NDANI YA BOKSI: Siyo bangi tu, hata video za utupu ni shida kubwa

Harmonize

What you need to know:

Wazee wamecharuka. Wamekasirika. Kifupi wamenuna. Wamefura. Hawataki tena kusikia masela wakiimba na kusifia ganja. Yes! Ni ganja pekee ndio dawa za kulevya zenye promo kubwa kwenye ngoma za Bongofleva. Kuanzia enzi za mikasi mpaka kikohozi cha Konde.

Wazee wamecharuka. Wamekasirika. Kifupi wamenuna. Wamefura. Hawataki tena kusikia masela wakiimba na kusifia ganja. Yes! Ni ganja pekee ndio dawa za kulevya zenye promo kubwa kwenye ngoma za Bongofleva. Kuanzia enzi za mikasi mpaka kikohozi cha Konde.

Mtu mwenye akili yeyote ataunga mkono hilo katazo lao. Lakini hawa madingi zetu mbona wanaona hili na kuacha lile? Wao ni ganja tu walizoona zinaathiri na kupotosha jamii yetu? Maneno ya kusifu ganja na video za utupu kipi kinaonekana kwa wingi?

Video za wasanii wengi zinatumia miili ya dada zetu kama kivutio. Na siyo hizo video tu, hata mapozi picha mitandaoni zinazingua tu kama ngoma za ganja. Kwa wakware wakitazama video za dada zetu, lazima wahamasike kujisajili katika vitabu vya Dar to Dar. Hata uchezaji wa baadhi ya nyimbo na hasa hizi singeli. Ni tatizo kubwa ambao linafaa kutazamwa kama zile promo za ganja. Tukiamua kusimamia kweli hizi taratibu za kimaadili, tutajikuta tupo enzi za kina David Wakati na Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD). Maana kila kona uozo mtupu wa maadili.

Nyimbo za taarabu asilimia mia moja, wana wake wanajisifu kuchukuliana mabwana. Kwani kubeba mume wa mtu kimaadili ni jambo zuri? Au wanatazama ngoma za Bongofleva tu?

Sasa tunapotazama kikohozi cha Konde kama shida kubwa kimaadili. Kama kweli kusifia ganja ni upotoshaji wa maadili kijamii. Basi zile singeli ukizifuatilia kwa kina unaweza kukuta ni nyimbo mbili au tatu zinazofaa kuchezwa au kusikika eneo la wazi.

Wanamuziki wamecharuka na video. Na watengenezaji wa video nao hivi sasa wako vizuri. Ni ngumu sana kukutana na video mbovu kwa muziki wa sasa. Zamani wimbo bora ulikuwa haufanyiwi video hapa Bongo. Nyimbo zilikuwa nzuri kuliko video, kitu ambacho wasanii waliamini kufanya video ni kuharibu wimbo wenyewe. Hatukuwa na vifaa vya kisasa na watengenezaji wenye elimu na kazi hiyo. Wengi walifanya kwa mizuka na siyo taaluma. Hii leo ukituletea video za kipaimara na komunio kama siyo kicheni pati utachonga viazi. Hutapata kazi za wasanii na hata vituo vya runinga haviwezi kucheza video yako.

Muziki ni shamba lenye mavuno kuliko sanaa yoyote Bongo kwa sasa. Kwenye muziki kuna utajiri na ajira za kutosha kama uwekezaji utakuwa mkubwa. Wasanii kama Snura na Shilole walishtuka mapema kabla ya jua la utosi kwenye filamu. Wakapita kushoto wakaliacha soko la filamu kulia. Kwenye sanaa ya filamu hawakupata kile wanachopata hivi sasa kwenye muziki. Hata mvuto wao kwa jamii siyo kwa kiwango kile. Ndiyo maana wasanii wenyewe wanasikika na kufuatiliwa kwa vitu vya nje ya sanaa yao. Jacquline Wolper utamsikia na kumsoma kwa uhusiano wake ma Rich Mitindo. Huku Wema jina lake likitajwa kwa matukio yake na Whozu. Katika mazingira haya ni ngumu Wema kufurahia kuitwa msanii wa filamu kama ambavyo Shilole anavyochekelea kuitwa mwanamuziki. Snura jina lake na sura vina uhusiano wa karibu na kamera za waandishi kuliko Johari. Kuna kitu kipo katika muziki na kwenye filamu hakipo. Tuyaache hayo. Biashara yoyote inapokubalika huwezi kuzuia ushindani, hilo lipo katika muziki pia. Upo ushindani kwenye utunzi, shoo mpaka video. Ndiyo maana wanamuziki hivi sasa wanapanda ndege kufuata ubora wa video Afrika Kusini na kwingineko.

