Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mtu hatari katika kupanga matokeo ya soka

Wilson Raj Perumal (kulia) akiwa mahakamani katika moja ya kesi zake za upangaji wa matokeo ya mchezo wa soka. Picha zote na AFP     

Muktasari:

Perumal alipanga matokeo katika michezo ya Olimpiki, kufuzu kwa Kombe la Dunia, Kombe la Dunia la Wanawake, michuano ya CONCACAF na Fainali za Mataifa ya Afrika.

Alianza taratibu kazi ya kupanga matokeo ya mechi za soka katika ligi ndogo kabla ya kuingia katika ngazi ya kimataifa na kuingizia mamilioni ya Dola za Marekani.

Ila kumbuka hii siyo historia ya mchezaji soka shujaa. Hii ni historia ya shujaa wa upangaji wa matokeo ya soka, mtu hatari katika kuharibu matokeo ya kweli ya soka duniani.

Unaweza usilitambue kirahisi jina la Wilson Raj Perumal, lakini utakapoambiwa vitendo alivyofanya, unaweza kutamani kushuhudia moja ya mechi alizozibadili matokeo.

“Kwa kweli sikumbuki idadi ya mechi nilizopanga matokeo, lakini zinaweza kuwa mechi kati ya 80-100 za soka,” Perumal aliiambia CNN katika mahojiano ya kwanza kuwahi kufanyika na mpanga matokeo huyo.

“Wakati mwingine nilikwenda katika benchi na kuzungumza na wachezaji nini cha kufanya, kutoa maagizo kwa kocha, ilikuwa rahisi kiasi hicho.”

Anasema maofisa wa mechi walikuwa rahisi kuwashika, hakukuwa na mipaka wakati wa kuwaomba juu ya kuchagua waamuzi fulani, baadhi ya mashirikisho ya soka yalinipokea kwa mikono miwili,” alisema Perumal.

Baada ya kukamatwa na kuachiwa 2011, ikiwa ni mara ya nne kutiwa hatiani kwa uhalifu wa kupanga matokeo ya soka, Perumal aliamua kuanza maisha mapya kutoka katika maisha yake ya zamani, ambapo hivi sasa anawasaidia polisi wa Ulaya kuwakamata wapangaji wa matokeo.

Wakati alipokuwa akishiriki katika uhalifu wa upangaji wa matokeo, Perumal anadai kuwa alifanikiwa kukusanya kiasi cha Dola 5 milioni peke yake.

Hata hivyo, alizipoteza fedha zote hizo katika kamari na labda ndiyo sababu ya mtu huyu mwenye miaka 49 aliandika kitabu cha maisha yake kiitwacho ‘Kelong Kings’, akielezea maisha yake kuanzia alipoanza kuharibu soka mjini Singapore, alipokuwa akijiita mwenyewe ‘Mr Fix-it’.

“Nilikuwa na ndoto tangu nikiwa mdogo. Nilitaka kuwa askari wakati nikiwa shuleni na nilikuwa na rekodi ya matukio polisi hivyo nilishindwa kufikia kile nilichotaka.

“Kuanzia hapo nikavutiwa na mchezo wa kamari (betting) wakati nikiwa na miaka kati ya 19-20. Nilivutiwa na kuuzoea na sikutaka tena kuacha, hivyo nilianza kucheza na matokeo ya timu za ligi ya nyumbani,” anasema.

Perumal alianza mchezo huo katika michezo ya ligi ya Singapore mwishoni mwa miaka ya 1980 kabla ya kuingia katika michezo ya kimataifa na kusakwa na askari wa kimataifa (INTERPOL) akitajwa kama mtu hatari zaidi katika kupanga matokeo akiongozwa na Tan Seet Eng ‘Dan Tan Eng’ ambaye hivi sasa yupo kifungoni nchini Singapore.

Baada ya kutambulishwa kwa huduma za intaneti kwa mara ya kwanza miaka ya 1990, wigo wa Perumal katika kuendeleza tabia yake chafu ya upangaji wa matokeo iliongezeka.

“Tuliziona mechi zote duniani, nilikuwa na uwezo wa kuzilenga nchi kadhaa, nchi ambazo watu wake ni rahisi kukubali rushwa.

“Hivyo nilisajili kampuni na kuanza kuyatumia barua pepe mashirikisho ya soka na kuunga nao urafiki,” anasema Perumal.

Perumal alianza kuhusishwa katika upangaji wa matokeo ya mchezo wa kimataifa wa kirafiki 1997, uliokuwa kati ya Zimbabwe na Bosnia Herzegovina, ambapo hata hivyo alifeli.

Perumal alisema wachezaji sita wa Zimbabwe walikubali dili hilo la kupoteza mchezo kwa mabao 4-0 kwa makubaliano ya malipo ya Dola 100,000, lakini mchezo huo uliopigwa mjini Kuala Lumpur, Malaysia, ulimalizika kwa sare ya mabao 2-2.

