Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Matumizi ya lugha za kuudhi yanaongezeka kadri uchaguzi mkuu unavyokaribia Kenya

Rais wa Kenya,Uhuru Kenyatta (kulia) akizungumza na makamu wake ,Wiliam Ruto.

Muktasari:

Viongozi wa vyama vya upinzani na wa muungano wa vyama vinavyotawala wa Jubilee nchini Kenya wamekuwa wakirushiana maneno tangu Juni mwaka huu. Kadri Uchaguzi Mkuu unavyokaribia ndiyo matamshi makali zaidi yanasikika kutoka kwenye kambi hiyo mbili zenye ushindani mkubwa kisiasa.

Siasa ni chafu ama wanasiasa ndio wachafu? Nafikiri jibu litategemea unasimama wapi unapojibu swali hili.

Viongozi wa vyama vya upinzani na wa muungano wa vyama vinavyotawala wa Jubilee nchini Kenya wamekuwa wakirushiana maneno tangu Juni mwaka huu. Kadri Uchaguzi Mkuu unavyokaribia ndiyo matamshi makali zaidi yanasikika kutoka kwenye kambi hiyo mbili zenye ushindani mkubwa kisiasa.

Waziri Mkuu wa zamani, Raila Odinga ndiye analengwa zaidi na kauli zinazotolewa ya Jubilee. Sababu ya msingi ni kuwa wanasiasa wanaamini njia ya kushusha umaarufu wa kiongozi huyo wa Chama cha Cord ni kumtolewa lugha za kuudhi.

Makamu wa Rais, William Ruto ndiye anaonekana kama kinara kati ya wanasiasa wanaomshambulia zaidi Odinga.

Humwita Odinga “mtu wa vitendawili”, “mganga” na maneno mengine yasiyochapishika katika gazeti hili linalosomwa na familia yote.

Rais Uhuru Kenyatta alijiweka kando na matamshi ya aina hiyo, hadi mwezi uliopita alipowashangaza Wakenya baada ya kuanza kumporomoshea maneno makali Odinga.

Joho anavutana na Ruto

Malumbano hayo yakizidi kuchukua sura mpya kila siku, Gavana wa Mombasa, Ali Hassan Joho naye ameanza kujibu mashambulizi kwa kuelekeza maneno makali kwa Ruto.

Uhasama kati ya Joho na Ruto uliibuka miezi miwili iliyopita wakati Makamu huyo wa Rais, alipozuru Mombasa na kusema Joho hana shahada anayodai ameishomea.

Alisema mwanasiasa huyo alidanganya na kulaghai Wakenya kwamba alisomea shahada kwenye chuo kikuu kimoja cha Uganda ilhali aliinunua na sasa anajidai kuwa msomi.

Pia, Ruto alimsuta mwanasiasa huyo wa ODM kwa kudai mali yake inatokana na biashara sisizo halali.

Ruto hakujua kwamba alikuwa amechokoza nyuki mzingani.

Punde si punde, Joho alimmiminia maneno ya kuudhi na kejeli bila kujali nafasi walizonazo kwenye jamii.

Hivi karibuni, Joho alimjibu Ruto akisema kwamba Makamu wa Rais ni mwizi na fisadi asiyeweza kusema mali yake nyingi alizipata vipi.

Joho naye aliibuka tena na kumkumbusha Ruto kwamba miaka miwili iliyopita, Mahakama ilimpata na hatia ya kumnyang’anya jirani yake Adrian Muteshi shamba lake mwaka 2007.

Ni kweli, Ruto alishtakiwa na Muteshi ambaye alikuwa mkimbizi wa ndani baada ya vita vya kikabila vya mwaka 2007 kumwadhirisha na kumlazimu atoroke.

Amani iliporejea, Muteshi alirejea shambani kwake na kuambiwa kuwa ardhi hiyo imechukuliwa na Ruto.

Mkimbizi huyo wa ndani alipiga kiguu na njia hadi kortini ambapo alimshtaki Makamu wa Rais kwa kunyakua shamba lake. Mahakama ilimpata Ruto na hatia na ikamwaru amplieMuteshi faini ya Ksh5 milioni (Sh105 milioni).

Kiini cha uhasama kati ya Ruto na Joho ni urafiki wa dhati kati ya gavana huyo na Odinga. Wiki iliyopita, Joho alitangaza kwenye mkutano ya siasa katika eneo la Nyanza kwamba, yuko tayari kutoa maisha yake kama hicho ndicho kinahitajika ili Odinga aingie Ikulu.

Ruto hampendi Raila ingawa viongozi hao walikuwa marafiki wakubwa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2007.

Makamu wa Rais wakati huo alikuwa Mbunge wa Eldoret Kaskazini na mgombea mwenza wa Raila.

Baada ya kura kuibwa na Rais mstaafu Mwai Kibaki kuendelea kuongoza hadi mwaka 2013, uhusiano kati ya hao wawili ulianza kudorora kwa kasi.

Sababu ya Uhuru kumshambulia Odinga

Uhuru amekuwa akirusha matusi kwa Raila kwa tangu mwezi uliopita. Hii ni kwa sababu mwanasiasa huyo wa upinzani amekuwa akifichua maovu serikalini hasa yanayohusiana na masuala ya ufisadi.

Badala ya Uhuru kufanya kila awezalo kuhakikisha ufisadi unapungua serikalini, anaanza kumkejeli na kumrushia cheche za matusi Raila kila wakati anapopata fursa.

