Vumbi kila kona ligi kii 2015/2016

Wachezaji wa Azam wakishangilia
Muktasari:
Yanga inashikiria rekodi ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara 25.
Msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara (Vodacom Premier League) unatarajia kuanza mwezi ujao, ukitanguliwa na mchezo wa Ngao ya Jamii baina ya Yanga na Azam utakaofungua pazia la ligi hiyo, Agosti 22.
Ili kujiandaa vyema na msimu ujao wa Ligi Kuu, timu 16 zitakazoshiriki ligi hiyo zimeanza mikakati, mipango kamambe ya kuhakikisha zinafanya vyema na ikiwezekana kumaliza kwenye nafasi za juu katika msimamo wa ligi mwishoni mwa msimu.
Spoti Mikiki inakuletea mikakati hiyo pamoja na maandalizi yanavyofanywa na timu 16 zitakazoshiriki Ligi Kuu msimu wa 2015/2016.
1-African Sports
Hawa ni watani wa jadi wa Coastal Union ya Tanga, ambao msimu ujao wataanza kuonekana tena kwenye Ligi Kuu baada ya kusota kwa muda mrefu wa zaidi ya miaka 20 wakiwa Ligi Daraja la Kwanza.
Timu hiyo, maarufu ‘Wanakimanumanu’ imeimarisha benchi lake la ufundi kwa kumpa mkataba kocha wa zamani wa makipa wa Yanga, Razack Siwa mwenye uzoefu wa kutosha wa soka la Tanzania akiwa amewahi kuzifundisha pia Coastal Union na Toto Africans ya Mwanza.
Kuhusu usajili, timu hiyo imetenga kiasi Sh 60 milioni kwa zoezi hilo na hadi sasa imeshanasa wachezaji wazoefu, Nsa Job, Jaffari Kibaya na Hassan Khatib.
2-Azam
Katika kuhakikisha hairudii makosa yaliyojitokeza msimu uliopita ilipojikuta ikipoteza ubingwa na kumaliza ligi kwenye nafasi ya pili nyuma ya Yanga, Azam iliamua kufanya marekebisho kwenye benchi la ufundi kwa kumrudisha kundini kocha wake wa zamani, Stewart John Hall.
Kocha Mganda, George Nsimbe ‘Best’ ambaye ameondoka alirudi kuwa kama kocha msaidizi, ingawa pia ilimleta nchini Mromania Mario Mariana ambaye ni kocha wa viungo.
Kwenye usajili, Azam imefanya usajili wa wachezaji wapya ambao ni, Ame Ally ‘Zungu’, Ramadhan Singano ‘Messi’, Baptiste Mugiraneza ‘Migi’na Allan Wanga kutoka Kenya.
Mara nyingi timu hiyo imekuwa ikiweka kambi yake kwenye uwanja wake, Azam Complex uliopo Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, ingawa kwa sasa ipo visiwani Zanzibar ilikoweka kambi.
3-Coastal Union
Baada ya kusuasua kwenye ligi msimu uliopita na kuponea chupuchupu kushuka daraja, timu hiyo yenye jina la utani, ‘Wagosi wa Kaya’ inaonekana kujiandaa vilivyo kwa ajili ya msimu ujao Ligi Kuu kutokana na usajili kabambe ilioufanya.
Tayari, imemnasa mshambuliaji Mnigeria, Chidiebere Abasilim kutoka Stand United ya Shinyanga. Wachezaji wengine na timu walizotoka kwenye mabano ni; Ibrahim Twaha (Simba), Nassor Kapama, Ernest Mwalupwani (Ndanda), Adeyum Saleh (JKU), Sultan Juma, Ahmed Shiboli (African Sports), Mohamed Suma na Yassin Mustafa ‘Evra’ kutoka Stand United.
Pia, timu hiyo imemwajiri aliyekuwa kocha mkuu wa Kagera Sugar, Jackson Mayanja anayesifika kwa falsafa ya soka la kuvutia.
4-JKT Ruvu
Maafande hao wanaendelea na maandalizi yao kimyakimya wakiwa na imani kuwa wanaweza kuwashangaza wengi kwenye Ligi Kuu msimu ujao.
Chini ya kocha mzoefu, Felix Minziro au Majeshi, JKT Ruvu imeshaanza mazoezi yake kwa ajili ya kujiandaa na Ligi Kuu huku ikijivunia usajili wa wachezaji kama Saad Kipanga, Gaudence Mwaikimba na Amour Omary ‘Janja’.
