Sekta ya ngozi yachechemea

Ng'ombe wakiwa malishoni
Muktasari:
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili unaonyesha kwamba juhudi hizo za kuamsha sekta ya ngozi nchini bado hazijafanikiwa. Kama kutakuwapo kwa mabadiliko ya mazingira ya biashara ya ngozi na bidhaa zake, taifa linaweza kusafirisha bidhaa nyingi nje na hivyo sekta hiyo kuchangia pato la taifa.
Pamoja na kuwapo kwa juhudi kubwa za Serikali za kuifanya sekta ya ngozi nchini kuongeza mchango wake katika pato la taifa, bado juhudi hizo hazijazaa matunda.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili unaonyesha kwamba juhudi hizo za kuamsha sekta ya ngozi nchini bado hazijafanikiwa. Kama kutakuwapo kwa mabadiliko ya mazingira ya biashara ya ngozi na bidhaa zake, taifa linaweza kusafirisha bidhaa nyingi nje na hivyo sekta hiyo kuchangia pato la taifa.
Ng’ombe milioni 21.3
Mbali na hayo ingawa Tanzania ina ng’ombe milioni 21.3, mbuzi milioni 15 na kondoo milioni 6.4, sekta ya ngozi iko shaghala baghala.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kwamba hadi kufikia Julai mwaka jana asilimia 30 za ngozi zilizozalishwa Tanzania, zilifika katika sokola ndani, huku kiasi kikubwa cha ngozi hizo zikipelekwa nje bila kusindikwa.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Serikali kuhusu ngozi zinaonesha kwamba kuna ngozi za ng’ombe milioni 3.8 za mbuzi milioni 2.4 wakati za kondoo ni milioni 2.2.
Ukusanyaji wa ngozi nchini, imeelezwa kuwa chini ya wastani wa asilimia 50 ya wanyama wanaochinjwa, ikimaananisha kwamba kuna ngozi za ng’ombe milioni 2.4, ngozi za mbuzi 900,000, na ngozi za kondoo 400,000.
Utafiti unaonyesha kwamba hali imekuwa mbaya zaidi tangu Serikali ilipopandisha kodi ya usafirishaji wa ngozi ghafi nje kutoka asilimia 40 hadi 90 ili kuongeza thamani, kwenye bajeti yake ya mwaka 2012/2013.
Akiwasilisha bajeti ya 2012/2013 mjini Dodoma mwaka jana, Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa aliliambia Bunge kwamba Serikali imeamua kupandisha kodi ili kuzuia usafirishaji wa bidhaa za wanyama nje.
Alisema ni lengo la Sserikali kuhakikisha kwamba inatengeneza mazingirana viwanda vya kusindika ngozi nchini vinapata mali ghafi ya kutosha kwa ajili ya kuendesha shughuli hiyo na kuongeza thamani ya bidhaa za wanyama zinazosafirishwa nje.
Tangu kuongezwa kwa kodi hiyo mwaka jana, imeelezwa kuwa matukio ya usafirishaji ngozi nje ya nchi kimagendo yameongezeka kutokana na bei kubwa inayotolewa na wanunuzi wa ngozi wa nchi jirani. Hali hiyo imefanya viwanda vya ngozi nchini kuwa na uhaba wa mali ghafi.
Utafiti uliofanywa na wizara baada ya kupandisha kodi umeonyesha kuwapo kwa tatizo hilo.
Ofisa kutoka Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Emmanuel Muyinga akizungumzia zaidi matokeo ya utafiti huo, anasema baada ya mabadiliko ya kodi katika viwanda vya nyumbani vilikuwa vinapata ngozi ya daraja la chini sana. Awali viwanda vilikuwa vikipata ngozi ya daraja la juu.
Mbali na hayo yakwimu zinaonyesha kwamba kuna utoroshaji mkubwa wa ngozi kwenda nchi jirani na kuisababishia hasara serikali ya Sh1 bilioni kwa mwaka. Inaelezwa kwamba ngozi 50,000 hutoroshwa kwenda nchi jirani na kuisababishia serikali kupata hasara ya Sh427 milioni kwa kukosa kodi yake.
