Mtoto anapenda soka? Njia sahihi za kumlinda

Muktasari:

Takribani wiki moja imepita tangu michuano ya Kombe la Dunia inayoshirikisha mataifa 32 ianze huko Qatar, huku macho na masikio ya watu wengi ulimwenguni, wakiwamo Watanzania yakiendelea kuelekezwa nchini humo.

Takribani wiki moja imepita tangu michuano ya Kombe la Dunia inayoshirikisha mataifa 32 ianze huko Qatar, huku macho na masikio ya watu wengi ulimwenguni, wakiwamo Watanzania yakiendelea kuelekezwa nchini humo.

Timu hizo zimeanza kushuka uwanjani kwa kuchuana kutafuta mshindi atakayeondoka na kombe hilo lenye heshima zaidi inapozungumziwa fani ya mpira wa miguu.

Huu ni wakati ambao mashabiki wa mpira wa miguu kutoka mataifa mbalimbali huungana kushabikia timu hata kama si za mataifa yao, kikubwa hapa ni burudani ya soka, ikizingatiwa ligi zote duniani husimama kupisha michuano hiyo.

Kama ilivyo kwa mataifa mengine, Tanzania nayo ina mashabiki wa mchezo huu wanawake kwa wanaume, wakiwamo watoto wa kiume wenye shauku ya kuwa wanamichezo na wanaopenda fani, wakiwamo watoto wa kike pia.

Kuanza kwa michuano hii kumeleta furaha kubwa kwa wapenzi wa mpira wa miguu, hasa wanaume, hivyo hiki ni kipindi ambacho wazazi wanatakiwa kuongeza umakini kuanzia kwa watu kwenye kaya hadi mali ndani ya kaya.

Hatari zaidi katika kipindi hiki ni michezo hii kuonyeshwa nyakati za jioni na usiku wa saa nne, hivyo wakati mwingine kuwalazimu wafuatiliaji wasio na ving’amuzi vinavyowawezesha kutazama nyumbani kwenda kwenye ‘vibanda umiza’ ambako huko hukutana na mashabiki wengine.

Ushawishi wa kuangalia mechi baada ya michuano hii kuanza huenda ikachochea watoto, hasa wa kiume kujiingiza kwenye vibanda hivyo ili kupata umakini kutoka kwa mashabiki ‘kindakindaki’ wa mpira huu.

Hata hivyo, katika kuepuka vitendo vya kikatili mtandao wa commonsensemedia.org umesema ni vyema familia kuungana kipindi hiki kutazama mpira pamoja ili kuwafundisha watoto vitu mbalimbali kuhusiana na mpira wa miguu na maisha kwa jumla.

“Kutazama michezo pamoja hukuwezesha kuwaonyesha watoto wako mifano ya stadi za maisha. Kuzingatia kile kinachotokea katika mchezo, kama vile jinsi wachezaji wanavyofanya au kuonyesha hisia zao, hii pia huwafunza kuwa pamoja katika kazi,” unaeleza mtandao huo.

Hivyo, umakini wa kuwaangaliwa watoto hawa unapaswa kuanzia ndani ya familia ili kuhakikisha watoto ambao ni mashabiki wazuri wa mpira wa miguu wanakuwa salama dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia ambavyo vimekuwa vikishika kasi, huku takwimu zikionyesha hali inazidi kuwa mbaya.

Takwimu zilizotolewa Novemba mwaka huu katika mkutano wa maofisa maendeleo ya jamii uliofanyika Dodoma, zinaonyesha kuanzia Januari hadi Septemba 2022 watoto wa kiume 1,044 wamelawitiwa, sawa na wastani watoto 116 kwa mwezi, hivyo kundi hili lipo kwenye hatari zaidi kwa sasa.

Upande wa ubakaji takwimu zinaonyesha wastani wa watoto wa kike 18 wamebakwa kwa siku.


Kutoka ustawi wa jamii

Akizungumza na Mwananchi, Ofisa Ustawi wa Jamii Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Twaha Kibalula anasema Kombe la Dunia limekuja wakati ambao kuna ongezeko la matukio ya ukatili wa kingono dhidi ya watoto, hasa wa kiume hivyo ni muhimu kwa wazazi kuwa macho.