5-Kagera Sugar
Ingawa timu hiyo maarufu ‘Wanankulukumbi’ inaonekana kuwa kimya, imekuwa ikiendelea kimya kimya na maandalizi ya Ligi Kuu.
Timu hiyo ni miongoni mwa klabu zilizoanza mapema maandalizi ya Ligi Kuu kwa kuingia kambini chini ya kocha wa mpya, Mbwana Makata alizawadiwa tuzo ya kocha bora wa Ligi Kuu msimu uliopita. Hadi sasa, usajili wake umekuwa wa kimya.
6-Majimaji
Baada ya kutumia nguvu kubwa kupanda Ligi Kuu, Majimaji au ‘Wanalizombe’imeweka mikakati mizito ya kuhakikisha inafanya vyema kwenye Ligi Kuu msimu ujao na kurejesha heshima yake ya siku za nyuma.
Kwanza, ilitenga bajeti ya Sh 100 milioni kwa ajili ya usajili na imefanikiwa kuwanasa wachezaji David Burhan, Iddi Kipagwile na Kelvin Friday anayetokea Azam huku pia ikiwawania wachezaji Rajab Zahir na Gaudence Mwaikimba.
Kwa kuonyesha jeuri ya fedha, timu hiyo nayo imemleta nchini kocha mzungu, Mika Lonnstrom kutoka Finland na tayari imeshaingia kambini kuanza maandalizi ya msimu mpya.
7-Mbeya City
Wagumu wa Mbeya baada ya kuporomoka nafasi yao ya tatu waliyomaliza nayo kwenye msimu wao wa kwanza Ligi Kuu mpaka nafasi ya nne kwenye msimu uliopita, Mbeya City imeamua kuimarisha kikosi chao kwa kusajili wachezaji watakaoirudisha kwenye chati huku tayari ikiwa imeshaingia kambini.
Timu hiyo imeondokewa na baadhi ya nyota waliotua Simba, Yanga, lakini imebaki na kocha wake, Juma Mwambusi pamoja na wachezaji, Ken Ally, Raphael Alfa, Hamad Kibopile na Steven Mazanda. Pia, imemsajili Joseph Mahundi kutoka Coastal Union na Gideon Benson wa Ndanda.
8-Mgambo
Maafande hao wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambao kila mwaka wamekuwa wakiponea kwenye tundu la sindano kushuka daraja, wameanza maandalizi yao mapema kwa kujifungia kambini mkoani Tanga. Katika kuimarisha kikosi chao, Mgambo JKT imewapandisha baadhi ya nyota wa kikosi chao cha vijana ambacho kimekuwa kikifanya vizuri kwenye mashindano mbalimbali ya vijana.
9-Mtibwa Sugar
Awali, ilidaiwa kuwa Mtibwa Sugar inataka kulifanyia marekebisho makubwa benchi la ufundi kwa kumwondoa kocha wao mzalendo, Mecky Maxime na kumleta kocha mzungu, lakini uongozi wa klabu hiyo ulikanusha taarifa hizo na kuamua kuendelea na maisha chini ya nahodha huyo wa zamani wa Taifa Stars.
Timu hiyo imeweka kambi jijini Dar es Salaam kwenye hoteli ya Itumbi, Magomeni huku ikifanikiwa kuwanasa nyota wake wa zamani, Hussein Shariff ‘Casillas’ na beki Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ waliokuwa Simba.
10-Mwadui FC
Ni timu ambayo imepanda daraja kwa kishindo na kurejea Ligi Kuu baada ya kutamba katika Ligi Daraja la Kwanza ilikoibuka bingwa wa jumla baada ya kuifunga Toto Africans bao 1-0 kwenye fainali iliyochezwa katika uwanja wa Azam Complex.
Mwadui inaonekana kuupania vilivyo msimu mpya wa Ligi Kuu 2015/16 kwani imefanya usajili kamambe wa kuimarisha kikosi chake kwa kuwasajili wachezaji, Maregesi Mwangwa, David Luhende, Anthony Matogolo, Razack Khalfan, Nizar Khalfan, Jabir Aziz ‘Stima’, Rashid Mandawa, Zahoro Pazi na Paul Nonga.
Zaidi ya hayo, timu hiyo inayonolewa na kocha mwenye maneno mengi na vituko, Jamhuri Kiwelo ‘Julio’ imepanga kwenda Afrika Kusini kuweka kambi ya muda mfupi kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu.
