Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

CCM yaitisha mkutano mkuu maalumu, sababu yatajwa

Muktasari:

  • Baada ya miezi mitatu, Chama cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza kufanya mkutano mkuu mwingine maalumu, ukihusisha marekebisho ya katiba yake.

Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM), kimetangaza kufanya mkutano mkuu maalumu Mei 29 na 30 mwaka huu, ukiwa ni wa pili kufanyika kwa kipindi cha miezi mitatu, pamoja na mambo mengine ukilenga kupitisha ilani ya uchaguzi.

Awali, chama hicho kilifanya mkutano mkuu maalumu Januari 18-19, 2025 uliohusisha kuwateua Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wa urais na Dk Emmanuel Nchimbi, katibu mkuu wa chama hicho, kuwa mgombea mwenza wake katika Uchaguzi Mkuu baadaye mwaka huu. Pia Dk Hussein Ali Mwinyi aliteuliwa kugombea urais Zanzibar.

Taarifa ya mkutano huo, imetolewa jijini Dar es Salaam leo, Jumamosi Mei 17, 2025 na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla katika mkutano wake na waandishi wa habari.

Amesema mkutano huo, utatanguliwa na kikao cha Halmashauri Kuu Mei 28, baada ya Kamati Kuu Mei 26, vyote vitafanyika jijini Dodoma.

"Kubwa katika mkutano huu ni hiyo kupokea na kuzindua ilani ya CCM. Huu ni mwaka wa uchaguzi kwa hiyo, lazima tupokee taarifa ya utekelezaji wa ilani kwa miaka mitano na baada ya hapo maana yake sasa, tunakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuona tumefanya nini," amesema.

Ajenda nyingine, amesema ni kufanya marekebisho madogo katika Katiba ya CCM.

Amesema tayari maandalizi yameshafanyika kwa kiasi kikubwa na kwamba wajumbe wote wanaalikwa kuhudhuria, kadhalika wote watakaopata mwaliko wahakikishe wanakwenda.

Hadi wanaandaa Ilani, amesema wamefanya tathmini ya kutosha ya utekelezaji na changamoto chache zilizobaki wanaziingiza katika Ilani ijayo.

Katika uzinduzi huo, amesema jamii itaona kwamba CCM inazingatia maoni ya wananchi kwa kuwa katika maandalizi yake wadau mbalimbali wameshirikishwa.

"Tunafurahi mwaka huu tumekuwa na mikusanyiko mikubwa huu wa tatu, tumekuwa na mkutano mkuu, tumekuwa na sherehe miaka 48 na huu unaenda kuwa wa tatu," amesema.

Akifafanua kuhusu marekebisho ya Katiba, Makalla amesema yanafanywa kwa maslahi ya CCM na kwamba chama hicho aghalabu kimekuwa kikijihuisha kuendana na wakati na mahitaji.

Makalla amesema mkutako Mkuu aghalabu ni jambo kubwa na hadi anatangaza kulikuwa na maandalizi yaliyokuwa yanafanyika.

Dk Nchimbi atapata mrithi

Alipoulizwa iwapo katika mkutako huo, atateuliwa Katibu Mkuu mpya wa CCM, kumrithi Dk Emmanuel Nchimbi aliyeteuliwa kuwa mgombea mwenza, Makalla amesema hiyo si sehemu ya ajenda zilizopo.

"Hiyo haipo kwenye ajenda, nimetaja ajenda tatu na ndizo zitakazokuwepo," amejibu Makalla kuhusu hatma ya nafasi ya Katibu Mkuu.


Ajibu kuhusu aliko Wassira

Katika mkutano wake huo, Makalla amesema kutoonekana kwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho bara, Stephen Wassira ni suala la ratiba na si vinginevyo kama inavyoelezwa.

Ufafanuzi wa Makalla unajibu kauli mbalimbali zinazoibuliwa katika mitandao ya kijamii kutoka kwa baadhi ya wadau wakihoji, yuko wapi Wassira ambaye hakuonekana kwa siku kadhaa hadharani.

Baadhi wamekwenda mbali zaidi na kusema, pamoja na kutoonekana majukwaani, hakuonekana hata katika msiba wa Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya.

Msuya (94) alifariki dunia Mei 7, 2025 katika Hospitali ya Mzena, Kijitonyama jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu ya moyo ambayo yalimsumbua kwa kipindi kirefu.

Kwa mara ya mwisho, Wassira alionekana hadharani alipofanya ziara yake katika Wilaya zote za Mkoa wa Dodoma na baada ya hapo hakuonekana tena.

Amesema ni kawaida kwa kiongozi kupumzika baada ya ziara na shughuli mbalimbali za kiofisi kama ambavyo mwingine yeyote angefanya.

"Ni Mzee hana jambo lolote kwa hiyo ni ratiba kwamba bwana nitafanya hapa, nikikamilisha nitapumzika kuna jambo la familia, kuona watoto, hata mimi mwenyewe lazima nijiwekee hilo," amesema Makalla.

Akifafanua zaidi, amesema hata yeye amekuwa akipumzika baada ya ziara, anafanya kazi nyingine za kiofisi na vikao vya kawaida.

"Kwa hiyo hata mimi nikipotea wiki moja mtasema mwenezi amekata moto au amekata pumzi hapana bwana ni suala la ratiba," amesema.