NDANI YA BOKSI: Dunia inataka vitu laini kama ngozi ya zari

Muktasari:
- Niliwahi kuandika katika ukurasa huu miaka minne iliyopita. Kuwa dunia ya sasa inamuhitaji zaidi Hamisa Mobetto kuliko Mchungaji Getrude Rwakatare. Wakati huo Mchungaji Lwakatare akiwa bado hai.
Niliwahi kuandika katika ukurasa huu miaka minne iliyopita. Kuwa dunia ya sasa inamuhitaji zaidi Hamisa Mobetto kuliko Mchungaji Getrude Rwakatare. Wakati huo Mchungaji Lwakatare akiwa bado hai.
Wapo walioelewa na ambao hawakuelewa. Hilo halikuwa jukumu langu kuelewesha mtu anayesema bila kuelewa. Wapo wengi wa namna hii ambao ni wazito kuelewa kwa sababu ndio dunia hii inavyowalea.
Lazima tukubali upepo wa mambo tuliyoona ya kijinga siku za nyuma, umekuwa mkali sana na leo unatusukuma kutupeleka unakotaka wenyewe, na sisi tunaenda kama vile maboya baharini.
Mwishoni mwa miaka ya 90, wimbi kubwa la ujio wa magazeti ya udaku lilitawala. Baadaye yakabatizwa jina la ‘Magazeti Pendwa’. Kwa sababu dunia ilikuwa kwenye mapito yake ya kuhitaji vitu vyepesi.
Usafiri ulirahisishwa kwa barabara nzuri na wingi wa gari. Mawasiliano yalilainishwa kwa simu na ‘intaneti’. Mwisho watu wakataka kila kitu kiwe rahisi. Na hata habari wakataka zile rahisi, laini na fupi.
Na habari nyepesi na zisizoumiza kichwa ni zile za kuhusu watu binafsi. Wenye umaarufu au matukio ya kimjini mjini. Udaku ukazalisha mastaa na kuwakuza zaidi waliokuwa mastaa tayari. Yes!
Miaka ile muziki na uigizaji ulizalisha mastaa wachache hata ‘umiss’ wachache. Udaku wa gazeti ukalazimisha kuandika watangazaji wa redio kama sehemu ya mastaa wa mjini. Ikawalipa.
Lakini kupitia udaku, wakazalishwa mastaa wengi zaidi wa kike. Na hii ni kupitia shindano la Miss Tanzania. Mashindano ya urembo yakawa kama kiwanda rasmi cha kuibua watoto wa kike maarufu.
Mwanzo Miss Tanzania tu ndiye aliyejulikana. 1994, Aina Maeda, 1995 Emily Adolf, 1996 Shose Sinare, 1997 Saida Kessy, 1998 Basila Mwanukuzi, 1999 Hoyce Temu. Wale washindi wa pili kushuka chini hawakupata mashavu.
Lakini kuanzia 2000 enzi zile za Jackline Ntuyabaliwe. Hata mshindi wa pili akaanza kupata shavu kubwa. Kina Mercy Galabawa, Irene Kiwia na wenzao. Wakageuka windo la watu wa udaku na kupamba kurasa za magazeti.
Lakini katikati ya mwaka 2000 na 2005. Kipindi cha mwisho ‘amezing’ cha utawala wa ‘Big Ben’ (RIP) awamu ya tatu. Waliibuka mastaa wengi wa kike na kiume. Kwenye umiss, muziki, uigizaji na hata madansa wa bendi maarufu.
Ni wakati ule Bongo, waliiteka Sinta na Juma Nature. Nora na kina Nina. Ni wakati ambao Zay B na Sister P, walifanya dakika zichelewe kuisha. Banza, Ally Choki, Muumini na kina Aisha Madinda walikuwa na dunia yao.
Hawa wote umaarufu wao haukuja kwa bahati mbaya. Walifanya kazi kubwa, zilizojulikana kwanza kabla ya majina yao. Ukisikia Lilian Internet, ukienda na kwenye shoo zao utazima fegi. Walifanya kazi.
Huu ndo wakati ambao Bongo Fleva ilichukua kijiji chote. Kisha ikazima taa zote za dansi, taarabu na uigizaji. Muziki uliongea zaidi kuliko kiki na ‘shoo ofu’. Ndivyo ilivyokuwa kwa tasnia nyingine na sanaa zote.
