CCM Kongowe yapata mfadhili kujenga ofisi

Mjumbe wa Halmashauri kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Pwani, Alhaji Musa Mansour akikabidhi Sh6,000,000 milioni kwa ajili ya ununuzi wa eneo la kiwanja cha ujenzi wa ofisi ya chama hicho Kata ya Kongowe. Picha Juliet Ngarabali
Muktasari:
- Jumuiya tatu za CCM mjini Kibaha zilizokua zikibanana kwenye chumba kimoja cha ofisi, sasa zitaondokana na adha hiyo baada ya mfadhili kujitokeza kuzijengea ofisi,
Kibaha. Jumuiya tatu za CCM katika kata ya Kongowe mjini Kibaha zimepatiwa fedha pamoja na vifaa vya kujenga ofisi ili kuondokana na adha ya kutumia chumba kimoja kiasi cha kushindwa kutekeleza shughuli zao kwa ufanisi.
Jumuiya hizo ni pamoja na Umoja wa Vijana (UVCCM), Umoja wa Wanawake (UWT) na Wazazi, ambapo kwa zaidi ya miaka 10 zimekuwa zikitumia chumba kimoja.
Hayo yameelezwa jana Agosti 4 na Katibu wa CCM Kata ya Kongowe, Mwalimu Said kwenye kikao maalumu cha Halmashauri kuu ya Kata hiyo kilichoketi kwa ajili ya kupokea msaada wa Sh6 milioni, tofali 2, 000, mifuko 100 ya saruji na lori mbili za mchanga kutoka kwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho mkoani Pwani, Alhaji Musa Mansour kwa ajili ya ununuzi wa eneo la kiwanja na ujenzi wa Ofisi.
“Tunamshukuru Alhaji Musa Mansour kwa kweli ametusitiri sisi Jumuia tatu tulikua tukifanya kazi kwa shida pasipo kuwepo hata usiri wakati mwingine maana tunatumia chumba kimoja kwenye jengo la Ofisi ya Tawi kwa hiyo ujezi wa ofisi yetu utaenda kutatua changamoto na kuleta ufanisi,” amesema Said.
Awali akikabidhi misaada hiyo, Mansour amesema wao kama wanachana wanawajibu wa kutambua wana kazi kubwa mbele yao ya kukiinarisha chama na jamboe hilo sio kazi ndogo inahitaji mshikamano wa hali ya juu na kujitoa zaidi.
"Kama tukishikamana tutafikia kata zote zenye shida ya ofisi na nina amini tutajenga, tutaitisha harambe ya pamoja na tukiwa na nia na dhamira ya dhati naamini tutaweza kujenga chama.
"Hiki chama unapoomba ridhaa ya wananchi na wanachama maana yake lazima ukubali kutumika pande zote na chama hakiwezi kuwa kikubwa kama hakina wanachama ndio maana lazima tuimarishe ofisi zetu," amesema Alhaji Mansour.
Naye Mwenyekiti wa CCM kata hiyo, Simon Mbelwa amemshukuru Mansour kwa kuguswa na changamoto ya kutokuwepo kwa ofisi na kwamba wanachama watahakikisha wanasimamia ujenzi huo ili ukamilike kwa wakati ili shughuli za chama ziendelee kwa weledi.