Jinsi ‘mikono’ ya Serikali ilivyotishia uhuru Bunge

Muktasari:

  • Zikiwa zimesalia siku chache kabla ya mwaka 2022 kumalizika, miongoni mwa matukio ya kukumbukwa ni kujiuzulu kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai baada ya kutofautiana kimtazamo na Serikali juu ya mikopo.

Dodoma. Zikiwa zimesalia siku chache kabla ya mwaka 2022 kumalizika, miongoni mwa matukio ya kukumbukwa ni kujiuzulu kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai baada ya kutofautiana kimtazamo na Serikali juu ya mikopo.

Kujiuzulu kwake kulisababisha majadala wa nguvu ya mkono wa Serikali ndani ya Bunge na uhuru wa chombo cha wawakilishi wa wananchi katika kukosoa na kuishauri Serikali.

Wapo wanaoona mpaka sasa bado Bunge na Mahakama havina uhuru mbele ya Serikali.

Ndugai alisema kuwa Tanzania ikiendelea kukopa nje iko siku nchi ‘itapigwa mnada’ na hivyo kutaka nguvu zaidi ziwekezwe katika kutoza kodi na tozo.

Kauli hiyo ilimfanya apingwe na viongozi, wabunge na wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM), akiwepo Rais Samia Suluhu Hassan.

Ulikuwa ni mtifuano wa Bunge na Serikali. Spika Ndugai aliamua kujiuzulu baada ya kuzidi kwa shinikizo. Alifanya hivyo Januari 6, 2022 na kuandika historia ya Bunge la vyama vingi nchini kwa Spika kuiachia nafsi hiyo.

“Ni lini sisi tutafanya wenyewe ‘and how’ (na kwa vipi),” alihoji Ndugai.

Mbali na mawazo hayo, kuliibuka kauli mitandaoni kwamba kiongozi huyo alijiuzulu kwa kulazishwa, jambo ambalo halikuthibitishwa wala kukanushwa.

Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Aida Khenan alisema kujiuzulu kwa Spika Ndugai ni jambo la kawaida, halikupaswa kubebewa uzito mkubwa kama jambo la kutisha.

Khenani, mbunge pekee wa Chadema mwenye Jimbo, alisema hakuna demokrasia iliyovunjwa kwa sababu ya kujiuzulu kwa kiongozi huyo, badala yake alisimama uwajibikaji.

“Mtu anasema wanakopa sana wakati anasahau Bunge alilolisimamia miaka mitano kabla lilikuwa chini ya Serikali iliyokopa zaidi kuliko Serikali nyingine na wote tunajua, sasa kwa nini azungumze hayo,” alisema Khenan.

Mbunge huyo anasema kauli ya Spika mstaafu ilionyesha dharau na kejeli kwa kiongozi mkuu wa nchi kwamba huenda alikuwa na nia nyingine zaidi ya alichokisema.

Kuhusu tofauti ya kiuongozi kati ya Ndugai na Dk Tulia, anasema “wote ni wale wale, chama chao kilimtoa mtu kikamuingiza mtu na kwa hiyo hakuna tofauti, kwani wanasimama kwa maslahi ya chama badala ya kuangalia nchi inataka nini.”

Katika maoni yake, Mbunge wa Mtera, Livingston Lusinde alisema kitendo kilichofanyika kwa Ndugai ni ukomavu mkubwa wa kisiasa, akitaka wengine kuiga mfano huo.

Lusinde (Kibajaji) alisema kauli za kuwa Ndugai alilazimishwa au demokrasia ilivunjwa hazina mashiko na huenda zinajengwa na wanasiasa aliowaita ni uchwara wanaoishiwa maneno na ajenda.

“Ndugai ni mtu mzima, lakini ukiuliza wanasiasa wakubwa ndani ya nchi huwezi kumkosa Ndugai, kwa hiyo hawezi kufanya jambo kwa kukurupuka, hebu tujifunze kwa gwiji huyu wa siasa,” alisema Lusinde.

Kibajaji anaulinganisha utawala wa mhimili huo kati ya Spika Dk Tulia Ackson na mtangulizi wake kwamba hauna tofauti sana, isipokuwa wa sasa anafuata sheria zaidi ambayo inatokana na msingi wa sheria alikobobea.

“Tutembeze bakuli ndio heshima, tukishakopa tunapiga makofi, sisi wa kukopa kila siku, tukasema pitisha tozo anayetaka asiye taka pitisha tozo, lazima tuanze kujenga wenyewe, nani atatufanyia, yuko wapi huyo mjomba, tukapitisha.

“Sasa deni letu ‘seventy trilioni’ (Sh70 trilioni). Hivi nyinyi si wasomi ‘is that healthy’ (hiyo ni afya). Kuna siku nchi itapigwa mnada hii,” alihoji Ndugai kwenye mkutano huo ambao kwa sehemu kubwa alizungumzia suala la kujitegemea waliposema wanataka kujenga makumbusho ya kabila la Wagogo akitaka waanzishe wenyewe.

