Kigoda cha Mkapa kiwe chachu ya kumkumbuka Mzee Mwinyi

Hayati Benjamin Mkapa
Muktasari:
- Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (Saut), Mwanza, kimezindua Kigoda cha Utafiti cha Mkapa kutoa fursa utafiti na machapisho kuhusu maisha, kazi na falsafa za aliyekuwa Rais wa Tatu, Benjamin Mkapa.
Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (Saut), Mwanza, kimezindua Kigoda cha Utafiti cha Mkapa kutoa fursa utafiti na machapisho kuhusu maisha, kazi na falsafa za aliyekuwa Rais wa Tatu, Benjamin Mkapa.
Hiyo ni fursa kwa wasomi na wanazuoni kufanya tafiti zitakazosaidia mabadiliko chanya katika jamii. Zaidi, kuwezesha na kuongeza uelewa wa wanazuoni katika kupambanua masuala mbalimbali kupitia uvumbuzi na tafiti za kisayansi.
Angalau jina la Mkapa lipo Saut. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuna kigoda cha Mwalimu Nyerere, kinachotumika kuenzi falsafa na maarifa ya Rais wa Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere.
Kwanza ni pongezi. Viongozi ambao kwa sehemu kubwa ya maisha yao wametoa mchango mpana kwa taifa kuenziwa ni jambo mwafaka. Mwalimu Nyerere na Mkapa, kila mmoja ana historia yake adhimu kwa utumishi wa nchi.
Mwalimu Nyerere kwa namna alivyoyavaa mapambano ya kudai uhuru na kuunganisha jamii za makabila kuwa taifa. Mkapa akiwa Rais wa kwanza kuchaguliwa chini ya mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Utumishi wa miaka zaidi ya 23 ambayo Mwalimu Nyerere aliitumikia nchi. Vilevile miaka 10 ya Mkapa. Kila mmoja kwa nafasi yake ameacha kumbukumbu nyingi chanya. Hapo ni bila kuonesha yupi alifanya zaidi.
Mwalimu Nyerere kama mwasisi wa taifa, kila kinachotokea kwenye Tanzania huru ni matunda ya jasho alilovuja na maono aliyoyasimamia. Mkapa alikuwa mwanamageuzi bora wa kiuchumi, kipindi ambacho nchi ilihitaji mabadiliko.
Hata hivyo, katikati ya Mwalimu Nyerere na Mkapa kuna Rais wa Pili, Ali Hassan Mwinyi. Aliipokea nchi katika mazingira magumu ya kiuchumi. Aliamua kuthubutu kuiondoa nchi ndani ya mizizi ya ujamaa na kujitegemea na kuielekeza kwenye uchumi wa soko.
Mambo mengi ambayo Mkapa aliyatekeleza kwa kasi kubwa, yalianza kipindi cha Mwinyi. Ubinafsishaji ulianzia kwa Mwinyi, kupitia Kampuni ya Bia Tanzania (TBL). Mkapa aliendeleza kwa ari kubwa zaidi.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), iliasisiwa na Mwinyi kipindi cha mwisho cha utawala wake. Kisha Mkapa akaanza nayo kikamilifu na kuwezesha nchi kuanza kukusanya mapato mengi zaidi.
Hivi sasa nchi inapokuwa inajivunia kukusanya mapato mpaka Sh2 trilioni kwa mwezi kwa sababu ya uwepo wa TRA, inabidi heshima irejee kwa aliyeanzisha. Mwinyi hapaswi kusahaulika pale tunapotaka kuanzisha masuala ya msingi, hasa katika kuenzi viongozi wa taifa.
Hoja hii inamhusu pia Rais wa Nne, Jakaya Kikwete, kwa wakati ujao. Na isiishie kwa marais tu, vilevile viongozi wengine wenye mchango mkubwa kwa taifa. Ni ajabu mpaka leo hakuna kumbukumbu ya Salim Ahmed Salim wala Adam Sapi Mkwawa.
Salim, si tu kama Waziri Mkuu na Naibu Waziri Mkuu katika vipindi vya Nyerere na Mwinyi, ni jinsi alivyokuwa taa ya nchi kimataifa. Alishakuwa Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, vilevile Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU).
Tangu Salim alipokosa urais mwaka 2005, imekuwa kama nchi imesahau nyakati bora ambazo alilihudumia taifa, au alivyoing’arisha nchi kwenye jumuiya za kimataifa.
