Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Maswali ni mengi kuliko majibu deni la taifa

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba akizungumza na Jumuiya ya wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo, Jijini Dar es Salaam jana, baada ya kusikiliza changamoto zinazowakabili na kuzipatia ufumbuzi ikiwemo msuguano baina yao na Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA kuhusu masuala ya kodi na risiti za kieletroniki. Picha Wizara ya Fedha

Muktasari:

  • Kwa rasilimali zilizopo Tanzania inapaswa kuwa miongoni mwa mataifa yenye uchumi imara zaidi kuliko ilivyo sasa

Nchi ilipata mshtuko. Ni kufuatia taarifa ya Deni la Taifa kukua hadi kufikia Sh91 trilioni. Kuna watu walihoji ni kwa nini imekuwa hivyo? Mbona Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imeweka rekodi ya juu zaidi ya kukopa?

Rais Samia anaelekea kutimiza mwaka mmoja na miezi tisa ofisini. Kipindi anapokea kijiti kutoka kwa Dk John Magufuli, deni la Serikali lilitajwa kuwa Sh64.5 trilioni. Sasa deni kufika Sh91 trilioni ndani ya muda usiofika miaka miwili ni hatari mno.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba, aliandika mtandaoni kufafanua kuhusu deni la Sh91 trilioni. Akasemaa deni la Serikali Kuu na Mashirika ya Umma ni Sh46.6 trilioni. Mikopo ya hati fungani za muda mrefu na mfupi (T-Bills na T-Bonds), Sh26.6 trilioni.

Mwigulu alieleza kuwa deni la sekta binafsi limekuwa hadi kufikia Sh17 trilioni. Hivyo, ukijumlisha deni la serikali, mashirika ya umma, mikopo ya hati fungani pamoja na deni la sekta binafsi ndio unapata Sh91 trilioni.

Kwa kuchukua ufafanuzi wa Mwigulu, bado hesabu hailingani. Sh46.6 + 26.6 + 17, jawabu ni 90.2 trilioni. Wakati deni linatajwa kuwa limefikia 91 trilioni. Hivyo, ufafanuzi wa Mwigulu bado haujataja Sh1 trilioni ipo wapi ili kupata ulinganifu wa Sh91 trilioni.

Mwigulu alisema deni la sekta binafsi ni dola 7.3 bilioni, ambazo ndizo Sh17 trilioni. Hata hivyo, alisema linaweza kufika mpaka Sh20 bilioni kulingana tofauti ya mabadilishano ya sarafu

Dola ya Marekani kwa sasa inabadilishwa kwa wastani wa Sh2,330 mpaka 2,340. Hata kama utaibadilisha kwa Sh2,350, dola 7.3 bilioni itakuwa Sh17.2 trilioni. Hivyo jumla kuu itakuwa Sh90.4 trilioni. Mpaka hapo ufafanuzi wa Mwigulu bado umeacha maswali.

Kutozingatia utoaji taarifa

Mwigulu kwa namna alivyotoa ufafanuzi kuhusu deni la Taifa kufikia Sh91 trilioni, ni kama aliona ni kitu kidogo. Kwamba watu waliibua hoja naye akawajibu kuwatuliza.

Bila kuzingatia kuwa suala hilo liliibua taharuki, hivyo lilitakiwa kujibiwa kwa namna ambayo kusingebaki na maswali.

Nini kilishindikana kufanya mkutano na waandishi wa habari ili kueleza kinagaubaga kuhusu mgawanyo wa deni la taifa? Watanzania wangapi wanajua kutofautisha kati ya Deni Kuu la Kigeni (Gross External Debt) na Deni la Taifa (National Debt) ambalo pia huitwa Deni la Serikali au Deni la Umma (Public Debt)?

Siku zote viongozi wenye dhamana hasa serikalini, wanapaswa kuzingatia kwamba taarifa zina nguvu. Haifai kudharau agenda yoyote inayoibuliwa. Mwigulu kama msemaji mkuu wa Wizara ya Fedha, alipaswa kutoa majibu ya kina.

