Rais Museveni hafai kupatanisha Burundi

Rais Yoweri Museveni wa Burundi
Muktasari:
Mwaka 2015 Nkurunziza si habari njema; ni jiwe linaloleta “inkurumbi” yaani habari mbaya. Tangu Aprili mwaka huu alipotangaza na baadaye kuidhinishwa na Mahakama ya Katiba kuwania muhula wa tatu wa urais, nchi hiyo imegubikwa na maandamano, jaribio la mapinduzi, milio ya risasi na mauaji ya watu hasa wapinzani.
Neno “PIERRE” kwa Kifaransa lina maana ya jiwe na “NKURUNZIZA” kwa Kihutu lina maana ya habari njema. Mwaka 2005 Pierre Nkurunziza alikuwa “jiwe” lililowapa Warundi “habari njema” alipochaguliwa kuwa rais wa Burundi baada ya miaka mingi ya mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.
Mwaka 2015 Nkurunziza si habari njema; ni jiwe linaloleta “inkurumbi” yaani habari mbaya. Tangu Aprili mwaka huu alipotangaza na baadaye kuidhinishwa na Mahakama ya Katiba kuwania muhula wa tatu wa urais, nchi hiyo imegubikwa na maandamano, jaribio la mapinduzi, milio ya risasi na mauaji ya watu hasa wapinzani.
Zaidi ya watu 70 wameuawa akiwamo kiongozi wa chama cha upinzani, Zedi Feruzi kwa kupinga Nkurunziza kuwania urais muhula wa tatu.
Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Mataifa (UN) wamekuwa wakifuatilia kwa karibu hali ya kisiasa ya taifa hilo dogo na masikini barani Afrika. Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walimteua Rais Yoweri Museveni wa Uganda kuwa mpatanishi ili kuirejesha katika amani, nchi hiyo.
“Je, Rais Museveni ataweza?” na “Je, ni mtu sahihi?” Kabla ya kumjadili Museveni, tuangalie kwa ufupi, historia ya Burundi ilivyogubikwa na mapigano ya kikabila kati ya Wahutu na Watutsi na mauaji ya viongozi.
Historia fupi
Mapambano ya kudai uhuru yalipata msukomo vyama vya siasa vilipoanzishwa mwaka 1959. Moja ya vyama vya mwanzo kabisa ni Uprona ambacho kiliwasilisha pia ajenda kwa mkoloni wao Ubelgiji, atenganishe nchi iliyojulikana kama Ruanda Urundi kuwa nchi mbili tofauti. Ikawa hivyo.
Mwaka huohuo, Wahutu walioko Rwanda walivamia na kuwaua, kwa maelfu, Watutsi ambao wengi wao walikimbilia Uganda. Wahutu wakaanza kuitawala Rwanda baada ya kushinda uchaguzi wa mwaka 1960.
Uprona, chama kilichoonekana kuwa na wanachama kutoka makabila yote mawili nchini Burundi chini ya Prince Louis Rwagasore na PDC ndivyo vyama vya mwanzo kuenea nchi nzima. Miezi michache baada ya Uprona kunyakua viti vingi vya ubunge, Prince Rwagasore aliuawa Oktoba 13, 1961. Burundi ilipata uhuru Julai 1, 1962 chini ya Mfalme Mwami Mwambutsa IV.
Japokuwa Wahutu na Watutsi walishirikishwa serikalini, mivutano ilikuwa mikubwa. Wahutu waliokuwa na wingi wa viti bungeni, walijiona wamesalitiwa baada ya mfalme kumteua Mtutsi kuwa waziri mkuu. Polisi wa Kihutu wakataka kufanya mapinduzi lakini walifyekwa vibaya na Jeshi lililokuwa linaongozwa na Mtutsi, Kapteni Michel Micombero.
Aliteuliwa Pierre Ngendandumwe (Mhutu) kuwa waziri mkuu lakini aliuawa mwaka 1965. Mauaji hayo yalichochea Wahutu kuwaua Watutsi kote Burundi. Mfalme aliangushwa mwaka 1966 na mtoto wake, Prince Ntare V.
Mwaka huo huo, Micombero alimng’oa Ntare na kuigeuza Burundi kuwa jamhuri ingawa kimsingi ilitawaliwa kijeshi. Mwaka 1972 Chama cha Wafanyakazi Wahutu (UBU) kiliratibu mauaji ya Watutsi. Jeshi lilijibu kwa kuwalenga Wahutu. Inakisiwa zaidi ya watu 100,000 waliuawa huku mamia kwa maelfu wakitorokea Rwanda na Tanzania.
Micombero alipinduliwa na Kanali Jean-Baptiste Bagaza (Mtutsi) mwaka 1976. Ikaandaliwa katiba mpya mwaka 1981 na kuifanya Burundi kuwa nchi ya chama kimoja. Mwaka 1984, Bagaza alichaguliwa kuwa mkuu wa nchi ambaye alikandamiza uhuru wa vyama vya siasa na madhehebu ya dini.