“Tuliwapa matokeo tunayoyataka, lakini ilikuwa ngumu kuyatimiza na kilichotokea ni kama vile mchezaji mmoja alipiga mpira wavuni kwake kwa bahati mbaya,” anasema.

Miaka 10 baadaye, Perumal aliilenga Zimbabwe tena katika kile kilichoitwa skendo ya ‘Asiagate’, ambapo wachezaji na maofisa wa mchezo husika walipokea rushwa kupanga matokeo katika michezo kati ya 2007 na 2009.

“Tulikuwa kama mikono miwili ambayo ilikuwa ikijiandaa kupiga makofi,” Perumal anasema.

Mpelelezi wa zamani wa Fifa katika masuala ya upangaji wa matokeo, Terry Steans alishtushwa alipopewa faili la upangaji wa matokeo nchini Zimbabwe 2009.

“Nililisoma lile faili na kusema ‘hapana, haiwezekani’!. Haiwezi kuwa rahisi namna hii,’” Steans aliiambia CNN.

“Miaka mitano baadaye, niligundua kweli kulikuwa na udanganyifu, lakini faili lile lilifumbua macho yetu na kuifanya FIFA kuongeza ulinzi na kwa wakati huo, tulianza kufanyia kazi taarifa zote za upangaji wa matokeo kote uliposambaa mchezo huo.”

Soka ya Zimbabwe iliathiriwa na skendo ya upangaji wa matokeo, kwa mujibu wa Steans.

Wachezaji wengi na maofisa walifungiwa na kupewa onyo, wakati wengine walifungiwa maisha, huku wachezaji wengine wakifungiwa kucheza kwa miaka kadhaa. Chama cha Wanasoka wa Zimbabwe kilikuwa kikali juu ya uamuzi wa Shirikisho la Soka la Zimbawe (ZIFA) kuhusu uchunguzi waliofanya, lakini Steans alisema shirikisho hilo linastahili pongezi kwa hatua walizochukua.

“Waliunda Kamati ya Uchunguzi na walifanya uchunguzi wao kwa kadri walivyoweza kwa mujibu wa taarifa walizokuwa nazo,” anasema.

CNN waliwaalika ZIFA katika mjadala huo juu ya upangaji wa matokeo, lakini hawakuzungumzia chochote hadi walipochapisha taarifa hizo.

Kifungo mara tatu:

Perumal anasema alifanikiwa kupata asilimia 70-80 ya mafanikio katika upangaji wa matokeo kwenye michezo ya Olimpiki, kufuzu kwa Kombe la Dunia, Kombe la Dunia la Wanawake, michuano ya CONCACAF na Fainali za Mataifa ya Afrika.

Lakini si mara zote amekuwa anakifanikiwa katika suala la kupenyeza rushwa na hasa mjini Singapore ambapo amekuwa akitiwa hatiani na hata kwenda jela mara tatu kutokana na masuala yahusuyo soka.

Mwaka 1995, alifungwa kwa miezi 12 kutokana na jaribio lake la kutoa rushwa kwa mchezaji. Miaka minne baadaye alifungwa miezi 26 kwa kumtaja mwamuzi kama mpangaji matokeo na 2000 alimshambulia mchezaji kwa fimbo ya kuchezea mpira wa magongo, akisema ni moja ya matukio yanayomhuzunisha na kumfanya kujuta.

Mwaka 2011, maofisa wengine waliingia tena katika mtego wa Perumal, safari hii ilikuwa nchini Finland, ambapo alikamatwa kwa tuhuma za kupanga matokeo ya mechi za Veikkausliiga, ambayo ni Ligi Kuu nchini humo.

Perumal alitumikia mwaka mmoja kati ya miwili aliyohukumiwa kabla ya kwenda Hungary, ambapo aliwasaidia polisi katika uchunguzi wa matukio ya upangaji wa matokeo katika ligi ya Balkans.

Steans alishangazwa na orodha ya matukio ya Perumal baada ya polisi kumuonyesha makosa aliyofanya mtu huyo.

“Perumal ana nchi 38 katika orodha ya majina katika simu yake anayowasiliana na maofisa wa huko, ana majina ya maofisa wa mashirikisho ya soka, wachezaji na waamuzi wa nchi hizo 38,” Steans aliendelea kuiambia CNN.

“Ukiingia katika orodha ya watu anaowasiliana nao katika kompyuta mpakato yake (laptop), kuna majina zaidi ya 50. FIFA ina wanachama 209, hivyo tunazungumzia nusu ya wanachama wa FIFA wanaofanya kazi na mpanga matokeo mmoja,” aliongeza.

“Kwa kufahamu hilo sasa, aliwatumia watu wengi kati ya hawa na wote anawatumia kwa kuingiza fedha nyingi.”

Angeweza kuwa amesahau kila kitu alichopitia katika maisha hayo ya udanganyifu, lakini Perumal aligeuka nyuma katika kipindi cha maisha hayo na kukumbuka vingi.

