Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Umaskini hohehahe aibu mbele ya macho yetu

Wao inawabidi waambulie maisha kwa kutegemea kipato cha chini ya dola 1.25 ya Marekani (Sh2,000) kwa siku. Inakubalika pia na wanauchumi kwamba si kazi kubwa kuitokomezea mbali dhuluma hii.PICHA|MAKTABA

Muktasari:

Zaidi na muhimu ni kuwa na mifumo ya kijamii na kisiasa ambayo inamsaidia mkulima kuuza mazao yake.

Tushukuru tumemaliza sherehe za Krismasi kwa salama, huku tukimuomba Mwenyezi Mungu atusambazie amani, neema na mafanikio katika maisha yetu mnamo mwaka huu mpya wa 2014.

Katika kipindi kifupi kilichopita cha furaha, nilitumia dakika chache kutafakari wapi tulikotokea na wapi tuendako. Nilijiuliza; je, sayari yetu hii ya dunia na sisi wanadamu hali zetu zimekuwa bora katika mwaka uliomalizika, ukilinganisha na miaka ya kabla ya hapo?

Hasa nilijiuliza; je, umaskini, tatizo kubwa ninaloliona hapa duniani, tena zaidi ni la kisiasa, bila ya kuyataja mengine, umepungua?

Binadamu wa kisasa anaishi katika neema ambayo hajawahi kuishuhudia katika historia, lakini, hata hivyo, bado wanaishi mamilioni ya watu katika umaskini mkubwa, hohehahe, watoto, wanawake na wanaume bilioni 1.2.

Wao inawabidi waambulie maisha kwa kutegemea kipato cha chini ya dola 1.25 ya Marekani (Sh2,000) kwa siku. Inakubalika pia na wanauchumi kwamba si kazi kubwa kuitokomezea mbali dhuluma hii.

Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, kuwatoa watu kutoka kwenye ufukara zinahitajika katika mwaka dola 169 bilioni za Marekani. Fedha hizo mtu ataziona ni nyingi, lakini ni nusu ya bajeti ya mwaka ya Serikali ya Ujerumani na ni sehemu ndogo ya faida inayopatikana katika masoko ya hisa kwa siku moja duniani.

Kabla ya miaka 30 iliyopita kazi ya kuuondoa umaskini ingegharimu mara mbili zaidi kuliko ilivyo hivi sasa, lakini isisahaulike kwamba nchi kama China, India na nyingine nyingi katika Amerika ya Kusini zimepiga hatua kubwa katika jambo hilo.

Ndio maana hivi sasa, ukilinganisha na mwaka 1980, watu milioni 700 wamepungua kati ya wale wanaotiwa katika mkumbo wa umaskini.

 

Jinsi ya kuushinda umaskini

Vita dhidi ya umaskini wa kukithiri, kwa mujibu wa wanasiasa. Ni jambo lenye matatizo yaliyosongamana. Ni tatizo ambalo halina dawa mujarabu ya aina moja. Hilo si suala la kuwamiminia watu mifukoni mwao Dola za Marekani, Euro za Ulaya wala Yuan za China. Kufanya hivyo si namna ya kuushinda umaskini.

Kuushinda umaskini ni kuwa na mkakati wa kuugawa utajiri wa taifa, mifumo ya kisiasa duniani, na hasa wenye kuisimamia katika nchi mojamoja wawajibike, ufisadi upigwe vita bila ya atiati na kuweko mfumo mzuri wa elimu.

Zaidi na muhimu ni kuwa na mifumo ya kijamii na kisiasa ambayo inamsaidia mkulima kuuza mazao yake.

Hizo dola bilioni 169 zilizotajwa kwamba zinahitajika kwa mwaka zimekisiwa mnamo mwaka 2005 kwa msingi wa uwezo wa watu kunua bidhaa.

Kwa hakika fedha hizo si sura halisi za gharama za kuzikiuka sababu zinazosababisha umaskini wenyewe.

Dhamira ya dhati

Umaskini si jinamizi ambalo sisi wanadamu hatuwezi kulishinda, ikiwa kuna dhamira ya kweli. Lile lengo la milenia la kupunguza umaskini duniani kwa nusu ifikapo mwaka 2030 inaweza kufikiwa.

Inahitajika tu kufanyika mabadiliko makubwa katika ngazi ya dunia. Kwa kweli hali imeboreka katika nchi zinazoinukia, kama vile China na India na hasa kwa watu wa tabaka zenye vipato vya chini au vya wastani.

China inabidi itumie theluthi moja ya uwezo wake wa kiuchumi ili kuwatoa wananchi wake wote kutoka kwenye umaskini.

Hivi sasa serikali inabidi itenge asilimia 0.2 ya pato lake kwa ajili ya shughuli hiyo.

Maskini ni kina nani?

Kwa mujibu wa takwimu, wengi wa watu walio maskini duniani wanaishi maeneo ya mashambani. Hasa wanaoathirika ni watoto.

Mmoja kati ya watu watatu wanaoathirika ni mtoto chini ya umri wa miaka 12. Jinsi zote mbili zinaathirika sawa kwa sawa.

Hata hivyo, wanawake wanaathirika zaidi kuliko wanaume kutokana na ukosefu wa elimu.

Juhudi za kuwaokoa

Zipo juhudi mbalimbali kwa mfano Serikali mpya ya mseto ya Ujerumani, nchi iliyo na nguvu kubwa kabisa ya kiuchumi katika eneo la Umoja wa Ulaya, itatenga euro bilioni mbili zaidi katika miaka minne ijayo kwa ajili ya misaada ya maendeleo.

Fedha hizo hata hivyo hazitatosha kutimiza ile ahadi iliyotolewa na serikali zilizopita za nchi hiyo, kwamba itumike asilimia 0.7 ya mapato jumla ya ndani nchini humo kwa ajili ya jambo hilo.

Hivi sasa Ujerumani inatumia asilimia 0.38 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya misaada ya maendeleo. Hicho ni kiasi cha Euro bilioni kumi.

Leo mtu hahitaji tena kufa kutokana na kukosa chakula. Inahitaji tu nchi tajiri kutimiza ahadi ilizotoa kwamba katika kila Euro 100 walizo nazo, basi angalau zitoe senti 70 za euro kama msaada kwa binadamu wanaolala hoi.

Si haki kuwaachia maskini hao wanashika tu tama, bila ya kuwa na matumaini wa mustakbali.

Tukiwasahau watu hao, dua zetu na furaha zetu za Krismasi na Mwaka Mpya zitakuwa hazina mashiko.

Sayari yetu hii ya dunia ni yetu sote kwa pamoja, kwa hivyo ni aibu pale mkazi mmoja wa sayari hii anaponda mali na mwingine anakufa kwa njaa.