Rushwa uchaguzi wa CCM

Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo chaguzi za CCM zinazoendelea. Picha na Merciful Munuo

Dar/mikoani. Wakati CCM ikifuta na kuahirisha uchaguzi wa ndani katika baadhi ya maeneo kwa tuhuma za rushwa, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imeonya ikisema itawashughulikia wahusika bila kujali jina au ukubwa wa mtu.

Onyo hilo la Takukuru limelotolewa na mkurugenzi wake mkuu, Kamishna wa Polisi Salum Hamduni saa chache baada ya CCM kutangaza kufuta matokeo ya uchaguzi wa Umoja wa Vijana (UVCCM) Mkoa wa Simiyu na kusimamisha uchaguzi wa wajumbe wa halmashauri kuu mikoa ya Arusha na Mbeya kwa tuhuma za rushwa.

Jana, Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma alisema uamuzi wa kufuta matokeo unaweza kuendelea katika maeneo yatakayobainika kukiuka sheria na kanuni za uchaguzi.

Chongolo aliweka bayana kuwa sababu kuu ya kufutwa ni vitendo vya rushwa ambavyo vimetajwa katika maeneo hayo na kuwa chama hakitavivumilia.

“Mbali na hilo, tunachunguza kuhusu uchaguzi wa CCM Mkoa wa Mjini Magharibi katika tuhuma za kada mmoja kubeba boksi la kura kwenda nalo chumba cha kuhesabia kura, ikibainika tutatoa maelekezo ama ya kufuta matokeo au kuruhusu aliyetangazwa aendelee,” alisema Chongolo.

Mwanasiasa huyo ambaye ni mkurugenzi wa uchaguzi wa ndani ya chama hicho, alisema CCM haiko tayari kuona viongozi wanaingia madarakani kwa rushwa wala vitendo viovu.

Kuhusu adhabu zitakazotolewa, alisema ni kuondolewa kwenye mchakato wa uchaguzi na kupelekwa katika vyombo husika.

Katika maeneo ambayo Chongolo aliyataja, gazeti hili lilizungumza na baadhi ya wajumbe na makada wa chama hicho, ambao walikiri vitendo vya rushwa kukithiri.

Moja matukio ambayo yamevuta mijadala katika mitandao ya kijamii ni kipande cha video kilichorushwa kikiwaonyesha makada wa UVCCM wakilizunguka gari dogo wilayani Itilima, Mkoa wa Simiyu, ambako inadaiwa walikuwa wanachukua mlungula.

Si Chongolo wala Katibu wa Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka aliyezungumzia video hilo.

Shaka alipoulizwa kuhusu video hiyo hakujibu chochote juzi hadi lilipotolewa tamko la kufuta uchaguzi katika maeneo hayo.

Chongolo alitoa taarifa hiyo wakati mikoa mbalimbali ya kichama ikiendelea kushuhudia wagombea uenyekiti, ujumbe wa NEC na mkutano mkuu wakichuana kwa kueleza sera na mikakati yao kwa wanachama.

Baadhi ya wenyeviti waliokuwa wakitetea nafasi zao waliangushwa sawia na wajumbe wa NEC huku sura mpya zikizidi kuchagua.


Kauli ya Takukuru

Mara baada ya Chongolo kuzungumza na wanahabari, gazeti hili lilimtafuta Kamishna Hamduni kujua mkakati wa taasisi hiyo kuhusu hali hiyo, naye akasema “tayari kuna chunguzi tunaendelea nazo, wao kama chama wametumia taratibu zao na sisi tunaendelea na taratibu zetu kwa mujibu wa sheria.”

Alipoulizwa kuhusu video inayowaonyesha wajumbe wanaodhaniwa kuchukua mlungula kwenye gari dogo, Hamduni alisema, “hiyo ya Itilima, Simiyu, hiyo taarifa tunayo na ofisi yangu ya Simiyu inaendelea na utaratibu.”


Diwani ashikiliwa

Katika hatua nyingine, Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Mbeya, Maghela Ndimbo alisema wanamshikiria diwani mmoja kwa tuhuma za rushwa kuelekea uchaguzi wa CCM uliokuwa ufanyike jana, ambao umesitishwa.

