Don Bosco Uwanja pekee wa mchezo wa kuteleza Tanzania

Muktasari:
- Uwanja wa Don Bosco Skate Park-Dodoma ulikamilika Julai 2011 na kuzinduliwa Februari 2012.
Hapa nchini kumekuwa na aina mbalimbali ya michezo ambayo imekuwa ikipata umaarufu kila kukicha. Baadhi ya michezo hiyo ni soka, mpira wa pete, kikapu, ngumi,tenisi na mingine mingi.
Michezo kama soka na mpira wa pete ni michezo ambayo kila kona ukipita utakutana na wachezaji wakicheza kwenye viwanja tofauti hapa nchini huku Serikali ikiitambua kwa kiasi kikubwa michezo hiyo na wakati mwingine hutoa ushirikiano kwa kuzisaidia timu mbalimbali hasa zile za taifa za michezo hiyo.
Lakini hivi sasa kuna mchezo mwingine nchini ambao siyo maarufu sana unaoitwa ‘skate boarding’ au mchezo wa kuteleza. Ni mchezo ambao hauna tofauti na ile ya kutembea kwenye mabarafu, lakini katika mchezo huu wachezaji hawatumii mabarafu.
Ni moja ya michezo ambayo imekuwa ikipendwa sana katika nchi za Ujerumani na Marekani, lakini kwa sasa umeanza kupendwa na vijana wengi sehemu mbalimbali duniani, ambapo vijana wengi wamekuwa wakiucheza kwa kiasi kikubwa hata katika nchi za Afrika Mashariki na kati.
Mchezo huu huhitaji umakini na ari pamoja na nia thabiti hasa katika kujifunza hususani kwa wanaoanza. Ama kwa hakika ukipata bahati ya kujionea jinsi vijana hawa wanavyocheza mchezo huu utavutiwa na kupendezwa. Usanifu na umakini katika kuruka juu ya viunzi mbalimbali na namna wanavyobadilisha mfumo katika uendeshaji wao huo.
Zipo jitihada mbalimbali zinazofanyika katika kuhakikisha mchezo huu wa kuteleza unafanikiwa nchini. Jumuiya ya Don Bosco, Dodoma kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi pamoja na jitihada za Shirika la SKATE-AID la Ujerumani wamesaidia kujengwa kwa kiwanja cha kwanza hapa Tanzania kwa ajili ya mchezo ya kuteleza.
Uwanja wa Don Bosco Skate Park-DODOMA ulikamilika Julai 2011 na kuzinduliwa mnamo Februari 2012. Uwanja huu kwa sasa ndiyo wa pekee hapa Tanzania na wa pili kwa Afrika Mashariki kufuatia ule wa Kintale Skate Park-Kampala (Uganda).
Uwanja huu wa mchezo wa kuteleza unamilikiwa na timu ya Tanzania Skate Miracle iliyo chini ya chuo cha Don Bosco kilichopo mjini Dodoma.
Ni uwanja ambao ukiungalia unaweza kuudharau, lakini chuo hicho kimetumia gharama kubwa kuujenga na ndiyo maana hakuna viwanja vingine vya mchezo huo wa kuteleza hapa nchini kwani ni gharama kuvijenga.
Spoti Mikiki ilifika kwenye uwanja huo wa Don Bosco Skate Park uliopo Dodoma wakati wa mashindano ya mchezo huo ambayo yanaendelea hivi sasa kwa kushirikisha wachezaji vijana na wale wenye rika la kuanzia miaka 10 hadi 15.
Mkurugenzi wa chuo cha Don Bosco Dodoma, Jose Padinjaparampil anasema kuwa uwanja huo ulianza kutumika mwaka 2012 baada ya kukamilika kwa hatua za awali.
Padinjaparampil anasema Shirika la Skate Aid la Ujerumani ndiyo lililosaidia kuhakikisha uwanja wa Don Bosco Skate Park unajengwa pamoja na ule wa Kintale uliopo Uganda ikiwa chini ya mhandisi Mjerumani Raif Mier.
Mkurugenzi huyo anasema uwanja huo umegharimu zaidi ya milioni 100 kuujenga mpaka unamalizika, ambapo amelishukuru shirika hilo kwa msaada wa uwanja huo pekee hapa nchini ambao amesema ni moja ya vivutio mjini Dodoma.
Anasema kuwa bado muitikio ni mdogo kwa wachezaji kutokana na wengi kutoufahamu mchezo huo hatua ambayo inafanya sasa kuamua kutumia watoto kuanzia miaka 10 kuweza kuwafundisha mchezo huo ambapo amesema lengo lao ni kuhakikisha wanazalisha wachezaji wengi ili baada ya miaka mitatu mchezo huo utambulike hapa nchini.
“Usione hivi huu uwanja umetumia zaidi ya milioni 100 ambapo kwa gharama hii unaweza kujenga viwanja vya kikapu, mpira wa pete na wa mikono kwa wakati mmoja na hiki ndicho kiwanja pekee hapa nchini cha mchezo huu,”anasema Padinjaparampil.
Kwa upande wake mchezaji na mkufunzi wa mchezo huo katika chuo cha Don Bosco Dodoma, Agustino Lutasingwa anasema uhaba wa viwanja ndiyo unaofanya mchezo huo kukosa hamasa kubwa hapa nchini hatua ambayo anasema wachezaji wengi wamekuwa wakicheza mchezo huo kwenye maegesho ya magari kwenye hoteli za kitalii hasa jijini Dar es Salaam.
Lutasingwa anasema pia gharama za kununulia seti nzima ya vifaa vya mchezo huo ni sh 100,000 ambazo ni fedha nyingi kwa wachezaji ambao wengi wao ni vijana wasiokuwa na ajira yoyote hali ambayo inafanya mchezo kutoweza kukubalika kwa kiasi kikubwa.
“Huu mchezo kwa kweli hapa nchini bado sana hakuna viwanja. Kipo hiki kimoja tu basi, hali inayosababisha vijana wanaocheza mchezo huu kwenda kuucheza katika maegesho ya magari na barabarani jambo ambalo ni hatari kwao, lakini kama kungekuwa na viwanja vingi hamasa ingekuwa kubwa,” anasema Lutasingwa.
Erick Ndole ambaye ni msimamizi wa Uwanja huo anasema kuwa kwa sasa wao wanachokifanya ni kufundisha watoto mchezo huo ambao wameanza kuupenda na lengo lao kuu ni kutaka kuwa na timu nzuri ndani ya miaka mitatu.
“Hivi sasa kuna haya mashindano. Hapa sisi tunachokifanya ni kuhakikisha tunaibua vipaji vya vijana hapa Dodoma na watoto wengi wameshaanza kuutambua huu mchezo kwa kiasi kikubwa,” anasema Ndole.