11-Ndanda FC
Maandalizi yao ni ya kusuasua na wachambuzi wengi wa masuala ya soka nchini wanaamini timu hiyo itakuwa miongoni mwa timu zitakazoteremka daraja msimu ujao.
Licha ya kufanya usajili wa nyota kama vile, Atupele Green (Kagera Sugar0 na Salvatory Ntebe (Ruvu Shooting), Ndanda inakabiliwa na ukata unaoaiathiri timu hiyo kiais cha kushindwa kuanza programu za mazoezi.
12-Prisons
Msimu uliopita, timu hiyo iliponea chupuchupu kushuka daraja jambo ambalo pengine uongozi, wanachama na mashabiki wake watakuwa hawapendi kuliona likitokea msimu ujao.
Hadi sasa, imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwashawishi wachezaji wake wengi tegemeo kubaki licha ya kuhitajika na timu kubwa nchini.
Kwa sasa, imejificha mkoani Mbeya ipo kwenye mipango ya kucheza mechi kadhaa za kirafiki ili kujiimarisha.
13-Simba
Kwa muda wa miaka minne sasa, wapenzi na mashabiki wa Simba wameshindwa kuiona timu yao ikishiriki mashindano ya kimataifa kutokana na kufanya vibaya kwenye Ligi Kuu nchini.
Katika kurudisha heshima yake ya zamani, Simba imebahatika kufanya usajili wa wachezaji mbalimbali wakiwamo, Peter Mwalyanzi, Mwinyi Kazimoto, Samih Nuhu, Mohamed Fakhi, Emiry Nibomana, Musa Hassan ‘Mgosi’ , Hamis Kiiza na wengineo.
Timu hiyo iliweka kambi mkoani Tanga, ikaelekea visiwani Zanzibar kwa kambi kabla ya kurejea jijini Dra es Salaam na kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Sports Club Villa ya Uganda. Bado inaendelea na maandalizi yake na uongozi wake umeahidi kuwa utaitafutia timu nzuri zaidi za kucheza nazo mechi za kirafiki kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu.
14-Stand United
Timu hiyo maarufu kama ‘Wapigadebe’ wa mjini Shinyanga, haikufanya vyema msimu uliopita na ilibakia kidogo ishuke daraja.
Kwa kulitambua hilo, timu hiyo sasa inaonekana kutotaka tena yaliyojitokeza nyuma kujirudia. Imempa mkataba kocha wa zamani wa Simba, Mfaransa Patrick Liewig, imefanikiwa kumbakiza kiungo wake, Haruna Chanongo na imefanya usajili wa baadhi ya wachezaji nyota, akiwamo Amri Kiemba aliyekuwa Simba.
Mbali na hilo imesaini mkataba mnono na Kampuni ya madini ya Acacia Mining wenye thamani ya Sh2.4 bilioni kwa miaka miwili, ambao unaifanya timu hiyo kuwa na udhamini ghali zaidi kuliko timu zote nchini.
15-Toto Africans
Wakali hao wa Mwanza au ‘Wanakishamapanda’ ambao msimu ujao wataonekana tena kwenye Ligi kuu baada ya miaka mitatu kupita , hawataki kuona wanarudi shimoni kama ilivyotokea miaka ya nyuma.
Wao walianza maandalizi ya msimu mpya mapema kwa mazoezi ya kuchuja wachezaji kwenye uwanja wa CCM Kirumba. Wamefanya usajili makini kwa kuwanasa Hamis Selemani, Abdallah Seseme, Edward Christopher, Abou Hashim na Deogratias Julius.
16- Yanga
Wahenga husema usione vyaelea vimeundwa. Usemi huu unaweza kuutumia kuonyesha ni kwa jinsi gani timu hiyo kongwe inavyojipanga kwa ajili ya kutetea ubingwa wake msimu ujao.
Kambi ya gharama kubwa kipindi ilipokuwa inajiandaa na mashindano ya Kombe la Kagame ilikoishia robo fainali na ile ya sasa hivi inapojiandaa na Ligi Kuu.
Usajili wa wachezaji wenye majina na vipaji vya soka kama vile, Godfrey Mwashiuya, Deus Kaseke, Malimi Busungu, Donald Ngoma, Thaban Kamusoko na Vivcent Bossou ni ushahidi wa dhamira hiyo.
Yanga na Azam ndizo timu zilizoanza mapema zaidi maandalizi ya Ligi Kuu na haitokuwa jambo la kushangaza kuiona ikitwaa taji kwa mara nyingine.