“Michezo ni sehemu muhimu ya makuzi na maendeleo ya mtoto, pamoja na hilo wazazi wana jukumu la kulinda watoto dhidi ya hali yoyote ambayo haitakuwa nzuri kwake, mfano vitendo vya ukatili ambavyo vimeshika kasi kwa sasa,” anasema Kibalula.

“Taarifa zinaonyesha kwa kiasi kikubwa vitendo hivi vinafanywa na watu wa karibu na tunaowaamini, sasa inapokuja hili suala la kuangalia mpira usiku niwaombe wazazi tuongeze umakini hata kama mtoto wako anaangalia mpira nyumbani usiku mwingi, basi hakikisha na wewe upo, haya mambo ya kuamini watu wengine tujiulize mara mbili kabla ya kuruhusu.”

Kibalula anasisitiza pia umuhimu wa wazazi kuhakikisha nyakati za usiku watoto hawatoki nje ya mazingira ya nyumbani kwa kuwa huko kunatengeneza mazingira hatarishi ya kuangukia kwenye mikono ya watu wabaya.

“Usiruhusu mtoto akaangalie mpira nje ya nyumbani tena usiku, wanaenda kwenye ‘vibanda umiza’ ambavyo katika wizara tumeshaviweka kwenye orodha ya maeneo hatarishi kwa watoto. Vibanda hivi vingi havipo kwenye maeneo rasmi, hivyo sio salama wanaingia watu wa kila aina,” anasema Kibalula.

“Huwezi kumbaini mtu mbaya na mwema wakiwa kwenye hivyo vibanda, lakini ukweli ni kwamba sio salama na vitu vingi vinafanyika huko, nisisitize watoto hawaruhusiwi kwenda kwenye hivi vibanda iwe mchana au usiku. Hakuna anayesimamia maudhui yanayoonyeshwa huko, sasa ni jukumu letu wazazi kusimamia hili na ikizingatiwa kwamba licha ya kombe la dunia msimu wa likizo za wanafunzi nao unakaribia.”


Wazazi je?

Hilo linaungwa mkono na Esha Omary, ambaye ni mzazi anayepigia chapuo umuhimu wa wazazi kuongeza umakini kwenye kuangalia ustawi wa watoto, hasa katika kipindi hiki kuelekea mwisho wa mwaka ambapo matukio mengi hutokea.

“Ukiacha hayo masuala ya mpira, tunaelekea mwisho wa mwaka, mambo ni mengi, mtaani wanaingia watu wapya hivyo ni muhimu kuongeza umakini kuwaangalia watoto wote, awali uangalizi ulikuwa zaidi kwa watoto wa kike lakini sasa tunaona hata watoto wa kiume wako hatarini,” anasema Esha.

“Tusiwaache watoto peke yao kwa muda mrefu, yaani mzazi umekaa hujui mwanao yuko wapi au unamtuma usiku iwe mtoto wa kike au wa kiume hakuna sababu ya kumruhusu kutembea usiku, ni kumuweka katika mazingira hatarishi, hebu wazazi wenzangu tushtushwe na haya matukio na tuwe mstari wa mbele kuwalinda watoto wetu.”

Wakati Esha akieleza hayo, Alex Maganga anaweka msisitizo wake katika kuhakikisha familia hazisambaratiki wakati huu kwa kuwa uzoefu unaonyesha kunatokea migogoro mingi kwa sababu ya kukosa uaminifu.

“Ni kipindi ambacho mambo mengi hutokea, kwa uzoefu ndoa nyingi hupitia kimbunga, wanawake ni wagumu kuwaelewa wenza wao pale wanapowaaga wanaenda kuangalia mpira au wanaporudi usiku wa manane,” anasema Maganga.

“Utakuta mwanamke anakulazimisha uangalie mpira nyumbani kwanza hakuna ile ‘vibe’ kama unayoipata kwenye ‘bar’ au kibandani, halafu pia usumbufu mwingi unaona bora ulazimishe kwenda, ukirudi huko ugomvi, sasa maisha yanakuwa hivi kila siku.

“Hata hivyo pia kuna wanaume hutumia vibaya fursa hii, anaaga anaenda kuangalia mpira kumbe amejibana sehemu, mke akigundua ugomvi ndoa inavunjika familia inasambaratika, ndiyo maana nasema tujitahidi kuepusha vitu hivi visitokee na hilo la kuangalia watoto pia liwe jukumu letu sote.”