Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hukumu yaibua mikasa ya kupita bila kupingwa

Dar es Salaam. Miongoni mwa mijadala iliyoshika kasi hapa nchini, hasa katika medani ya siasa ni hukumu ya Mahakama Kuu kuzuia wagombea wa nafasi mbalimbali kupita bila kupingwa katika chaguzi zinazofanyika hapa nchini hasa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2019 na Uchaguzi Mkuu wa 2020.

 Hukumu hiyo inatokana na kesi namba 19 ya 2021 iliyofunguliwa na Naibu Katibu Mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo, Joran Bashange.

Hukumu hiyo imekuja kufuatia malalamiko ya vyama vya upinzani kuhusu kuvurugwa kwa chaguzi, ukiwemo Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019 ambapo CCM ilishinda kwa asilimia 96 na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Hukumu hiyo iliyotolewa Machi 29, mwaka huu, Mahakama Kuu ya Tanzania imebatilisha Sheria ya Serikali ya Mitaa Sura Na.292 kifungu cha 45(2) na kifungu cha 13 (7) pia sheria ya uchaguzi sura Na.343 kifungu cha 44, ikisema vinakinzana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977, ibara ya 21(1 na 2).

“Hivyo tunaendelea kuvitupilia mbali vifungu hivyo kutoka katika vitabu vya sheria,” inasomeka sehemu ya hitimisho la hukumu hiyo iliyoamuliwa na jopo la majaji watatu waliosikiliza kesi hiyo; John Mgetta (kiongozi wa jopo), Dk Benhajj Masoud na Edwin Kakolaki, vifungu hivyo vinakinzana na Katiba.

Kimsingi hila, vituko na kadhia wanazokumbana nazo wagombea wa upinzani mara kwa mara katika chaguzi zimekuwa ni sehemu ya maisha ya kisiasa hapa nchini licha ya mambo hayo kutia doa demokrasi lakini hatua zinazostaili hazikuwa zikichukuliwa.

Hukumu ya Mahakama Kuu kama haitatenguliwa na Mahakama ya Rufani iwapo Serikali itakata rufaa inaweza kuwa mwanga wa kukua kwa demokrasia na kuzuia wagombea hasa wa chama tawala kupita bila kupingwa

Hata hivyo baadhi ya wachambuzi wa kisiasa, sheria na wagombea walioenguliwa kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 wanasema licha ya uzuri wa hukumu hiyo kama hakutafanyika mabadiliko ya Katiba mambo yanaweza kuwa yaleyale.

Monica Nsaro aliyegombea jimbo la Nzega vijijini kupitia Chadema, anasema uamuzi wa Mahakama utasaidia kuondoa mizengwe wakati wa uchaguzi.

“Uamuzi wa mahakama ni mzuri, lakini uende mali zaidi. Wasimamizi wa uchaguzi wasiteuliwe na Rais,” alisema Nsaro aliyedai kuenguliwa kinyume cha utaratibu.

“Mimi nilienguliwa wakati tayari nimeshapitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Kwanza nilipewa fomu feki, lakini baadaye watu wakanidokeza hivyo nikapata fomu halisi nikazijaza zote na siku moja kabla ya kuzirudisha, mmoja wa walinzi wangu alinigeuka na kuipoteza fomu feki, lakini kwa kuwa nilikuwa na fomu halisi nilifanikiwa kuirudisha,” anasema

Nsaro anasema baada ya kurudisha fomu na kupitishwa kuwa mgombea, aliwekewa pingamizi.

“Jioni ile ile nilikwenda Tabora mjini kwa wanasheria wetu wakajibu pingamizi kesho yake nikarudisha, lakini wakaibua pingamizi jingine kuwa wadhamini wangu hawanitaki,” anasema

Anasema demokrasia haiwezi kupiga hatua kama kila kukicha utaratibu wa kuwaengua wapinzani utakuwa ukiendelea na kuratibiwa na viongozi wa Serikali.

Kwa upande wake Peter Mdidi aliyegombea ubunge na udiwani kupitia Chadema katika jimbo la Mvomero, anasema alijikuta akihatarisha maisha yake kwa kutekwa na watu anaodai aliwafahamu siku aliporejesha fomu Agosti 25, 2020 na hivyo kushindwa kurejesha fomu zake.

“Dawa ya mambo haya yote ni Katiba mpya, kwani iliyopo ina viraka vingi. Hatuna Tume huru ya uchaguzi kwa sababu ya Katiba hii, ni tume ambayo Rais anateua wasimamizi wakati yeye ni Mwenyekiti wa chama tunachopingana.