Lengo ni kutaka kuteka soko la kimataifa kwa video nzuri. Wachache wamefanikiwa katika hilo. Safari ya Diamond kimataifa ilifunguliwa na video kali. Achana na midundo yake. Puuzia sauti yenyewe mpaka ‘melodi’. Weka pembeni ubora wa shairi. Video yenyewe ya wimbo wake ‘Number One’ ni ya kiwango cha juu.

Kupitia ubora wa video kama ile ilikuwa rahisi kumshawishi Davido akaelewa. Ndicho kilichotokea kwa Iyanya na wengineo aliofanya nao kazi. Mbali ya kufanya kazi na wanamuziki hao nyota wa Kinaijeria na kwingineko, pia mfereji wa kutiririsha tuzo za kimataifa ulizibuliwa na video hiyo.

Yawezekana kulikuwa na mengi zaidi yaliyochangia kufanya nao kazi, lakini ubora wa video ile ulichangia kwa kiasi kikubwa. Msanii wa kimataifa hawezi kufanya kazi na msanii yeyote bila kuwepo na sababu. Ilikuwa video ya kimataifa. Ambayo hata Diddy angeweza kupoteza muda kuitazama kwa sekunde kadhaa.

Ila kama ilivyowahi kutokea kwa wale wasanii wa Bongo Movie. Kuna kitu kibaya kinaanza kushamiri kwa wasanii wengi wa Bongofleva. Zamani Bongo Movie waliposema wanatengeneza filamu ya kimataifa, waliamini ni kuigiza uzungu mwingi, kuanzia matendo, mavazi, picha ya ‘kava’, jina la filamu na viingereza vingi vya kunyapianyapia ndani. Ni kama leo katika Bongofleva. Video zinazoitwa za kimataifa basi ujue ndani kuna vimini na mikao ya ajabu na nguo za faragha.

Kutazama video zao ni lazima ujihakikishie hakuna unayemheshimu. Vijana wa sasa ni kama ubunifu umeisha au wanakurupuka bila kujua dhana ya video ya kimataifa. Ubunifu na kuvaa utupu ni vitu viwili tofauti. Unaweza kuimba mtupu kama ulivyozaliwa na ukaonekana umefanya kitu ‘loco’. Na unaweza kuimba ukiwa ndani ya vazi la maadili ukaitwa wa kimataifa. Kuna uhusiano gani wa kuvaa vichupi katika video na ukimataifa mnaoutaja? Miriam Makeba ni mwanamuziki wa kimataifa mbona hana video za utupu? Marehemu Whitney Huston mbona alikuwa wa kimataifa bila vichupi? Msijitoe akili kwa kuacha tupu zenu wazi kwenye video ukidhani utapaa na kuwa kama Rihanna. Kifupi washua wetu wanashangaza sana kuona ganja ndio msala zaidi ya maungo ya mama zetu kuachwa wazi. Moja kati ya wanamuziki bora Afrika Mashariki ni Wahu, mke wa Nameless. Vipi video zake? Kuna vichupi kama vilivyo katika video zenu za Manzese? Kuna kitu mnatakiwa kufikiri kwanza. Mmebeba maana na heshima ya Watanzania. Sisi wote wajinga, lakini sio wa kitu kimoja. Kupanuka kwa teknolojia lisiwe lango la kuondoa kinyemela maadili kwenye jamii yetu kama makontena ya makinikia bandarini.

Si lazima uvae kama Beyonce ili uwe wa kimataifa. Kuna mengi ya maana ya kuiga. Lakini siyo kwa kuacha maungo wazi kama mbwa. Kina Chakachaka hawakuweka mapaja wazi ili watajwe kama ni ‘intaneshino atisti’.