Serikali haioni wajibu wa kufanya kazi kwa takwimu zilizohakikiwa? Ukisoma taarifa ya Mwigulu, unaona kuwa kuna maeneo hana uhakika. Ndio maana alitumia maneno “karibu trilioni 17 hadi trilioni 20”, vilevile sehemu nyingi alitumia makadirio badala ya tarakimu halisi.

Kilichoonekana, Mwigulu alijibu haraka ili kutuliza hali ya hewa. Matokeo yake akawa anatumia makadirio na kusababisha tarakimu zake zisioane na kiwango halisi cha deni kinachotajwa. Ni muhimu sana kujenga utulivu katika kujibu hoja zinazoibuliwa dhidi ya serikali.

Kipindi Deni la Taifa likitajwa kufikia Sh91 trilioni na mashambulizi dhidi ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwa amekopa sana ndani ya muda mfupi, Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa, alikuwa anajirekodi video akipanda Mlima Kilimanjaro. Alikuwa pamoja na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Tehama, Nape Nnauye.

Msigwa hakuonekana kabisa kuguswa na mjadala wa Deni la Taifa. Kwa nafasi yake, ndiye alipaswa kukusanya taarifa kutoka Wizara ya Fedha ili kuzungumza na umma wa Watanzania kuhusu usahihi wa kuongezeka wa Deni la Taifa.

Kuna mahali unafika unaona kuwa tatizo kubwa ni utoaji wa taarifa sahihi na kwa wakati mwafaka. Msigwa hajui kuwa kila hoja dhidi ya Serikali, ni yeye na ofisi yake ndio wenye wajibu wa kujibu ili kusafisha hali ya hewa.

Kwa nini deni linakua?

Kwanza, Mwigulu na wahusika wengine wanapaswa kujua kuwa Deni la Serikali ndio mara nyingi hutambulika kama Deni la Taifa. Hii sio tafsiri ya Tanzania, bali ulimwenguni kote. Kwamba taifa haliwezi kudaiwa kwa deni la taasisi binafsi.

Kampuni binafsi hulazimika kukopa mitaji nje ya nchi ili kukua. Taarifa za kimataifa, hasa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), itaonekana nchi husika inadaiwa, kwa maana taasisi binafsi zenye usajili kwenye nchi hiyo zimekopa.

Kutokuchanganya mambo, madeni ya Serikali na ya taasisi binafsi nje ya nchi, huwekwa kwenye kipengele cha jumla kuu ya madeni ya nje (gross external debt). Kwa maana ya kiwango ambacho nchi inadaiwa kimataifa; serikali na taasisi zake pamoja na sekta binafsi.

Deni la Serikali hujumuisha pia mikopo ya ndani. Wakati sekta binafsi zikikopa kwenye benki za ndani, haiwezi kuathiri chochote kwenye namba za ongezeko la deni la umma. Hivyo, mpaka hapo bado kuna uhitaji wa ufafanuzi usioacha maswali.

Swali la msingi kwa nini Serikali inakopa? Jibu ni kuwa mikopo hasa kutoka nje ya nchi ni njia rahisi zaidi kwa Serikali kupata fedha za kuwekeza kwenye ukuaji wa uchumi na kutekeleza miradi ya maendeleo.

Na wanasiasa wengi, hukimbilia kukopa kwa sababu huepukana na mtihani wa kuongeza kodi kwa wananchi. Sasa, kuondoa mzigo kwa wapigakura, wanasiasa hukimbilia kukopa ili kufanikisha malengo ya Serikali.

Jitihada za Rais Samia

Rais Samia ameingia madarakani akikuta kuna miradi mingi ipo njiani. Kuanzia ujenzi wa reli ya Standard Gauge (SGR), Bwawa la Kuzalisha Umeme la Julius Nyerere (Stiegler’s Gorge), Barabara za Mwendokasi Dar es Salaam na kadhalika.