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Joyce Mapunjo amekiri kwamba serikali inapoteza mamilioni ya fedha kutoka kwa wafanyabiashara ambao siyo waaminifu. Wafanyabiashara hao wanatoa takwimu za usafirishaji bidhaa nje zisizokuwa kweli.
“Wafanyabiashara hao hutoa takwimu zenye bei ndogo ya bidhaa na kiasi kidogo cha mauzo waliosafirisha kwa lengo la kukwepa kulipa kodi stahiki kwa serikali,” anasema bila kutaja takwimu halisi.
Anasema Serikali imekuwa ikiwasaidia wafanyabiashara wa ngozi nchini na kwamba hata ongezeko la kodi kutoka asilimia 40 hadi 90 kwa wale wanaotaka kusafirisha ngozi ghafi nje lilifanywa kwa kusudio la kulinda viwanda vya ndani na kuongezea thamani ngozi zinazozalishwa nchini.
Mapunjo anasema maamuzi hayo yalilenga kufanya viwanda vya ndani kushamiri zaidi pia kuwezesha uanzishaji wa viwanda vingine vinavyotegemea ngozi.
Pamoja na nia njema hiyo ya Serikali, viwanda vingi vya ngozi nchini huenda vikafungwa kutokana na kukosekana kwa ngozi. Viwanda hivyo ni pamoja na Moshi Leather Industries, Tanzania Leather Industries, Afro Leather, Kibaha Tannery, Himo Tanners na Salex Tanners – yenye uwezo wa kusindikia futi 40 za mraba za ngozi. Viwanda hivyo hivi sasa vinafanya kazi chini ya asilimia 30.
Mkurugenzi wa Ushawishi na Sera wa Shirikisho la wenye viwanda nchini (CTI), Hussein Kamote, akizungumzia sekta ya ngozi amesema inaweza kuwa
mkombozi mkubwa wa ajira kwa vijana, ingawa hivi sasa inasuasua.
“Ni bahati mbaya kwamba Tanzania imeshindwa kutumia sekta hii, ambayo kama ikiratibiwa vyema kungekuwapo kwa nafasi mpya za ajira kila kukicha” anasema Kamote.
Mwenyekiti wa Shirikisho la wenye Viwanda vya Ngozi, Onorato Garavagli anasema hali ya upatikanaji wa ngozi nchini ni mbaya kwa sasa kuliko wakati ule kodi ya kusafirisha ngozi nje ilikuwa ndogo.
“Hali ya kufanyabiashara kwa sasa si kama ile ya zamani. Viwanda vingi vya ngozi nchini vinapita katika kipindi kigumu huku vikiwa havina mali ghafi ya kufanyia kazi, hivi karibuni vitafungwa kutokana na kukosa mali ghafi,” anasema Kamote.
Sekta ya ngozi Tanzania
Mkurugenzi wa maendeleo ya Viwanda, Wizara ya Kuinua sekta ya ngozi Viwanda na Biashara, Eline Sikazwe ameliambia gazeti hili kwamba ipo mipango ya kutekeleza ili kunyanyua sekta ya ngozi Tanzania.
“Taifa limekuwa likipoteza mamilioni ya fedha kutokana na kusafirisha ngozi ghafi, muda umefika kubadili sekta hii na kuleta faida inayotakiwa kwa taifa na kwa wafanyabiashara wenyewe,” anasema Sikazwe.
Uwekezaji hafifu katika sekta ya ngoz kumeinyima nchi takribani asilimia 90 ya ngozi zinazosafirishwa nje ya nchi zikiwa bado ghafi.
Unaweza kuzungumza nasi kwa kutuma ujumbe mfupi wa simu (SMS) kwenda 15774 ukianza na neno BIZ na kisha unaandika ujumbe wako: SMS ni bure!!