zikawa wauzaji wakubwa wa mafuta ya kula baada ya kushusha bei zake na hatimaye kuua kabisa kilimo cha mbegu zinazotoa mafuta ya kula Tanzania na duniani kwa ujumla.
Katika miaka ya hivi karibuni, Tanzania ilianzisha ushuru wa asilimia 10 katika mafuta yanayoingizwa ili kulinda wakulima na wazalishaji wa mafuta nchini, kwa mujibu wa kampuni ya Meru Agro.
Mkurugezi Mtendaji wa kampuni hiyo, Chacha Watanga anasema kwa sasa kuna mwitikio chanya kuhusu uzalishaji wa mafuta hivyo ni jukumu la nchi kuongeza uzalishaji wa mbegu zinazotoa mafuta kama vile alizeti ili kukidhi mahitaji ya ndani na hatimaye kuuza nje ya nchi.
“Hii itasaidia kutufanya nchi ya viwanda badala ya kuwa soko la bidhaa za wenzetu tu,” anasema Chacha.
Huenda kilimo cha alizeti kikapanda thamani na kuongeza kipato kwa wazalishaji baada ya Taasisi ya Maendeleo ya Masoko ya Kilimo (AMDT) kuandaa mkakati utakaoboresha masoko na mazingira ya biashara ya zao hili.
AMDT ilianzishwa na Serikali za Denmark, Uswisi, Ireland na Sweden kwa ajili ya kuongeza kipato na ajira kwa vijana, wanawake na wanaume masikini. Inatarajia kuimarisha mnyororo wa thamani wa alizeti kama njia mojawapo ya kufikia malengo ya kumkomboa mwananchi kutoka kwenye umasikini. Mpango huu unaotekelezwa kwa miaka kumi unatarajia kuboresha uzalishaji wa alizeti na kuongeza masoko ya mbegu bora kwa kilimo cha mkataba ambacho kitamhakikishia mkulima soko.
AMDT inajihusisha na mahindi, alizeti na kunde katika mnyororo wa thamani ya mazao hayo, lakini kwa mujibu wa tangazo la hivi karibuni lina mpango maalumu kwa ajili ya alizeti.
Sasa shirika hili linatafuta mashirika mengine na kampuni binafsi zijitokeze ili washirikiane kuhakikisha upatikanaji wa mbegu bora za alizeti na kujenga uhusiano wa kimkataba baina ya wakulima wadogo na wananuzi wa zao hili linalotumika kutengeza mafuta ya kula.
Tanzania inatajwa kuongeza uzalishaji wa alizeti mwaka hadi mwaka, lakini bado haijafikia uwezo wa kuzalisha inaotakiwa kuwa nao kutokana na changamoto zilizopo katika upatikanaji wa mbegu pamoja na vikwazo vya kimfumo vilivyopo sokoni.
Kwa mujibu wa ripoti ya chama cha wanaojihusisha na mbegu za mafuta ya kula Tanzania (Teosa), ipo mikoa 15 inayolima alizeti kwa wingi nchini, lakini karibu asilimia 40 inatoka mkoani Singida.
Ripoti hiyo ya mwaka 2012 inakadiria uzalishaji wa alizeti ulikua kwa asilimia 34 katika msimu wa mwaka 2011/12.
Hata hivyo, wakulima wengi wanaaminika kutumia mbegu zinazojulikana kama Open Pollinated seed Varieties (OPV) ambazo zimezunguka kwa muda mrefu kiasi cha kupoteza uwezo wake wa kuongeza mavuno na kumnufaisha mkulima.
Ripoti hiyo inatolea mfano Wilaya ya Kondoa ambako wakulima huzalisha alizeti katika mashamba madogo, ya kati na makubwa, lakini hukutana na changamoto ya masoko pamoja na fedha za kuendeleza uzalishaji.
Licha ya kuwapo alizeti na mbegu zingine za kuzalisha mafuta ya kula, Tanzania inaagiza asilimia 50 ya mafuta kutoka nje ya nchi kwa matumizi yake kila mwaka. Mbegu muhimu zinazotumika kuzalisha mafuta ya kula ni pamoja na alizeti yenyewe, karanga na ufuta.
Kumekuwapo na nia ya serikali na wadau wengine wa sekta binafsi kutaka kuendeleza ushindani wa vyanzo vya mafuta ya kula, lakini ripoti ya Teosa inasema bado hakuna sera, mikakakti wala mipango madhubuti ya kuwezesha hilo kutokea.
Hata hivyo, mpango huu wa AMDT kuhusu alizeti huenda ukafufua upya matarajio ya zao hili na kupunguza umasikini wa wakulima kama inavyokusudiwa.
Maeneo muhimu
Awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mkakati wa kuongeza thamani ya alizeti unatarajia kuhusisha maeneo ya Dodoma na Morogoro; Mbeya na Rukwa; Lindi na Mtwara; Iringa na Njombe; Shinyanga na Singida na Manyara.
Mkakati huu unaotekelezwa kuanzia mwaka 2016 hadi 2020 unatarajiwa kuchochea soko la mbegu bora kwa kushawishi sekta binafsi kuzizalisha zaidi mbegu hizo. Lengo lililopo ni kuzalisha aina nne had sita za mbegu mpya kufikia mwaka 2020.
Aidha, mkakati huu unalenga kusaidia upatikananji wa mbegu bora kwa wakulima wadogo na kujenga mazingira yatakayowezesha hali hiyo kuwa endelevu.
Lengo jingine la mkakati wa kuongeza thamani na uzalishaji wa alizeti ni kujenga mazingira ya kilimo cha mkataba baina ya wakulima wadogo, wa kati na wazalishaiji wa mafuta au wanunuzi wa zao hilo.
Katika kutekeleza hilo, mradi utahakikisha kuwapo kwa huduma muhimu kama vile ushauri, taarifa za masoko na huduma za kifedha kwa wakulima.
Pia, vyama vya ushirika vya wakulima wa alizeti vitajengewa uwezo wa kujiendesha, kushawishi mabadiliko ya sera na kusimamia kilimo cha mkataba kinachopendekezwa.
Ukurasa wa mazingira bora ya kufanya biashara umerudi kwenye gazeti la Mwananchi kila Alhamisi ukiwa na lengo la kuunga mkono jitihada za wajasiriamali nchini. Kwa maoni tuma ujumbe mfupi kwenda namba 0786240172 ukianza na neno RB kwa gharama za kawaida za ujumbe au baruapepe: [email protected]