Lakini leo kuna watu kibao maarufu bila kueleweka shughuli zao. Yaani mtu anaanza kuwa maarufu kisha ndo anaamua kutuaminisha kuwa anaweza kufanya muziki. Au anafaa kuwa mtangazaji au mbunge.
Achana na Wema ambaye dunia yote inajua ni Miss Tanzania wa 2006. Na huo mwaka Miss Tanzania, ilizalisha mastaa wengi sana wa kike. Jokate, Lisa Poulsen, Irene Uwoya na Aunty Eziekiel ambaye hakuingia hata top 10.
Ukicha Bongo Movie, Miss Tanzania ndio wanaongoza kwa kuzalisha sana mastaa wa kike. Zamaradi Mketema ni Miss Mwanza 2007. Uwoya na Jokate wakiwa ni baadhi ya majaji waliompatia ushindi.
Pia Uwoya na Jokate ni zao la Umiss kupitia staa wa filamu, Chuchu Hans. Hata Chuchu pia ni zao la ‘umiss’ akiwa ni Miss Tanga 2005. Yeye na ‘eksi wake’, waliandaa shindano la Miss Temeke lililowaibua Uwoya na Jokate.
Staa wa muziki kwa sasa Lulu Abbas a.k.a Lulu Diva. Kabla ya muziki pia ni staa kutoka kiwanja cha ‘umiss’, ni Miss Pwani namba 2 na Miss Kibaha namba moja wa mwaka 2013. Leo hii ni staa mkubwa wa muziki.
Hamisa Mobeto ni Miss Dar Indian Ocean namba mbili 2011. Akashiriki Miss Tz mwaka huo huo lakini alitoka patupu. 2012 Hamisa alishiriki Miss University Africa na kuingia top 10. Leo ni staa wa muziki aliyezaa na staa wa muziki.
Kuna msanii wa filamu Flora Mvungi, pia naye ni uzao wa shindano la Miss Tanzania. Akiwa ni Miss Pwani na Miss Kanda ya Mashariki wa mwaka 2008. Baadaye akajiegemeza kwenye sanaa ya filamu anakokimbiza hata leo.
Miriam Jolwa, maarufu kama Jini kabula. Alikuwa Miss Kariakoo miaka ya nyuma, ingawa hakutoboa Miss Tanzania Taifa. Rashida Wanjara ni Miss Mara, Miss Kanda ya Ziwa na Top Model Miss Tanzania 2002.
Tumeelewana? Hawa wote ni uzao wa kiwanda cha ulimbwende. Kisha wakatoboa zaidi baada ya majina yao kupaa. Lakini majina yao yalikuja baada ya kufanyia kazi kitu, tofauti na sasa jina linaanza kabla ya kipaji.
Watoto wengi sana wa kike wapo mitandaoni, wana umaarufu sana. Lakini ukitaka kujua umaarufu wao umetokana na nini? Hata muhusika mwenyewe hawezi kuwa na jibu sahihi. Wanajikuta tu wana jina mitandaoni. Basi!
Kesho unamsikia anatangaza wimbo mpya. Au anatangaza uhusiano wake na mtu fulani maarufu. Na mitandao inachafuka kwa habari zao. Na wana habari wapenda mitandao kuliko kazi zao, wanawapa nafasi.
Dunia imeamua kuwa hivyo. Na hiki kitu siyo bahati mbaya. Msingi wa haya ulianza wakati ule wa udaku. Watu wakapenda vitu laini kusoma. Kama walivyopenda kila kitu rahisi rahisi.
Dunia haitaki mambo magumu sana. Dunia haivutiwi na vitu fikirishi. Ndio maana hata maandiko watu wengi husoma kichwa tu cha habari kisha wanatoa hukumu. Hawataki kabisa kusumbua akili na mwili.
Watu wanataka kuletewa kila kitu kiganjani. Ndio maana wanaoweza kuzalisha vitu vya kutazamwa au kusomewa kiganjani hupewa nafasi zaidi dunia ya sasa. Mambo yale magumu, fikirishi na mtambuka hayana nafasi.
Mnaokutana na Jimmy Mafufu a.k.a Kipunje, mpeni salamu nyingi.