Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Uchaguzi wa Kenya ulivyotoa somo la kuheshimu katiba, sheria na uwazi

Rais mteule wa Kenya, William Ruto (kushoto) pamoja na mgombe mwenza wake, Rigathi Gachaua wakionyesha cheti baada ya kutangazwa kuwa washindi wa Uchaguzi Mkuu wa nchini hiyo, jijini Nairobi jana. Picha na AFP

Muktasari:

  • Mwaka 2022 unaoelekea ukingoni utakumbukwa kwa matukio mbalimbali, likiwemo lile la uchaguzi mkuu wa Kenya ambao ulishuhudia William Ruto akimbwaga mwanasiasa mkongwe, Raila Odinga.


Mwaka 2022 unaoelekea ukingoni utakumbukwa kwa matukio mbalimbali, likiwemo lile la uchaguzi mkuu wa Kenya ambao ulishuhudia William Ruto akimbwaga mwanasiasa mkongwe, Raila Odinga.

Agosti 9, 2022 Kenya ilifanya Uchaguzi Mkuu wake ikiwa ni utaratibu wa kikatiba wa kila baada ya miaka mitano, uchaguzi huo ulikuwa na mchuano mkali kati ya Ruto na Odinga na kuna wakati ilionekana nchi hiyo itatumbukia kwenye vurugu za kisiasa kama zilizotokea mwaka 2007.

Hata hivyo, uchaguzi huo ulipita salama na kuacha gumzo kwa namna ulivyofanyika.

Ulionyesha ilivyojiandaa kukuza demokrasia kwa kuruhusu watu kuchagua wanaowataka.

Licha ya kuwepo kwa historia mbaya ya uchaguzi wa mwaka 2007 uliombakiza madarakani Rais wa wakati huo, Mwai Kibaki, lakini pia ukitupilia mbali siasa zao za kikanda na ukabila, bado wanabaki kuwa walimu wazuri wa namna ya kufanya uchaguzi huru na wa haki.

Uchaguzi wa Kenya wa mwaka huu ulihusisha wagombea wanne kila mtu akiwakilisha umoja au chama chake; William Ruto (Kenya Kwanza), Raila Odinga (Azimio la Umoja), David Waihiga (Chama cha Agano) na Profesa George Wajackoyah (Chama cha Roots).

Kati ya wagombea hao wanne wa urais, watatu walikuwa na wagombea wenza wanawake kasoro William Ruto, ambaye mgombea mwenza wake alikuwa Rigathi Gachagua.

Mizani ya zaidi ya siku 90 za kampeni ilielemea upande wa kambi mbili, moja iliwakilishwa na aliyekuwa Naibu Rais, William Ruto na nyingine bendera yake ikipeperushwa na Waziri Mkuu mstaafu wa nchi hiyo, Raila Odinga ‘Baba’.

Katika uchaguzi huo kampeni za Odinga ziliungwa mkono na Rais aliyekuwepo madarakani kipindi hicho, Uhuru Kenyatta ambaye alimpiga vijembe sana Naibu Rais wake aliyekuwa anagombea pia kiti hicho.

“Nyinyi watu wa mlima Kenya niwaambie tu msichague waongo waje kuwaongoza (akimaanisha Ruto), mchagueni Baba (Odinga) ili awaletee maendeleo,” Kenyatta alisema hayo akiwa kwenye ziara ya kikazi eneo la mlima Kenya.

Vijembe vya Kenyatta havikuweza kuvumiliwa na Ruto, ambaye alijipambanua kama kiongozi wa ‘mahustler’ (wananchi wa kipato cha chini), mara kadhaa kwenye kampeni zake alimtaka Kenyatta atulie na asubiri kuikabidhi nchi kwa amani.


Yapi ya kujifunza?

Jambo la kwanza, msimamo wa Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC), Wafula Chebukati ambaye alimtangaza Ruto kuibuka mshindi kwa kura milioni 7.1, huku akifuatiwa na Odinga aliyeambulia kura milioni 6.9.