“Hata Jeshi la Polisi nalo linajikuta likitumika kwa masilahi ya chama tawala na wagombea wake,” anasema.

Suzan Kiwanga aliyegombea jimbo la Mlimba na kuenguliwa, anasema hukumu hiyo imetenda haki.

“Majaji wamefuata Katiba japo tunasema haifai, lakini pamoja na ubovu wake, sheria za uchaguzi ziko kinyume chake, tunataka kabla ya kwenda kwenye uchaguzi wa 2024 na wa 2025, haya mambo yarekebishwe,” anasema.

Wakili Furgence Massawe anasema hukumu hiyo itaongeza amani na utulivu katika uchaguzi za ngazi zotezitakazofanyika miaka ijayo.

Kwa mujibu wa Massawe, uamuzi huo unaondoa utaratibu unaoruhusu mgombea kupita bila kupingwa hasa inapotokea hana mpinzani.

“Hii itafanya kama mgombea hana mpinzani hatapitishwa moja kwa moja, bali atalazimika kufanya kampeni na kupigiwa kura ya ndiyo na wananchi. Atashinda iwapo atapata asilimia 50 ya kura hizo, lakini kinyume chake hatashinda,” anasema.

Wakili huyo ambaye pia ni Naibu Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), anasema hatua hiyo itachagiza kukoma kwa figisu katika chaguzi zinazotarajiwa kufanyika baadaye.

“Kulikuwa na zile tabia za mgombea akishapita anamtengenezea mazingira mpinzani wake ya kushindwa kuwania nafasi hiyo ili apite bila kupingwa.

Mtazamo wa Massawe unaungwa mkono na mbobevu wa sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Emeritus Fimbo anayesema wanaokosa wapinzani wapigiwe kura za ndio au hapana.

Hata hivyo, anasema ni idadi ndogo ya wagombea ndiyo waliokuwa wanapita bila kupingwa na walionekana zaidi katika uchaguzi wa mwaka 2020, akisema kulikuwepo na kasoro nyingi.

“Lakini sasa hivi hatuwezi kuwaona tena kwa haya maridhiano na hata kama watakuwepo wafanye uchaguzi wapigiwe kura ya ndiyo au hapana,” anasema.

Kwa mujibu wa Profesa Fimbo, uamuzi huo utachagiza utekelezwaji wa haki ya msingi ya mwananchi kuchagua kiongozi anayemtaka, badala ya kujibiwa kuwa hakuna kupiga kura kwa kuwa mgombea amepita bila kupingwa.


Uhalali wao

Mwenyekiti wa Ngome ya vijana ACT wazalendo Taifa, Abdul Nondo anasema viongozi waliopita bila kupingwa katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019 na Uchaguzi Mkuu wa 2020 sio halali

“Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, vijiji na vitongoji asilimia 96 waliopita bila kupingwa 2019 sio halali, madiwani zaidi ya 400 waliopita bila kupingwa 2020 sio madiwani halali na wabunge katika majimbo 28 waliopita bila kupingwa sio wabunge halali sababu hawakuchaguliwa na wananchi,” alisema.

Katibu mkuu wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), Julius Mwita, anasema uwepo wa baadhi ya wabunge walioingia bungeni kwa hila kunaliondolea uhalali Bunge.

“Mahakama Kuu imetoa hukumu kuhusu watu wanaopita bila kupingwa, imesema msimamizi wa uchaguzi kutamka kwamba mtu amepita bila kupingwa, awe mwenyekiti wa Serikali za mitaa awe mbunge, diwani awe Rais ni kinyume cha Katiba.

“Mle ndani (bungeni) kuna wabunge wamepita bila kupingwa. Mimi mwenyewe walipora kwenye uchaguzi…” anasema.

Hata hivyo, akizungumzia uhalali wa viongozi hao kwa mujibu wa hukumu hiyo, Wakili Dk Rugelemeza Nshalla anasema wao si miongoni mwa walioshtakiwa katika kesi hiyo, hivyo hukumu haiwahusu.

“Kuna mgongano wa kisheria kwenye hili wengine wanasema nafasi zao zinakomea hapo lakini wengine wanasema hawahusiki kwa sababu si miongoni mwa walioshitakiwa,” alisema.