Alipozuru Kenya ya Kati hivi karibuni, ambako ana wafuasi wengi, Kenyatta alisema Odinga ni kama kidonda sugu kwa uchumi wa Kenya na kwa hivyo hafai kabisa awe akizungumza kuhusu ufisadi na masuala mengine yanayoathiri Serikali yake.

Rais amenukuliwa akimwita Odinga mjinga, mtu mdogo, mchawi, mwendawazimu na kadhalika.

Kauli hizo zimewaudhi viongozi wa upinzani ambao sasa wametoa onyo kali kwa Uhuru na wanasiasa wa mrengo wake wasidhubutu tena kumchokoza Odinga.

Kwenye taarifa waliotoa kwa pamoja kwa vyombo vya habari, wanasiasa hao wakiongozwa na mwenyekiti wa ODM, John Mbadi walisisitiza kwamba kamwe hawatavumilia matusi hayo.

Raila amekuwa akijizuia kulipiza kizazi kwa kurusha matusi kwa Rais na naibu wake. Ameonyesha uzalendo na ukomavu mkubwa kwa jinsi anavyoenenda. Kila anapotukanwa na Jubilee, siku inayofuata hujaribu kuonyesha jinsi viongozi wanafaa kuongoza.

Wanasiasa wa upinzani wana kero kubwa kwa matamshi hayo machafu kutoka Jubilee na sasa wanasema jamii ya kimataifa wanafaa kuona na jinsi viongozi wakuu wanaendesha nchi kwa kutoa lugha za matusi na chuki dhidi ya viongozi wengine.

“Tunawaonya,” wakasema kwenye taarifa kwa vyombo vya habari. Wanasema hasira za Uhuru na Ruto dhidi ya upinzani kwa sababu ya orodha ndefu kutoka Nairobi hadi Timbuktu, inaweza kuteketeza nchi mwakani.

Ama kwa kweli, viongozi wanafaa kuwa mfano mwema kwa wananchi na kuonyesha ukomavu na mienendo inayofaa katika jamii. Kama upinzani unawaudhi, kuna njia za kutatua hali hii. Matusi yanasaidia katika kupanua mwanya wa chuki miongoni mwa viongozi.

Baadaye, chuki hiyo inaenea hadi kwenye matawi na kusababisha mapigano miongoni mwa makabila mbalimbali.

Upinzani unateta kwamba, Uhuru na Ruto wanawasha moto ambao watashindwa kuuzima. Wanawataka kupunguza matamshi yao mabaya na kuanza kuunganisha nchi ili amani na utangamano yaweze kupenya katika kila pembeb ya nchi.

Uhuru na Ruto pengine wanadhani wanamtusi Odinga lakini wanasahahu kwamba kiongozi huyo mwenye umaarufu mkubwa anawafuasi wengi.

Kuna Wakenya wasioweza kufikiria mara mbili kumtetea Odinga hata kama ni kufa. Kwa hivyo, yafaa viongozi wa pande zote mbile kuchunga ndimi zao wasije wakaweka nchi kwenye lindi la mapigano.

Kenyatta alipochaguliwa mwaka 2013, aliapa kulinda Katiba na kutetea Wakenya wote bila kujali msingi wa kikabila wala tabaka. Lakini Uhuru anasahau hayo. Anafikiri yeye ni kiongozi wa Jubilee pekee.

Nawasihi viongozi wa mirengo yote miwili kuachana na matusi na kuleta wananchi pamoja ili taifa liweze kwenda mbele kama nchi nyingine.

Upinzani unaonya Ruto aachane na matamshi ya uongo na propaganda anayoelekeza kwa viongozi wa upinzani na wandani wao.

“Wanafaa kuacha kutoa habari sisizo za kweli kwa umma kuhusu upinzani kwa lengo la kujitafutia kura mwakani,” taarifa ilisema.

Mbadi na wenzake wanasema, lugha chafu sasa imekuwa kama sera kwa Jubilee.

Matamshi ya Jubilee yanadhihirisha kwamba hawataki ushauri kwa kuwa wanafikiri wanajua kila kitu kuhusu uongozi.

Wanaonyesha upinzani kwamba wao wako madarakani na hakuna kitu wanaweza kuwafanyia.

Ni kiburi. Lugha hii chafu inaweza kuwasha mioto yasiyoweza kuzimwa. Jubilee wafaa kusikia wanayoambiwa ili waachane na matamshi yanayoleta chuki.

Viongozi wanapoanza kutumia matusi dhidi ya viongozi wengine, wanaonyesha kwamba wanakosa heshima. Ikiwa viongozi wanatapika matusi, je, wananchi watafanya nini?

Ni ajabu kwamba, viongozi wa upinzani husumbuliwa na maajenti wa serikali wanapoanza kugombana na Uhuru na Ruto, lakini hawajawahi kuwaonya Jubilee wanapochokoza na kutukana upinzani.

Matamshi ya Ruto na Uhuru yanapochunguzwa kwa kina, yana maana kwamba, walio upinzani Serikali siyo yao. Dhana kama hii, siyo nzuri. Serikali inafaa kuwa ya kila mtu kwa sababu kila mmoja anatoa ushuru unaotumiwa kuwalipa viongozi na kuendesha miradi ya maendeleo.

Mwandishi ni mchambuzi wa siasa, anaishi Nairobi, Kenya. Baruapepe: [email protected]