Takwimu za Benki ya Dunia zinaonyesha kuwa mwaka 2020, uchumi wa Tanzania ulikuwa unakua kwa asilimia 2, wakati Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), ilionesha kasi ya uchumi ilikuwa asilimia 2.5.

Rais Samia aliingia madarakani Machi 19, 2021, hivyo alikuta nchi ikiwa dhaifu, ikisuasua kiuchumi. Changamoto ya ugonjwa wa Covid-19 na sera zilizokuwepo kwa sehemu kubwa zilichangia kudidimiza uchumi.

Rais Samia alifanikiwa ndani ya muda mfupi kuivusha Tanzania kutoka kwenye pigo la Covid-19. Tanzania ikapanda kutoka asilimia 2 ya Benki ya Dunia na 2.5 ya AfDB mpaka asilimia 4, kisha kufikia asilimia 6.9, kwa mujibu wa Mamlaka ya Taifa ya Takwimu (NBS).

Katika mazingira yaliyokuwepo, ilikuwa vigumu mno kutoka kwenye uchumi uliokuwa unakua kwa asilimia 2.5, tena Serikali ikiwa inadaiwa miradi mingi ya kutekeleza, bila kukopa. Hivyo, Serikali inaendelea kukopa ili kukamilisha miradi mingi ya mkakati, vilevile kwa mambo mengine.

Taarifa ya Tamisemi ilieleza kuwa mwaka 2021, Serikali ilijenga shule mpya za sekondari 231 na madarasa 5,000, wakati mwaka 2022, madarasa mapya 8,000 yanajengwa. Haya yote ni matokeo ya fedha za kukopa. Wahusika wanapaswa kutoka na kueleza mikopo imetumikaje na faida zake.

Angalizo la kukopa sana

Nape Nnauye, kabla hajateuliwa kuwa Waziri wa Habari, aliwahi kujenga hoja bungeni kutaka mikopo mikubwa ambayo Serikali ilikopa kipindi cha uongozi wa Magufuli, ichunguzwe ilivyopatikana na ilivyotumika. Kwa maana hakukuwa na uwazi.

Ni kwa sababu Nape aliona kuwa ndani ya miaka mitano, Magufuli alikopa fedha nyingi na kutengeneza deni kubwa kuwazidi marais wote waliomtangulia kwa kuwaweka pamoja.

Magufuli alipoingia ofisini alikuta Deni la Umma ni Sh31 trilioni, yeye akaacha likiwa Sh64.5. Hivyo, yeye peke yake alitengengeneza deni la 33.5.

Katika hoja yake, Nape alisema kwa vile miradi ingechelewa kukamilika, wakati wa marejesho ya mikopo, itabidi kuchukua fedha kwenye miradi ya huduma kama elimu, afya na kadhalika ili kuwalipa wadeni wa nchi. Katika hili Nape alitilia shaka uzalendo wa wachumi ambao walikuwa wakimshauri Rais Magufuli.

Upande wa pili, Nape alionya kuwa nchi inapiga hatua kwenda kuwa isiyokopesheka ikiwa itakopa kwa ajili ya miradi miwili tu; wa kwanza ni ujenzi wa reli ya kisasa (standard gauge) dola 15 bilioni (Sh33.8 trilioni) na wa ufuaji umeme wa Stiegler’s Gorge megawati 2,100 dola 5 bilioni (Sh11.27), jumla dola 20 bilioni (Sh45 trilioni).

Hivyo basi, mkopo wa SGR na Stiegler’s Gorge peke yake unaongeza deni kwa Sh45 trilioni. Ndio maana deni linakua. Mwigulu na Msigwa wasione aibu kutoka na kueleza kwa nini nchi inabeba mzigo mkubwa wa madeni. Muhimu ielezwe faida na ulazima wake.

Pamoja yote, tahadhari za kuendelea kukopa lazima zichukuliwe. Rais wa Tatu, Benjamin Mkapa, alifanya kazi kubwa kuirudisha nchi kwenye mstari wa kukopesheka. Isije tena Tanzania ikarudi kuwa nchi isiyokopesheka.