Heche amng’ata, ampuliza Dk Bashiru

Muktasari:

  • Mbunge wa zamani wa Tarime Vijijini mkoani Mara, John Heche adai mabadiliko duniani hayaletwi na watawala bali yanaletwa na vijana na watu wenye umasikini wanaopigania maisha na maendeleo katika Taifa.

Dar es Salaam. Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, John Heche amedai mabadiliko duniani hayaletwi na watawala bali yanaletwa na vijana na watu wenye umasikini wanaopigania maisha na maendeleo katika Taifa.

Amedai watawala wapo katika hali kuridhika na hawawezi kuuletea mabadiliko, kwa sababu wao hawana cha kupoteza.

Amesisitiza mabadiliko duniani yanaletwa na vijana na sio matajiri.

“Ukitaka kujua unafiki wa watu wenye mali, huwezi kuwakuta wapo Chadema hata mmoja, hivi ni bahati mbaya wote hawatuelewi? Au sera zetu hazieleweki wala kazi tunazozifanya ni kweli?

“Sio kweli kwa sababu huko waliko wapo salama kwa nini wakuunge mkono wewe mtu masikini? Ni wajibu wewe mtu masikini kukataa hali hii,” amesema Heche ambaye ni mbunge wa zamani wa Tarime Vijijini.

Ametoa kauli hiyo leo Jumanne Novemba 22, 2022 wakati akizungumza na viongozi na wanachama wa Chadema kanda ya Pwani, katika mkutano wa ndani uliofanyika wilayani Kibaha mkoani Pwani.

Heche ambaye ni mwenyekiti wa zamani wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), amesema Chadema kushika dola ili kubadilisha mfumo wa kupendeleana.

Amesema Chadema ikiwa madarakani kila mwenye uwezo atapata kazi Serikali bila kujali yupo wapi CCM au upinzani.

Mbali na hilo, Heche kuanzia mwezi ujao pasipo kueleweka Chadema itaanza mikutano ya hadhara kwa lazima katika maeneo mbalimbali ili kuimarisha chama hicho.

Katika mkutano huo, Heche alizungumzia sakata la aliyekuwa katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally akisema kuna wanaCCM wanamshambulia kwa kusema ukweli uliomgusa mtu fulani.

Hata hivyo, yeye hamuungi mkono Dk Bashiru kwa sababu ni miongoni mwa viongozi waliosababisha mambo kuwa magumu.

Wiki iliyopita, Dk Bashiru ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu Kiongozi, akihutubia mkutano wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (Mviwata) mkoani Morogoro, alisema mtandao huo si chombo cha kutoa shukrani kwa yeyote yule, bali ni chombo cha kudai haki na heshima.

Kauli hiyo iliwabua Wanaccm wakiwemo viongozi na wabunge wakimtaka ajitathimini na kuomba radhi kwa kauli yake huku wengine wakienda mbali zaidi wakimtaka ajiuzulu ubunge.

Lakini Heche amesema, “sisemi kama Bashiru ni mtu mwema, lakini hoja alioizungumza ina ukweli na inapaswa kuungwa mkono bila kujali ameisema nani. Hata kama hatumpendi Dk Bashiru kwa vitendo vyake, lakini hoja alioizungumza inapaswa kujibiwa na Serikali.

Hata hivyo, Heche amesema, “Dk Bashiru ametekeleza wajibu wake kama mbunge, lakini kuna watu fulani… wanamshambulia bosi wao wa zamani kwa hoja ya ukweli.”

“Bashiru anapaswa kujibu maswali kwa sababu alikuwa kiongozi CCM na Serikali kwa nini hakuyafanya haya ambayo wakulima wanayoyapaswa kufanyiwa.”