“Sijutii chochote nilichowahi kufanya. Ni kama ilikuwa sehemu ya maisha niliyotakiwa kuyapitia, na nafurahia hali ile na kusafiri katika nchi mbalimbali duniani. Nilikuwa na wakati mzuri.”

Kuna wakati unahisi kuwa alifanya vitu vya kuumiza. Perumal anasema anajisikia mkosaji kwa kuharibu baadhi ya matokeo ya mechi, lakini tena anakiri kuwa hajutii katika michezo mingine.

“Soka si mchezo tena kwa sasa. Ni kama biashara kwa maisha ya wakati huu. Nafikiri tulikuwa tunajaribu kutengeneza fedha katika biashara hii. Watu wanataka kushinda na wanafanya kila liwezekanalo kupata matokeo mazuri.”

Perumal anasema alizisaidia Nigeria na Honduras kufuzu Fainali za Kombe la 2010 kwa staili yake ya kupanga matokeo.

Vita ya uwanjani:

FIFA inasema kuulinda na kuheshimu soka ndiyo kipaumbele chao kikubwa na 2011 walitangaza kuwapa INTERPOL Euro 20 milioni (Dola 26.5 milioni) kwa ajili ya kupambana na wapangaji wa matokeo.

“Tulichukua kila taarifa zilizohusu upangaji wa matokeo kwa umakini mkubwa na kufanyia uchunguzi taarifa hizo,” ilisema Idara ya Habari ya FIFA katika mahojiano na CNN kupitia barua pepe (email).

“Bila shaka tuna taarifa mbalimbali ikiwamo ile ya ‘Kelong Kings.’ Hatuwezi kuzungumzia zaidi juu ya jinsi tunavyofanya kazi na hatuwezi kuwashirikisha katika ripoti zetu za uchunguzi.

“FIFA inaendelea kufanya kazi na mashirika madogo ya uchunguzi pamoja na mamlaka mbalimbali za kijamii na vyama vingine vya michezo katika ngazi ya kila nchi juu ya upangaji wa matokeo.”

Lakini Perumal anaamini kuwa shirikisho hilo lenye dhamana ya kusimamia soka duniani linatakiwa kuongeza nguvu zaidi katika hilo.

“FIFA bado haina mbinu au njia, ama matangazo au hata elimu kwa jamii kwa ajili ya kupambana na suala zima la kupanga matokeo,” anasema Perumal.

“FIFA inafanya kazi kubwa ya kutokomeza ubaguzi, lakini nafikiri upangaji wa matokeo ni mbaya zaidi ya ubaguzi. Sisemi kwamba haikuwekeza fedha katika kutokomeza ubaguzi, lakini ninachomaanisha ni kwamba upangaji wa matokeo ni suala baya zaidi.”

Steans anasema Perumal ana thamani ya fedha katika suala la uchunguzi wa masuala ya upangaji wa matokeo.

“Wilson ni mtu wa ‘mgumu kuelewa’,” alisema na kuongeza: “Lakini unajua, kila taarifa aliyotoa wakati wa uchunguzi wa sakata hili nchini Finland na Hungary ilikuwa sahihi.”

Mfanyakazi huyo wa zamani wa FIFA bado anaendelea na vita dhidi ya upangaji wa matokeo, akifanya kazi katika kampuni ya kupambana na rushwa michezoni.

Lakini katika mawazo yake, anahofia zaidi mchezo wa soka kufa endapo upangaji wa matokeo utakuwa ukiendelea.

“Unadhani mashabiki wataangalia? Tunaweza kuishia kwa mtindo unaofanana na Zimbabwe, ambapo mashabiki hawajitokezi kuangalia mechi za soka, wadhamini wamejitoa, mwisho wa siku tutakuwa mchezo wa soka usiokuwa na lolote.

“Wakati mchezo wa soka ukiwa hauna maana, wadhamini wataukataa na mashabiki vilevile. Timu zitakuwa zikicheza katika viwanja visivyokuwa na mashabiki. Itakuwa ni kama jangwa.”

=================

Nukuu

“Soka si mchezo tena kwa sasa. Ni kama biashara kwa maisha ya wakati huu. Nafikiri tulikuwa tunajaribu kutengeneza fedha katika biashara hii. Watu wanataka kushinda na wanafanya kila liwezekanalo kupata matokeo mazuri,” Wilson Raj Perumal.

“Wilson ni mtu wa ‘mgumu kuelewa’,” alisema na kuongeza: “Lakini unajua, kila taarifa aliyotoa wakati wa uchunguzi wa sakata hili nchini Finland na Hungary ilikuwa sahihi,”Terry Steans, mpelelezi wa zamani wa FIFA.

“Tutaishia kuwa na mchezo ambao utakosa nidhamu, na hadhi ya mchezo wenyewe kushuka huku mashabiki wasijue wanaangalia nini,” Terry Steans, mpelelezi wa zamani wa FIFA.