Msimamo wa Chebukati ulionekana baada ya makamishna wanne kati ya saba wa tume hiyo kujitenga na kuyakataa matokeo hayo, wakiongozwa na Mwenyekiti msaidizi, Juliana Cherera.

Kwenye hotuba yake wakati akitangaza matokeo kwenye ukumbi wa Bomas, nje kidogo ya jiji la Nairobi, Chebukati alisema alipokea vitisho pamoja na baadhi ya wasaidizi wake wa IEBC kuuliwa, lakini ameamua kusimamia ukweli kutangaza matokeo sahihi.

“Haijakuwa safari rahisi, tunapozungumza makamishna wangu wawili na ofisa mkuu mtendaji wa IEBC wamejeruhiwa,’ alisema Chebukati muda mfupi baada ya vurugu ya kupinga matokeo hayo kuibuka kwenye ukumbi wa Bomas, lakini hali ilitulia.

Kitu kingine cha kujifunza kutoka Kenya ni kuwa na katiba ambayo inaipa Tume ya uchaguzi (IEBC) uhuru wa kuamua na njia nzuri ya kupata watendaji wa IEBC.

Kupitia katiba mpya ya Kenya ya 2010 iliyopatikana baada ya machafuko ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2008, kwa sasa mwenyekiti na makamishna wa Tume hiyo wanapatikana kwa kuomba kazi (kujaza fomu) majina yenye vigezo yanapelekwa Bungeni yanachujwa tena kisha Rais atamchagua mmoja kuwa mwenyekiti.

Huenda mchakato wa kupatikana kwa viongozi hao unawafanya wawe huru kufanya maamuzi yao bila kuogopa au kulinda maslahi ya mteuzi wake.

Katika hali ya kushangaza, Kenya pia imetufundisha Afrika kuwa vyombo vya dola wakati wa uchaguzi visimamie haki na si kulinda chama tawala na kunyanyasa wapinzani wa Serikali iliyopo madarakani.

Polisi walisimamia kampeni zote kwa usawa na pale kulipokuwa na malalamiko walitoa taarifa ya kuyachunguza mara moja.

Mfano, wanafunzi tisa wa Chuo Kikuu cha Moi walishikiliwa na polisi kwa muda wa siku tatu kwa tuhuma zinazosemekana za kusambaza ujumbe wa kumchafua mgombea wa urais kwa tiketi ya Kenya Kwanza, Naibu Rais William Ruto.

Hakimu Mkazi wa Eldoret, Onkoba Mogire aliagiza wanafunzi hao washikiliwe katika kituo cha polisi cha Langas kwa siku tatu huku uchunguzi ukiendelea. Hatua hiyo ilikuja baada ya Ruto kujitokeza hadharani kulaani uwepo wa vipeperushi vyenye ujumbe wa kumchafua, eneo la Eldoreti na maeneo mengine nchini humo.

Fundisho la nne, Kenya wanatuonesha ni kwa namna gani wananchi wake wana msimamo na maamuzi ya wapiga kura yanaheshimiwa. Katika uchaguzi ambao Rais aliyekuwa madarakani anamuunga mkono Odinga lakini bado wananchi wanamchagua Ruto, ni kitu cha kipekee kwa siasa za Afrika. Mara nyingi nchi za Afrika mgombea anayeungwa mkono na Rais anayetoka madarakani anashinda kwa sababu ya ushawishi na mazingira yanayotengenezwa kwa makusudi, lakini mbinu hii haikufua dafu Kenya.

Mwisho kabisa tunajifunza uwazi kwenye mchakato mzima wa uchaguzi, Kenya walituonyesha mwenendo wote wa kila kura iliyopigwa na kulikuwa na tovuti rasmi ambayo IEBC ilikuwa inaweka matokeo ya fomu namba 34A na kila mwananchi aliweza kuona.

Wakati uwazi huo kwenye kuhesabu matokeo ukiwepo, lakini pia kila chombo cha habari kiliruhusiwa kuwa na vituo vyao vya kuhesabia kura kutoka kwenye takwimu zinazorekodiwa za fomu 34A.


Wadau wa siasa wanasemaje?

