Hapi ahoji fedha za ‘tone tone’ Chadema, yenyewe yajibu
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Taifa, Ally Hapi.
Kahama. Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Taifa, Ally Hapi, ameitaka Chadema kuweka wazi vyanzo vya fedha inazopokea kutoka kwa marafiki na wafadhili wake wa nje ya nchi, huku akihoji sababu za chama hicho kuendelea kuendesha kampeni ya uchangishaji fedha ya “tone tone” wakati kinadai kupata ufadhili kutoka nje.
Akizungumza jana Juni 18,2025 katika mkutano wa hadhara wilayani Kahama mkoani Shinyanga, Hapi alisema wananchi wana haki ya kufahamu ni nani anayefadhili shughuli za kisiasa za Chadema, kiasi cha fedha kinachopokelewa na namna fedha hizo zinavyotumika.
“Mimi ninawauliza viongozi wa Chadema, fedha mnazosema mlipata kutoka kwa marafiki zenu wa nje ya nchi zilitoka kwa nani, zilikuwa kiasi gani na zilitumika kufanya nini? Watanzania wanastahili kuambiwa ukweli wote kuhusu fedha hizo,” alisema Hapi.
Alisema uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya fedha ni jambo muhimu kwa vyama vyote vya siasa, hivyo Chadema inapaswa kutoa maelezo yatakayosaidia kuondoa maswali yaliyopo miongoni mwa wananchi na wanachama wake.
Hapi pia alihoji uhalali wa kampeni ya “tone tone”, akidai kuwa bado kuna maswali yanayohitaji majibu kuhusu vyanzo vya fedha vinavyotumika kuendesha shughuli za chama hicho.
Mbali na suala la fedha, Hapi alizungumzia mjadala wa Katiba Mpya akisema hoja hiyo si mali ya chama chochote cha siasa bali ni ajenda ya kitaifa inayowahusu Watanzania wote.
Alisema mchakato wa Katiba Mpya ulianza wakati wa utawala wa Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, ambapo Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliundwa na baadaye Bunge Maalumu la Katiba likajadili rasimu iliyowasilishwa.
“Ni muhimu kutambua kuwa Katiba Mpya si suala la chama kimoja. Ni jambo linalohitaji ushiriki wa Watanzania wote ili kufikia mwafaka wa kitaifa,” alisema.
Chadema yajibu
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Chadema, Gerva Lyenda, alisema chama hicho hakijahusika kukwamisha mchakato wa Katiba Mpya kama inavyodaiwa, akisisitiza kuwa uamuzi wa kuendeleza mchakato huo uko mikononi mwa Serikali.
Lyenda alisema Chadema imekuwa miongoni mwa wadau wanaosukuma agenda ya Katiba Mpya kwa muda mrefu, kwa lengo la kuhakikisha maoni ya wananchi yanazingatiwa katika kupata katiba inayokidhi matarajio ya Watanzania.
“Sisi hatujakwamisha mchakato wa Katiba Mpya. Hatuongozi Serikali, hivyo maamuzi ya kuendeleza au kutokuendeleza mchakato huo yako mikononi mwa Serikali,” alisema.
Kuhusu madai ya ufadhili kutoka nje ya nchi, Lyenda alisema si jambo la kipekee kwa vyama vya siasa kuwa na marafiki au taasisi zinazovisaidia katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kisiasa na kijamii.
Alisema fedha hizo hupokelewa kwa malengo maalumu, ikiwemo mafunzo kwa wanawake, vijana na wazee, na kwamba matumizi yake hufuata taratibu zote za kisheria na kiutawala.
“Chadema, kama ilivyo kwa CCM na vyama vingine, kina marafiki nje ya nchi. Fedha zote zinazoingia kwenye akaunti za chama hukaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kila mwaka tunapata hati za ukaguzi,” alisema.
Akijibu madai kuhusu kampeni ya “tone tone”, Lyenda alisema fedha zinazochangwa na wanachama na wafuasi wa chama hicho hutangazwa hadharani baada ya kila mkutano na kutumika kugharamia shughuli mbalimbali za chama.
“Huwa tunatangaza wazi kiasi kilichokusanywa katika kila mkutano. Hakuna jambo la siri. Kama kungekuwa na utakatishaji fedha, mamlaka husika zingechukua hatua za kisheria,” alisema.
Aliongeza kuwa makusanyo ya “tone tone” hayajawahi kuzidi Sh18 milioni kwa mwezi na fedha hizo zimekuwa zikitumika kuendesha shughuli za chama, ikiwemo kampeni za Katiba Mpya na harakati mbalimbali za kisiasa.