Meja Pierre Buyoya (Mtutsi) alimpindua Bagaza mwaka 1987 akasimamisha Katiba na kufuta vyama vya siasa. Masalia ya wafuasi wa UBU, waliojiunga upya kama Palipehutu mwaka 1981, waliendesha mauaji ya wakulima wa Kitutsi mwaka 1988.
Mwaka 1994, Bunge lilimteua Cyprien Ntaryamira (Mhutu) kuwa rais. Lakini yeye pamoja na Rais wa Rwanda Juvénal Habyarimana waliuawa ndege waliyokuwa wanasafiria kutoka Arusha ilipotunguliwa Rwanda.
Spika wa Bunge, Sylvestre Ntibantunganya (Mhutu) aliteuliwa kuwa rais Oktoba 1994 akaunda serikali iliyoshirikisha vyama 12 kati ya 13. Machafuko yalizuka, watu waliokuwa wakiishi kwenye makambi Bujumbura waliuawa. Chama cha Watutsi kikajitoa serikalini na bungeni.
Mwalimu Nyerere
Mwaka 1996, Buyoya alipindua tena serikali, akafuta katiba na akaapishwa kuwa rais. Hicho ndiyo kipindi, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alisimamia mazungumzo ya kupatanisha vyama vya siasa kwa lengo la kurejesha amani Burundi.
Mwalimu Nyerere alianza kukutanisha wawakilishi wa serikali na viongozi wa vyama vya upinzani waliokuwa na uwakilishi katika Bunge la Burundi Mei 1996. Vyama vilivyoshiriki ni Abasa, Anadde, AV-INTWARI, CNDD, Frodebu, Frolina, Inkinzo, Palipehutu, Parena, PIT, PL, PP, PRP, PSD, Raddes, RPB, na Uprona. Moja ya vikundi vilivyokosa uwakilishi ni CNDD/FDD kilichoongozwa na Radjabu Hussein na Pierre Nkurunziza.
Baada ya Mwalimu kufariki dunia Oktoba 1999 aliteuliwa Rais wa Afrika Kusini, Nelson Mandela ambaye alifanikisha mazungumzo hadi yakatiwa saini Makubaliano ya Amani ya Burundi, Agosti 28, 2000.
Museveni hafai
Bahati mbaya, viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamemteua Museveni ambaye siyo mtu sahihi wa kuwapatanisha Warundi. Wakati wa mapambano miaka ya 2000, viongozi wa CNDD/FDD walikuwa wakihifadhiwa Uganda au Rwanda. Paul Kagame na Rais Museveni walifanya ushawishi na kumuunga mkono Nkurunziza ambaye mama yake ni Mtutsi na baba Mhutu, akashinda urais. Ikiwa Museveni ni mshirika wa Nkurunziza, hawezi kuridhia matakwa ya wapinzani.
Kwanza, Museveni ni king’ang’anizi wa madaraka. Huu ni mwaka wa 29 tangu aingie madarakani kijeshi mwaka 1986 na sasa anahangaika kubadili Katiba ili uondolewe ukomo wa mihula miwili; anataka aongezewe kipindi kingine cha miaka mitano (2016 – 2021). Kagame “amefanikiwa” kushawishi Bunge ili uondolewe ukomo katika katiba; Joseph Kabila wa DR Kongo anafurukuta.
Pili, unyanyasaji ni jambo la kawaida kwa Museveni. Nchini Uganda hivi karibuni aliwatia ndani, bila sababu za msingi, wapinzani wakuu wa kisiasa, Kizza Besigye na Amama Mbabazi ili kuendeleza mradi wake wa kuwa “rais wa maisha”.
Tatu, alipokuwa anakwenda Burundi, alitua kwanza Rwanda kwa majadiliano na Kagame. Huko ndiko ilikubaliwa aingie Burundi na askari kadhaa kwa magari badala ya ndege na akaongeza mkanganyiko.
Mosi, aliwaambia wapinzani wasihangaikie ukomo wa kugombea bali namna ya kutajirika. Pili, aliipongeza serikali kwa kuwapokonya silaha imbonerakure akisema “silaha zibaki kwenye mikono ya serikali yenye wajibu wa kulinda wananchi,” kinyume na kinachofanyika Uganda ambako silaha na mafunzo wanapewa raia huku chama chake kikiandaa wanamgambao wa chama chake waitwao Wadhibiti Uhalifu kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2016.
Tatu, aliwachefua wapinzani aliposema: “Mnakilaumu chama tawala lakini ninyi mna matatizo yenu; kwa nini msiwe na mgombea mmoja?”. Akawataka pia wawasilishe vielelezo kuthibitisha kwamba uchaguzi haujaandaliwa vizuri.
Nne, alipinga katakata pendekezo la kuundwa serikali ya mpito akidai kwamba “…inatoa ishara kwamba kuhusu uthabiti wa nchi.” Mazungumzo yamekwama. Imebaki “inkurumbi.”