Akizungumzia uchaguzi huo, Katibu wa NEC Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (Suki) CCM, Kanali mstaafu Ngemela Lubinga alisema tunachotakiwa kujifunza kutoka Kenya ni umuhimu wa kuvumiliana kwenye siasa.

“Kwenye uchaguzi wowote kuvumiliana kisiasa ni jambo la muhimu, ndio maana Kenya ukiacha mbali tofauti zao za kimtazamo lakini uchaguzi ulienda vizuri na baada ya kumaliza wamerudi kuwa kitu kimoja,” alisema.

Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema fundisho tunalolipata kutokana na uchaguzi wa Kenya ni umuhimu wa kuwa na katiba imara ya nchi.

“Naweza kusema tunatakiwa tujifunze kuwa katiba imara imeweka taasisi imara ya kusimamia haki. Ukiangalia hata Jeshi la Polisi halijaingilia uchaguzi, lakini pia mahakama imefanya maamuzi kwa uhuru na na usawa bila kushinikizwa,” alisema.

“Hii pia inatuonyesha kuwa wananchi wa Kenya walikuwa na uelewa mkubwa wa kisiasa kuhusiana na umuhimu wa uchaguzi huu,” aliongeza.

Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano kwa Umma wa CUF, Mohamed Ngulangwa alisema Tanzania inapaswa ijifunze kuendesha uchaguzi kwa uwazi kama ambavyo Kenya imefanya mwaka huu.

“Tanzania inapaswa ijifunze uwazi kwenye shughuli za uchaguzi kuanzia kupiga, kuhesabu kura na kutangaza matokeo, wenzetu wa Kenya waliacha matokeo wazi na kila mtu alikuwa ana uwezo wa kuyapata kadiri kura zinavyohesabiwa,” alisema.

Ngulangwa alisema uchaguzi wa nchi hiyo umekuwa wa demokrasia, wenye uhuru na Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilikuwa huru kutokana na katiba yao nzuri ya mwaka 2010

“Katika mapendekezo yetu tuliyopeleka kikosi kazi, CUF tulipendekeza Serikali ijifunze kutoka kwa Kenya kwa sababu ilipitia kipindi kigumu kwenye uchaguzi 2008, lakini katiba mpya ilikuja 2010 na ikawakomboa kutoka kwenye mkwamo huo,” aliongoza.


Wachambuzi wa siasa wanena

Mchambuzi wa siasa na mhadhiri wa idara ya sayansi ya siasa UDSM, Profesa Mohamed Bakari alisema uchaguzi wa Kenya unaakisi ni jinsi gani kuna umuhimu wa kuwa na katiba mpya nchini inayokidhi matakwa ya wananchi.

“Kenya ni nchi yenye katiba nzuri zaidi Afrika Mashariki, ukiachana na mapungufu ambayo kila katiba inayo. Hapa tunajifunza umuhimu wa kuwepo kwa katiba mpya,” alisema.

“Pia, tunajifunza kuwa kuendelea kuchelewesha mchakato wa kupatikana kwa katiba mpya hakuna afya kwenye demokrasia yetu, mfano mgogoro wa kupinga matokeo ya uchaguzi uliotokea Kenya umeisha kwasababu Katiba inaelekeza mahakama ya juu ihusike kuutatua,” aliongeza.

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Dk Faraja Kristomus aliunga mkono suala la nafasi ya Katiba nzuri kwenye Uchaguzi Mkuu ambaye alisema matokeo kupingwa mahakamani ni hatua kubwa kwa Kenya kwenye ukomavu wa siasa. “Katiba yao inaruhusu matokeo ya urais kupingwa mahakamani, huo ndo msingi wa demokrasia. Kwa sababu unawafanya wananchi kuamini matokeo yaliyopatikanba kwenye uchaguzi,” alisema.

Dk Kristomus alisema kuna haja ya kujifunza kutokana na mapungufu yao ili tusiyafanye kwetu ikiwemo na vyombo vya habari kuchagua upande mapema, kitu ambacho kina athari kubwa kwa uendeshaji wa vyombo hivyo baada ya uchaguzi.