Katika majibu yake, Rais Samia alisema nchi imekuwa ikikopa tangu utawala wa awamu ya kwanza na kushangaa kwamba inakuwaje watu wanahoji wakati huu.

Siku moja baada ya kauli ya Samia, makundi mbalimbali ndani ya CCM yalianza kutoa kauli za kumpinga Ndugai na kutaka achukuliwe hatua kutokana na kauli yake hiyo dhidi ya Rais wake.

Katika maelezo yake kwa waandishi wa habari katika Ofisi za Bunge jijini Dodoma, Ndugai alisema kwamba video iliyosambazwa na vyombo vya habari kwenye mkutano ambapo alisikika akikosoa mikopo “haikuwa halisi” lakini akasema anaomba msamaha kwa Rais, Mwenyezi Mungu kutokana na kauli yake hiyo.

Pamoja na msamaha huo wa hadharani, Januari 4, 2022 Rais Samia alizungumza Ikulu jijini Dar es Salaam na kutoa maelezo ya kuonyesha kutofurahishwa na maneno ya Ndugai, huku akikumbuka kauli aliyoambiwa na mtu mmoja mwenye busara kuwa watakaomsumbua ni wenzake wa CCM na sio wapinzani. “Na hapa inanikumbusha mtu mmoja mwenye busara, nilipotwishwa huu mzigo alikuja kuniona akaniambia, ‘nimekuja kukuona, kukupa hongera lakini pia kukupa pole’. Nikamwambia napokea,” Rais Samia alianza kueleza.

“Akanipa mawaidha mengi, lakini akaniambia, ‘atakayekusumbua kwenye kazi yako na kwenye uongozi wako ni shati ya kijani mwenzio na sio mpinzani. Mpinzani atakuangalia, ukimaliza hoja zao hawana neno. Lakini, shati ya kijani mwenzio anayetizama mbele mwaka 2025, 2030 huyu ndiye atakayekusumbua’,” alisema Rais Samia.

Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kati, Asha Luja alisema ilikuwa lazima Spika ajiuzulu kwani kutoa kauli kama ile nje ya Bunge haikuwa sahihi isipokuwa angetaka ingemfaa kuitolea bungeni.

Hata hivyo, Luja alisema mifumo ya uendeshaji wa bunge haizingatii maslahi ya wengi kwa sababu wanaoongoza mhimili huo wanaangalia kwanza masilahi ya chama chao.

Kwa upande mwingine, mwanasiasa huyo alisisitiza kuwa huenda Spika alishinikizwa kujiuzulu lakini haukuwa msimamo wake, huku akisisitiza kwamba demokrasia ndani ya chombo kama bunge ni kitu cha msingi sana.

“Chama chetu kina utaratibu wake, huwezi kuwa na kauli ya kupingana na kiongozi wako, pale Mzee aliteleza, ingawa naona ilitumika nguvu kubwa ya kumhukumu kwa kesi ambayo ingesameheka ili maisha yaendelee,” alisema mmoja wa maofisa ngazi ya juu ndani ya CCM.

Ofisa huyo anasema mtu aliyepaswa kumaliza sekeseke hilo alikuwa ni Katibu Mkuu wa CCM ambaye angetoa mwelekeo badala ya kuruhusu barua ya kujiuzulu ifanyiwe mijadala mingi inayoibuka na kukigharimu CCM katika kusababisha makundi.


Dk Tulia Ackson achaguliwa

Kujiuzulu kwa Ndugai (59) kulitoa nafasi ya kiti kuwa wazi na hivyo kuhitaji mtu mwingine, jambo lililotekelezwa kwa mujibu wa Katiba, lakini kanuni za kibunge.

Katika kinyang’anyiro cha kumpata mrithi wa kiti cha Spika, aliyekuwa Naibu Spika, Dk Tulia Ackson alijitosa na Februari Mosi 2022 jina la Dk Tulia Ackson liliibuka na akatangazwa rasmi kuwa mrithi wa kiti hicho.

Nafasi ya Dk Tulia ilizibwa na Mwenyekiti mzoefu wa Bunge, Mussa Zungu baada ya kuukwaa unaibu Spika, nafasi iliyokuwa wazi kwa wakati huo na nafasi yake haijazibwa hadi sasa.


Mabadiliko bungeni

Pia, katika mwaka unaomalizika Bunge lilipitia kwenye kipindi cha mabadiliko, ikiwemo kuzifumua kamati mbalimbali na kuweka utaratibu tofauti kwa mawaziri wanapojibu maswali bungeni.

Zamani Waziri au Naibu Waziri walipokuwa wanajibu maswali walisimama kutoka vitini na walipomaliza kujibu walirudi kusubiri maswali ya nyongeza kabla ya kurudi mimbarini tena.

Kwa sasa Waziri au Naibu anatakiwa kusimama mahali pamoja hata kama angeulizwa maswali mengi na anapomaliza ndipo anaruhusiwa kuketi.