Wadau wagawanyika CCM kurudisha kofia mbili

Wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM wakiimba na kushangila walipokuwa wakiendelea kushiriki mkutano mkuu wa 10 wa chama hicho, jijini Dodoma.
Picha na Edwin Mjwahuzi
Muktasari:
Siku moja baada ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kupitisha marekebisho ya katiba ambayo imerudisha mfumo wa kofia mbili, wadau na wanasiasa wametofautiana wakitaka liangaliwe upya.
Dodoma. Siku moja baada ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kupitisha marekebisho ya katiba ambayo imerudisha mfumo wa kofia mbili, wadau na wanasiasa wametofautiana wakitaka liangaliwe upya.
Katika mkutano wake juzi CCM kilipitisha marekebisho hayo ambayo yanaruhusu mtu yeyote kugombea nafasi ya uongozi wa chama hata kama ana madaraka mengine yaliyotokana na chama.
Utaratibu wa kofia mbili za uongozi ulikuwapo ndani ya CCM, lakini uliondolewa wakati wa utawala wa Rais wa awamu ya tano, John Magufuli.
Kufuatia hatua hiyo, baadhi ya watu wameonyesha shaka kuhusu chama kuisimamia Serikali kwa madai haiwezekani kwani ni hao hao hivyo kesi zao itakuwa ni sawa na majadiliano.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza jana katika mkutano mkuu alisema, uwepo wa mawaziri ndani ya halmashauri kuu utawezesha kupatikana majibu ya haraka.
Rais alisema kwa kipindi kirefu hakukuwa na fursa ya kujadili taarifa za utekelezaji wa Ilani.
“Kama kuna majibu ya ufafanuzi, kwa bahati nzuri, jana (juzi) mawaziri wengi mliwapitisha hapa kuwa wajumbe wa NEC, wapo humo ndani, kukiwa na changamoto watazungumza.”alisema Rais Samia na kuongeza;
“Kama kuna jambo linahitaji ufafanuzi litatolewa, hii ndio chama kushika hatamu kwa Serikali yake, kutaka majibu ya Serikali hapa na ndio yale mageuzi niliyoyaleta kwamba Serikali na chama ziko pamoja,” alisema.
Baadhi ya mawaziri waliopenya katika uchaguzi huo na wizara zao kwenye mabano ni Angela Kairuki (Tamisemi), Dk Ashatu Kijaji (uwekezaji, viwanda na biashara), Angelina Mabula (Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi), January Makamba (Nishati) na Hussein Bashe wa Kilimo.
Wengine ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Innocent Bashungwa, Profesa Makame Mbarawa (Ujenzi na Uchukuzi), Dk Mwigulu Nchemba (fedha na mipango) na Waziri wa Fedha wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk Saada Mkuya.
Mitazamo
Aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela alisema suala la kuwa na kofia mbili halina mashiko kwani kushika madaraka sehemu hizo hakumpotezei mtu uwezo wa kutenda jambo ilimradi iwe ni ndani ya CCM.
Alisema uwepo wa mawaziri ndani ya Halmashauri Kuu ya CCM, kunakwenda kuimarisha na kukisaidia chama kupata majibu ya haraka kwa kadri inavyotakiwa badala ya kusubiri kwa wakati mwingine.
Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima alisema jambo hilo halina ukakasi hata kidogo kwani chama ni kile kile na Serikali ni hiyohiyo.
Askofu Gwajima ambaye pia ni Mbunge wa Kawe alisema mawaziri watatimiza wajibu wao kwa nafasi walizoteuliwa na kusimia chama kwa nafasi walizochaguliwa kwa hiyo hakuna mwingiliano wala mgongano wa kimaslahi.
Kada wa CCM, Mariam Selasi Haji alipinga mfumo wa kofia mbili akisema unakwenda kuwaumiza kwa sababu utawafanya wengine kufanya kazi kwa mazoea bila kuwa na watu wa kuwashurutisha. “Lakini, kwa sasa wameshachaguliwa acha waende kama ilivyo, ila mbele hukotunahitaji kulitazama jambo hili, mtu awe huyo huyo kwenye chama na kisha serikalini hivi anaweza kuitwa kweli akahojiwa jambo?” alihoji Mariam ambaye alikuwa miongoni mwa wagombea nafasi za NEC kundi la wanawake.