Sapi Mkwawa ni Spika wa Bunge wa kwanza Tanzania. Hata sasa hakuna mtu aliyekalia kiti cha uspika wa Bunge la Tanzania kwa muda mrefu kama yeye. Wapi umewahi kuona wanaenziwa?
Soko Kuu Dodoma limepewa jina la Job Ndugai. Hakuna ambaye amewahi kushangaa kuona mtangulizi wa Ndugai kwenye kiti cha spika, Anne Makinda, hana kumbukumbu yoyote ya kitaifa.
Daraja la juu la Ubungo, Dar es Salaam, linaitwa John Kijazi Interchange. Je, makatibu wakuu waliohudumia kabla ya Kijazi hawakustahili? Daraja la juu la Tazara, limepewa jina la Injinia Patrick Mfugale. Taifa halijawahi kuwa na mainjinia wengine wenye michango mikubwa?
Kuna ukweli sharti usemwe. Kumekuwa na hulka ya kutunuku majina vitu kwa utashi na urafiki kuliko kuangalia na kupima mchango. Ndio maana kuna hali kama ya wengine kupewa na wapo wanaorukwa.
Mathalan, Mfugale na Kijazi walitajwa kuwa watu wa karibu na Rais wa Tano, Dk John Magufuli, hivyo, akaamua kuwatunuku madaraja ya kupitisha magari ya juu, Tazara na Ubungo.
Kadhalika, Ndugai alionekana kuongoza Bunge kwa namna iliyompendeza Magufuli. Naye akampa jina la Soko Kuu Dodoma. Watu kama Salim na Sapi ambao wamekosa marafiki, huwaoni kokote.
Dar es Salaam kuna Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, ila ni fupi. Inaunga kutoka makutano ya Ohio na Bibi Titi mpaka Mwenge, inakoanzia Bagamoyo Road. Tabora upo Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi. Si vibaya. Hata hivyo kuna mjadala kuhusu jumuiya ya wanazuoni.
Mkapa amekumbukwa. Safi kabisa. Hata hivyo, Makamu Mkuu wa Chuo cha Sauti ni Balozi Costa Mahalu, watu wengi huamini kuwa Mahalu alikuwa swahiba wa Mkapa.
Kumbukumbu nzuri ni kuwa Mahalu alipokuwa anakabiliwa na mashitaka ya matumizi mabaya ya ofisi alipokuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mkapa alikwenda mahakamani kutoa ushahidi uliomsaidia mno kushinda kesi.
Mkapa kupitia kitabu chake alichokiita “My Life, My Purpose” – “Maisha Yangu, Kusudi Langu”, alisema kuwa sababu ya kwenda mahakamani kumtetea Mahalu ni kwa kuwa aliona hakuna kosa alilofanya.
Ameandika kuwa kila kitu Mahalu alichofanya, alikiidhinisha yeye alipokuwa Rais. Akasema, kabla ya Takukuru kumfungulia mashitaka Mahalu, walikwenda kwake na akawaeleza waachane na kesi. Kwa kuwa Takukuru waliamua kuendelea, ndio maana aliamua kwenda mahakamani kutoa ushahidi.
Kwa historia hiyo ya Mkapa kwenda mpaka mahakamani kumtolea ushahidi Mahalu, jumlisha na minong’ono ya uwepo urafiki baina yao, yupo mtu anaweza kuhisi kuwa ni sababu ya Mkapa kukumbukwa haraka Saut na kuundiwa Kigoda chake cha utafiti.
Kama atatokea mtu wa kuwaza hivyo, basi hatakosekana ambaye atasema Mwinyi hajawahi kukumbukwa na taasisi yoyote ya elimu ya juu kwa kuwa hana rafiki mkuu wa chuo chochote.
Ni changamoto tu. Haina maana ya kukosoa uwepo wa Kigoda cha Mkapa. Ni sahihi kabisa kuenziwa. Tena anastahili. Kinachotakiwa kufanyika isiwe kwa sababu ya urafiki ndio majina fulani yatokeze na mengine kimya, bali mchango wa mtu kwa taifa ndio uamue.
Inatakiwa kuwepo mchakato wa kutathmini mchango wa viongozi wa kitaifa. Kisha majina yapitishwe na yaanze kuenziwa kwa mtiririko unaofaa. Kuna siku atatokea Rais ataamua jina la baba yake ndio litambuliwe kuwa Ikulu.