Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

‘Vyama vya siasa viongeze nafasi za wanawake’

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Wanasiasa(Ulingo) Anna Abdallah akifungua  mkutano wa wanawake viongozi uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Muktasari:

  • Siku moja baada ya Serikali kutoa wito kwa wadau wa demokrasia kujitokeza mbele ya Kamati ya Bunge kupeleka maoni, Umoja wa Wanawake Wanasiasa (Ulingo) umekutana kujadili miswada ya sheria ya vyama vya siasa ili kuchakata maoni yao watakayoyapeleka bungeni

Dar es Salaam. Wanawake wanaounda Umoja wa Wanawake Wanasiasa (Ulingo), wamependekeza vyama vya siasa kuweka utaratibu wa asilimia fulani ya nafasi zitakazowezesha wanawake kuingia kwenye nafasi za uongozi.

Wamesema hayo jana jijini hapa kujadili miswada ya Sheria za Vyama vya Siasa, ikiwa ni siku moja tangu Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko kutoa wito kwa wadau wa demokrasia ya vyama vingi kutoa maoni.

Dk Biteko alitoa wito huo Januari 4, 2024 wakati akifunga mkutano maalumu wa siku mbili wa Baraza la Vyama vya Siasa, uliojadili miswada ya Sheria ya Uchaguzi na Sheria ya Vyama vya Siasa iliyosomwa kwa kwanza bungeni Novemba 10 2023.

Akizungumza na wanahabari katika mkutano wa viongozi wanawake wa vyama vya siasa 19 vyenye usajili wa kudumu, makamu mwenyekiti wa Ulingo, Zanzibar, Mgeni Hassan Juma amesema wanapendekeza muswada wa sheria ya vyama siasa utambue na kuwawezesha wanawake kuingia katika uongozi kuanzia ngazi za vijiji hadi Taifa.

"Kwa mfano katika kijiji basi tupate angalau asilimia fulani, mara nyingi kundi hili linaongea nafasi nyingi lakini uwezekano wa kupata ni mdogo, sasa kama hatujaweka mikakati ndani ya vyama vyetu basi changamoto itaendelea kuwepo.

"Tunazungumzia 50/50 ndiyo maana tunavitaka vyama vyetu vitupe nafasi wanawake kushiriki katika chaguzi za majimbo," amesema Mgeni ambaye pia ni Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Mgeni amesema lengo la kikao hicho ni kuzungumza na kujadiliana kama viongozi wa wanawake wa vyama vya siasa kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu sheria za vyama vya siasa na sheria ya uchaguzi.

"Jana (Alhamisi) katika mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa, vyama vingi vilikuja na msimamo wao, leo Ijumaa tumekutana ili kutafakari kuona kipi cha kukipeleka mbele ya kamati ya Bunge ili kuyapa umuhimu na kuyaingiza katika muswada," amesema

Mwenyekiti wa Ulingo, Anna Abdallah amesema kila chama cha siasa kina jumuiya za wanawake, hivyo taasisi hiyo inawakusanya viongozi hao na kuwaweka pamoja ili kujadili masuala ya siasa yanayohusu maendeleo ya wanawake katika Taifa hili.

"Tunataka kwenda na nguvu ya wanawake kutoka vyama 19, ni nguvu kubwa yale yaliyozungumza jana ( juzi) katika mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa kuhusu wanawake tutakubaliana na kuyaweka vizuri kisha tutayapeleka mbele ya kamati kama maoni ya wanawake wa Tanzania wanavyosema kuhusu uwakilishi ndani ya vyama.

Anna ambaye amewahi kuwa mbunge miaka iliyopita amesema mkutano huo utajikita kujadili Sheria ya Vyama vya Siasa, akisema demokrasia lazima ianzie ndani ya vyama hivyo.

Pia, amewataka Watanzania kufanya uamuzi sahihi kwa baadhi ya wabunge wanaume na wanawake wa viti maalumu ambao hawatekelezi wajibu ipasavyo ifikapo mwaka 2025.

"Hawa hawastaili kupewa tena nafasi imetosha, wale ambao hawatekelezi na wananchi wanaona huyu mbunge hajui shida zao, sasa uchaguzi si unakuja wanayo nafasi ya kuwaondoa," amesema

Makamu Mwenyekiti wa Ulingo, Bara Suzan Lyimo amesema kubwa wanaloliangalia ni usawa wa kijinsia kwa sababu wanawake ndiyo ajenda na turufu ya ushindi.

"Pamoja tunatoka vyama vya siasa tofauti, lakini linapokuja suala la wanawake wote tunakuwa kitu kimoja, tunatamani wale makamishna wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), suala la jinsia walizingatie," amesema Lyimo.