UWT Zanzibar yawaitia uongozi wanawake CCM

Muktasari:
Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) umewataka akina mama kuchangamkia fursa za kugombea uongozi wa ngazi mbalimbali kupitia uchaguzi unaoendelea.
Zanzibar. Huku kukiwa na habari katika baadhi ya maeneo za kusuasua kwa uchukuaji wa fomu za kugombea uongozi wa CCM, chama hicho kimeendelea kuwasihi wanachama wake kuwania nafasi za uongozi.
Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) umewataka akina mama kuchangamkia fursa za kugombea uongozi wa ngazi mbalimbali kupitia uchaguzi unaoendelea.
Kaimu Katibu wa umoja huo Zanzibar, Tunu Juma Kondo alisema hayo wakati wa ziara ya UWT kuzungumza na viongozi wapya wa matawi wa umoja huo eneo la Kaskazini ‘A’ Unguja.
Aprili 28, Makamu Mwenyekiti wa CCM (Zanzibar), Dk Ali Mohamed Shein aliwaambia vijana na makada waliosusia kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali ndani ya chama hicho kuwa kitendo hicho siyo cha uzalendo.
Kauli hiyo ya Dk Shein ilifuatia ile ya Katibu wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja, Sauda Mbamba aliyesoma taarifa ya mkoa huo katika hafla maalumu ya kukabidhi vifaa vya michezo kwa vijana wa Jimbo la Uzini, akisema vijana wengi hawachukui fomu hizo.
Ikiwa ni kama majibu kwa vijana hao, Dk Shein alisema suala la msingi ni kuwa na uzalendo ambao ndiyo mwongozo sahihi katika kulinda heshima na nidhamu ya mtu kwenye jamii na Taifa kwa ujumla.
“Kilio kikubwa cha vijana hao inawezekana ikawa ni suala la ajira, lakini suala hilo ni gumu kwani haiwezekani kila mtu kuajiriwa na Serikali kama wengi wanavyotaka,” alisema.
Makamu huyo wa mwenyekiti wa CCM alisisitiza kuwa ajira ni changamoto kubwa kutokana na sasa idadi ya watu visiwani humo kuwa ni kubwa.
“Hivi sasa Zanzibar tumeongezeka sana na hili linachangiwa na sisi wenyewe kwa kuzaa sana, hivyo ni vigumu kila mmoja kupata ajira serikalini kwa kuwa utaratibu wa ajira hauko hivyo,” alisema Dk Shein.
Awali, Sauda alimwambia Dk Shein kuwa pamoja na chama kutangaza kwa vijana kuchukua fomu za uongozi, bado fomu hizo zimedoda matawini.
Pia, katibu huyo alisema jambo hilo linahitaji nguvu ya pamoja ya viongozi wakuu wa chama hicho kuwashawishi vijana kuchukua fomu hizo, ili kuomba uongozi katika ngazi za CCM.
Hata hivyo akizungumza wilayani Kaskazini ‘A’ Unguja jana, Tunu alisema uchaguzi huo unaweza kuwa fursa nzuri ya wanawake kupata nafasi za uongozi na kuwawezesha kufikia malengo ya kupata uwakilishi wenye idadi sawa na wanaume ndani ya chama hicho.
Alisema wanawake wanatakiwa kuondokana na dhana ya kuendelea kuongozwa kwa kila nafasi ndani ya CCM, bali wajiongeze kwa kuwania uongozi.
Tunu alisema ushiriki wao utawezesha kupata viongozi makini na wenye uwezo wa kwenda na kasi za kiutendaji za chama hicho.
Katibu Msaidizi wa Idara ya Oganaizesheni UWT (Zanzibar), Mgeni Ottow alisema CCM itadumu madarakani endapo viongozi wanaopatikana kupitia uchaguzi watakuwa na uzalendo wa kweli katika kulinda masilahi ya taasisi hiyo kwa vitendo.
“Lazima tuwe wa kwanza kujitokeza kwa kila tukio linalohusu uimarishaji wa chama na hasa michakato ya uchaguzi,” alisema.
Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Kaskazini Unguja, Miza Ali Kombo alisema uchaguzi ngazi ya wadi unaendelea na kwamba, wagombea wamejaza fomu na kinachosubiriwa ni upigaji kura ili kupata viongozi wapya na bora.