Sina Makosa wa Les Wanyika unatokana na kisa cha kweli

Muktasari:
- Wimbo huu ulitungwa na Omari Shaabani, maarufu kwa jina la Profesa Omari ambaye alikuwa kiongozi na mpiga gitaa la rhythm katika bendi ya Les Wanyika.
Si ajabu kusikia wasanii wakiwa katika mgogoro au kutoelewana. Iwe ni kwa masuala yanayohusiana na muziki au maisha binafsi.
Kutandikana makonde wanamuziki si jambo geni. Pombe, mapenzi na hata ubishi wa kitaaluma umekuwa sababu tosha za wanamuziki kukosa staha na kuamua kumaliza tofauti zao kwa kutiana ngeu.
Wakati nawaza hili, kuna nyimbo mbili ambazo zinanijia kichwani zilizotokana moja kwa moja na wanamuziki kuwemo katika timbwili la ugomvi.
Nyimbo hizi zinaonyesha bado umahiri wa kujibu ngumi kwa muziki na ukiangalia ukweli, kutunga nyimbo hizi kumefanya mwanamuziki aibuke mshindi katika mpambano huo kwani nyimbo nitakazozitaja zilitungwa miaka zaidi ya 25 iliyopita na bado zinatamba.
Katika wimbo mmoja wahusika wote hatunao tena dunia. Wimbo wa kwanza ni maarufu wa Les Wanyika uitwao Sina Makosa. Wimbo huu ulikuwa maarufu mpaka ukawa kama wimbo wa Taifa wa Afrika ya Mashariki, kwani ulipigwa kila mahala duniani ambapo walipokuwapo wapenzi wa muziki kutoka Afrika ya Mashariki.
Wimbo huu ulitungwa na Omari Shaabani, maarufu kwa jina la Profesa Omari ambaye alikuwa kiongozi na mpiga gitaa la rhythm katika bendi ya Les Wanyika.
Kundi lililojitenga kutoka bendi ya Simba wa Nyika. Muimbaji kiongozi katika wimbo huo alikuwa Issa Juma, waliokuwa wakijibu ni John Ngereza ambaye pia alikuwa anapiga solo akishirikiana na Mohamed Tika.
Huyu John Ngereza alitokea bendi ya Amboni Jazz kutoka Tanga na umahiri wake wa kuimba unajitokeza katika nyimbo kama Afro, Amigo na Nimaru. Issa Juma sauti yake husikika vizuri katika nyimbo za Les Wanyika kama Pamela, Kasuku na Paulina.
Turudi kwenye mada yetu, chanzo cha wimbo Sina Makosa kilikuwa ni binti mmoja mzaliwa wa Kisumu aliyekulia Nairobi na alikuwa akifanya kazi kwenye shirika la mawasiliano la Kenya.
Wadhifa wake na maisha yake yalikuwa mazuri. Pia alikuwa mpenzi mkubwa wa bendi ya Les Wanyika na hatimaye akakutana na Profesa Omari na kuwa na uhusiano wa kimapenzi, japo ulikuwa siri kwani binti alikuwa na bwana mwingine ambaye alikuwa anafanya kazi katika idara ya usalama iliyoitwa Special Branch.
Kuingia ubia wa mapenzi na mtu wa usalama katika nchi nyingi Afrika si suala la busara hata kidogo. Huyu bwana wa usalama alikuwa na familia yake.
Siku moja Profesa na mpenzi wake walikuwa wamekaa katika mgahawa uliokuwepo Kenya Cinema ndipo wakakutwa na huyu ofisa wa Special Branch.
Alianzisha vurugu kubwa na kutoa kipigo kikali kwa Profesa ambaye aliokolewa na wapenzi wa muziki waliomfahamu. Pamoja na mkasa huo binti aliendelea kuwa mpenzi mkubwa wa Les Wanyika hata wimbo ulipotungwa na kupata umaarufu alikuwa pembeni mwa Profesa.
Hasira za nini bwana,
Wewe una wako nyumbani
Mimi nina wangu nyumbani
Chuki ya nini kati yangu mimi na wewe
Wataka kuniua bure bwana
Nasema sina makosa baba
Wimbo mwingine ambao unanijia kichwani ni Jogoo la shamba uliopigwa na Morogoro Jazz Band. Bendi hii iliyoanza mwaka 1944 katika Mji wa Morogoro ilikuwa maarufu sana katika miaka ya 60 na 70.
Mkasa wa wimbo huu unasemekana ulianza na kisa cha bwana mmoja ambaye pamoja na kuwa fundi cherehani mzuri, pia alikuwa akipenda sana mazoezi ya kujenga misuli, hili lilimfanya awe na mwili uliojazia na kumpa uwezo wa kufanya ubabe mwingi ikiwemo hata kuingia katika madansi kwa nguvu bila kulipa kiingilio.
Bwana huyu inasemekana aliwahi kumshawishi Mbaraka na kumpeleka kujiunga na Kilombero Jazz Band, iliyokuwa Kilombero ambako ndiko kwao mbabe huyu.
Mbaraka hakukaa huko akarudi Moro Jazz na ndipo ‘bif’ likaanza kwa huyu jamaa kumfanyia fujo Mbaraka kila alipokutana naye. Hatimaye siku moja alimkuta Mbaraka na watu wake wa karibu wakiburudika kwa vinywaji kama kawaida akaanzisha timbwili lake la kibabe, mdogo wake Mbaraka, aliyeitwa Zanda akawa amechoka na uonevu huo akaamua kumkabili mbabe huyu na zikaanza kupigwa ngumi.
Mbaraka akaondoka na kuelekea kwake na kuamua kuacha hata bendi kutokana na kukerwa na usumbufu wa huyu mbabe. Jambo hili likaiathiri bendi kwa kuanza kukosa wapenzi, hivyo wanamuziki wenzie wakamfuata na kumtaarifu kuwa wanataka arudi kazini na kuna mambo ambayo wamerekibisha.
Moja likiwa ni kumtafutia Mbaraka walinzi wawili ambao walipelekwa kutoka Dar es Salaam, hao wakawa naye kila anapokwenda, jambo la pili ni wenzie walimwambia kuwa wametunga wimbo uliohusu mbabe yule kupigwa na mdogo wake Mbaraka.
Hapo ndipo Mbaraka akarudi katika bendi na kushiriki kupiga solo na kuimba wimbo huo ambao ni maarufu mpaka leo.
Hiloo, Ulijidai wewe mbabe sana,
Leo umepigwa na kijana mdogo,
Aibu imekupata,
Kiko wapi sasa, ulichokuwa ukijidai nacho,
Je ungepigana na mimi kaka kilema ungekipata.