Mambo ya msingi ya kuzingatia katika upangaji bei za bidhaa
Muktasari:
Mjasiriamali anashauriwa wakati wa kupanga bei asifikirie kupata faida kubwa kwa mara moja kwenye bidhaa moja.
Mara nyingi wajasiriamali wamekuwa wakipata changamoto mbalimbali katika upangaji bei za bidhaa zao au huduma wanazozitoa. Matokeo yake wamekuwa wakipanga bei ambazo hazina uhalisia katika dunia yao ya kufanyia biashara.
Bei ambazo hazina uhalisia zinaweza kuwakimbiza wateja wa bidhaa au huduma husika, hivyo kuhatarisha maendeleo ya biashara husika. Katika makala haya tunazungumzia mambo ya msingi ya kuzingatia katika upanga bei za bidhaa na huduma mbalimbali.
Bei ni kiasi cha pesa ambacho mteja anatakiwa kulipa kwa ajili ya bidhaa au huduma anayohitaji. Bei hupangwa kwa ajili ya kuuza vitu halisi kama vile nguo na vitu ambavyo siyo halisi (huduma) kama vile afya.
Kuna baadhi ya wajasiriamali huonyesha bei zao moja kwa moja kwenye bidhaa zao. Mathalani, bidhaa zilizoko “supermarket” huwa zimeandikwa bei zake moja kwa moja. Vilevile wapo wajasiriamali ambao hawaonyeshi moja kwa moja bei ya bidhaa au huduma wanazozitoa. Wajasiriamali hawa hutaja bei ya kitu pale mteja anapokiulizia.
Hata hivyo, inashauriwa kuonyesha bei kwenye bidhaa husika ili kuepuka kuchanganya bei ya bidhaa moja na nyingine. Kuonyesha bei kwenye bidhaa au huduma inayotolewa husaidia pia kuonyesha uwazi na ukweli hivyo kujenga uaminifu kwa mteja juu ya kiasi anachotakiwa kulipa. Vilevile huweza kuzuia wafanyakazi ambao siyo waaminifu kutaja bei ambazo hazijapangwa kwa ajili ya bidhaa husika.
Upangaji wa bei hutegemea vitu vingi na hubadilika kulingana na wakati na mazingira. Kwa maana hiyo upangaji wa bei hauna budi kubadilika kulingana na hali halisi ya biashara.
Kigezo muhimu cha upangaji wa bei huamuliwa na gharama za uzalishaji wa bidhaa, mbinu za kimasoko ikiwa ni pamoja na gharama zinazohusiana na usambazaji, matangazo na mambo mengine.
Katika upangaji wa bei, mjasiriamali anatakiwa kujua aina ya bidhaa anayouza kama ni halisi (tangible) au huduma (service). Pia anatakiwa kuangalia mwenendo wa soko, idadi ya wauzaji wa bidhaa zinazofanana na za kwake, makundi ya watu watakaonunua bidhaa zake na wastani wa juu na chini wa kipato cha wateja watakaonunua bidhaa/ huduma zake.
Mjasiriamali anashauriwa wakati wa kupanga bei asifikirie kupata faida kubwa kwa mara moja kwenye bidhaa moja. Anashauriwa pia apange bei ambayo itamwezesha kuuza kwa haraka bidhaa yake na kuingiza bidhaa nyingine mpya kwa ajili ya kuuza. Hasara ya kutaka faida kubwa mara moja kwenye bidhaa moja ni kuwa anaweza kuwakimbiza wateja na hivyo kuua biashara yake.
Pale inapobidi, inafaa kuwa na utofauti wa bei za bidhaa za zamani na mpya hasa katika bidhaa halisi. Bidhaa ambazo zimekaa muda mrefu zinabidi kuuzwa kwa haraka kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwamo ya promosheni ambapo bei ya bidhaa husika itapunguzwa ili kuzuia kuharibika na hivyo kumpa mjasiriamali nafasi ya kuagiza bidhaa nyingine mpya za kuuza.
Mjasiriamali anaweza pia kufanya promosheni kwa kutoa punguzo la huduma anayouza katika muda fulani ili kujitangaza zaidi, kupata soko kubwa zaidi na kuvuta wateja. Hili linaweza kufanyika hata katika bidhaa za huduma kama vile intarnet, ushauri wa masuala ya biashara n.k.
Kwa jumla jambo la kuzingatia katika upangaji bei ni gharama za uzalishaji bidhaa au huduma husika, aina ya bidhaa au huduma na wateja unaohitaji.