ADC kupata viongozi wapya leo
Muktasari:
- Uchaguzi huo unalenga kuwapata viongozi wapya watakaokiongoza chama hicho kwa kipindi cha miaka mitano kwa mujibu wa katiba yao, huku wagombea wawili wakitarajia kuchuana katika kinyang'anyiro hicho.
Dar es Salaam. Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Mohamed Ali Ahmed akimekipongeza Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), kwa kuweka utaratibu wa ukomo wa uongozi licha ya uchanga wake.
Amesema chama hicho ni kichanga lakini kimezidi kukua, huku kikiwa na wanasiasa wakongwe na wabobezi.
Ahmed ametoa pongezi hizo leo Juni 29, 2024 wakati akifungua mkutano wa uchaguzi wa chama hicho, unaotarajia kuwezesha upatikanai wa viongozi wapya watakaokiongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
"Niwapongeze ADC ni chama kimojawapo kati ya vyama vichanga, lakini kimeweka utaratibu mzuri wa kupokezana vijiti,"amesema Ahmed.
Amebainisha kuwa vipo baadhi ya vyama vya siasa (bila kuvitaja) ukiviangalia, unaona viongozi wake hawataki kutoka na wengine wakijaribu kuingia.
Mbali na pongezi hizo, msajili huyo amewaasa viongozi watakaochaguliwa pamoja na wapiga kura kuweka maslahi ya chama hicho mbele.
"Pamoja na mambo mengine mnaenda kwenye uchaguzi, kwenye uchaguzi huwa kuna mambo mengi ikiwemo fitna, majungu, rushwa na mambo mengine. Tukubaliane mkaweke imani atakayeshinda wengine msubiri muda ufike "amesema.
Uchaguzi huo wa nne wa ADC unafanyika ambapo baadhi ya viongozi wamemaliza muda wao wa wa kipindi cha miaka kumi, kwa mujibu wa katiba akiwemo mwenyekiti Hamad Rashid Mohamed.
Akizungumza kwenye mkutano huo mwenyekiti huyo anayemaliza muda wake, amewataka viongozi watakaochaguliwa kutokubali kuuza utu wao, kwa kuwa watakibomoa chama endapo wataingia kwenye rushwa.
Amesema siku zote siasa ni ibilisi ndio maana huanza kwa kumtanguliza Mwenyezi Mungu, ndio maana katika chaguzi zao zote hufanyika bila tatizo la Russia.
"Msije mkamweka ibilisi mbele, simamieni misingi ya haki katika kujenga taasisi na kuanzisha vitengo vitakavyosimamia mambo mbalimbali,"amesema Hamad.
Awali aliyekuwa Mwenyekiti wa kwanza wa ADC Said Miraj Abdallah, amesema sifa ya kiongzi mzuri ni yule anayefikiri kwa ajili ya anaowaongoza kwa kutumia akili kwa maslahi ya taasisi badala ya kikundi cha watu au maslahi ya watu.
Utaratibu wa uchaguzi
Katibu wa kamati ya uchaguzi, Innocent Siriwa akizungumzia mchakato huo amesema wapiga kura ni 197 kutoka Bara na Zanzibar, ambapo wataanza kwa kumchagua mwenyekiti nafasi inayowaniwa na Shabani Haji Itutu aliyekuwa makamu mwenyekiti na Doyo Hassan Doyo aliyekuwa kuwa katibu mkuu. Mshindi atakabidhiwa madaraka na mwenyekiti anayemaliza muda wake.
"Atakapokabidhiwa, mwenyekiti mpya ndiye ataendelea na mchakato wa kuwapata makamu mwenyekiti wa Bara na Zanzibar," amesema Siriwa.
Wanaowania nafasi hiyo upande wa Bara ni Scola Kahana na Hassan Mvungi na Zanzibar ni Fatma Salehe na Shara Amrani huku pia kukifanyika uchaguzi wa nafasi 19 za wajumbe wa bodi ya uongozi taifa.