Alisema diwani huyo (hakumtaja jina) alipewa fedha na mmoja wa wagombea ambaye hakumtaja pia, ili akawagawie madiwani wengine 12 ili wamsaidie kupiga kampeni.

“Kweli jambo hilo lipo na hatua zilichukuliwa na kuwasilisha kwenye mamlaka husika, ndio maana umeona uchaguzi umesitishwa, lakini kusema nani anahusika kwa kweli kwa sasa siwezi kulisema, lakini ushahidi tunao wa picha na video, ndiyo maana tuliripoti,” alisema

Ndimbo alisema, “fedha zilizokuwa zikitolewa zilikuwa zikagawiwe kwa wajumbe, hivyo huyo diwani yeye ni kama wakala tu, tumefanya hatua ya kwanza ya kuzuia, kwa sababu ilitokea purukushani na mtuhumiwa kukimbilia chumbani, hivyo wewe jua ushahidi wa kupeana na kupokea upo.”

Pia kinachoelezwa ni kuwa baadhi ya wajumbe walikuwa wamepokea fedha kwa ajili ya kwenda kupiga kura na baadhi ya wajumbe walipokea kutoka kwa mgombea zaidi ya mmoja, jambo ambalo lilianza kushtukiwa mapema.

Waliokuwa wakigombea NEC Mkoa wa Mbeya alikuwa, Ndele Mwanselela, Saul Mwaisenye na Christopher Uwagile.

Hata hivyo hakuna mgombea aliyekuwa tayari kuzungumzia sakata hilo wakisema lipo katika ngazi za juu ambako wanaweza kulitolea ufafanuzi.

Alex Kinyamagoha, Diwani wa Itewe, Chunya alisema hapingi yaliyofanyika kwa kuwa japo na yana gharama unaporudiwa uchaguzi.


Ni aibu

Msimamizi wa uchaguzi Mkoa wa Simiyu ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila alisema kilichotokea mkoani humo ni aibu kwa chama ngazi ya mkoa.

Mshindi wa nafasi ya uenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Simiyu, William Shilingi ambaye hata hivyo hakuwepo ukumbini wakati tangazo la kufutwa uchaguzi wake linatolewa, alikuwa mmoja kati ya wajumbe watatu waliowakilisha jumuiya hiyo kwenye mkutano mkuu huo wa uchaguzi mkoa.

Tangazo la kuwataka wajumbe wa mkutano mkuu wa mkoa kupitia UVCCM kuondoka ukumbini kutokana na matokeo ya uchaguzi uliowapa fursa hiyo kufutwa, lilitolewa na Katibu wa CCM Mkoa wa Simiyu, Mohammed Ally Khalifani.

Wajumbe wengine waliotokana na UVCCM walioondolewa ukumbini ni Mjumbe wa Baraza Kuu la Taifa na mjumbe wa mkutano mkuu wa mkoa waliokuwa wameshinda nafasi hizo kupitia uchaguzi ambao matokeo yake yamefutwa na chama.

Chalamila aliwasihi wana CCM kuacha tabia ya kuzungumza rushwa kwa unafiki huku kwa kificho wanawabeba na kuchagua watoa rushwa.

Awali, Khalfani aliwaeleza wajumbe kuwa ndani ya siku mbili zilizopita, video inayoonyesha viashiria vya vitendo vya rushwa ilisambaa kupitia mitandao ya kijamii ikionyesha watu waliodaiwa kuwa za wajumbe wa mkutano wa uchaguzi wa UVCCM mkoani humo.


Hofu Arusha

Wakati Kamanda wa Takukuru, Mkoa wa Arusha, Zawadi Ngairo akisema wamepata taarifa za tuhuma za rushwa na wanaendelea na uchunguzi, hofu imeibuka miongoni mwa wagombea wa halmashauri kuu.

“Tunawaonya wagombea na wapiga kura waache kujihusisha na rushwa kwani, wajue Takukuru tupo na tangu kuanza mchakato wa chaguzi tumekuwa tukifuatilia lakini pia muhimu kutumia vizuri haki ya kugombea na kupiga kura,” alisema.


Imeandikwa na Habel Chidawali (Dodoma), Yohana Challe (Mbeya), Samirah Yusuph (Simiyu) na Mussa Juma (Arusha).