Dk Nshalla anasisitiza wabunge na madiwani hao kutohusika kwa kile alichofafanua kuwa hawakushtakiwa ili wasimame mahakamani kujitetea.

“Ili umhukumu mtu lazima umpe nafasi ya kujitetea kwa mujibu wa sheria, kwa muktadha huu wabunge na madiwani waliopita bila kupingwa hawahusiki,” alisema.


Kilichomsukuma Bashange

Naibu Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo (Bara) Joran Bashange, aliyefungua kesi hiyo mwaka 2021 anasema ameruka vihunzi vingi kutoka ndani na nje ya serikali hadi hukumu hiyo inatolewa.

Kwa mujibu wa Bashange, uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kubatilisha vifungu vya sheria vinavyoruhusu kuwapo kwa wabunge na madiwani wanaopita bila kupingwa una maana kubwa katika demokrasia nchini na utasaidia kuwarudisha katika mstari wananchi waliokata tamaa ya kushiriki katika chaguzi.

Anasema baadhi ya wananchi hawajitokezi kwenda kupiga kura kutokana na vitendo vilivyokuwa vinajitokeza vya wagombea kupitishwa bila kupingwa.

Bashange, aliyewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, alifungua kesi hiyo Mahakama Kuu Masjala Kuu, Dar es Salaam, dhidi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, akipinga kuwepo kwa wabunge na madiwani wanaotangazwa kupita bila kupingwa.

Katika kesi hiyo ya kikatiba namba 19 ya mwaka 2021, Bashange alikuwa akihoji uhalali wa kikatiba wa kifungu cha 44 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi (NEA), Sura 343 kinachoruhusu kuwepo kwa wabunge wanaopita bila kupingwa.

Pia, alikuwa akihoji uhalali wa kikatiba wa vifungu vya 45(5) na 13 (7) vya Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Sura 292 vinavyoruhusu kuwepo kwa madiwani wanaopita bila kupingwa.

Hivyo, mahakama hiyo imesema ni batili kwa kukiuka masharti ya Ibara ya 21(1) (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kama ambavyo imekuwa ikirekebishwa mara kwa mara.

“Hivyo tunaendelea kuvitupilia mbali vifungu hivyo kutoka katika vitabu vya sheria,” inasomeka sehemu ya hitimisho la hukumu hiyo.

Uamuzi huo wa mahakama umekuja wakati Bunge la sasa hivi likiwa na wabunge 28 waliopita bila kupingwa katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020. Pia wamo madiwani waliopita bila kupingwa.

Unaweza kusema uamuzi huo umepokewa kwa shangwe na baadhi ya wanasiasa, hasa upinzani ambao katika uchaguzi wa mwaka 2020 walilalamikia rafu za mchakato huo, ikiwemo wagombea wao kuenguliwa kwenye nafasi mbalimbali.

Katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Bashange anasema “ukiangalia katika takwimu za uchaguzi kila mwaka namna ya watu kushiriki mchakato huu ilikuwa inashuka, hii ilihitimishwa mwaka 2020 ambapo zaidi ya asilimia 90 ya wagombea wa upinzani walienguliwa.

“Ilikuwa anayebaki ni mgombea dhaifu, mwenye nguvu anaenguliwa, ndio maana wananchi walikata tamaa na kuona hakuna sababu ya uchaguzi. Haki yao kikatiba waliiona haina maana,” anasema Bashange.

Bashange anasema katika mfumo wa demokrasia unataka wengi wapewe lakini kuwa na mazingira ya tabaka la wengi waliokata tamaa, hapo hakuna demokrasia tena. Hata hivyo, Bashange anasema kwa uamuzi wa mahakama watu watajitokeza wengi kushiriki uchaguzi na kupiga kura.

Anasema, “kwa sababu kutakuwa na ushindani, hata ikitokea amebaki mmoja basi atapigiwa kura ili aonekane ameshinda au kukubalika katika eneo lake, lazima apate kura zaidi ya nusu.

“Haya ndiyo masharti yaliyomo katika ibara ya 30 kwa ajili ya urais, kama unafanya mambo yote, ukibaki mgombea peke yako uhakikishe unapata kura zaidi ya nusu. Kama una uhakika wa kupata zaidi ya nusu ya kura kwa nini uweke mapingamizi au kutumia rushwa.

Bashange, aliyewahi kuwa Katibu wa Bodi ya Wadhamini wa CUF, anasisitiza kwa hatua hiyo, hivi sasa demokrasia itakuwa imefunguliwa milango na wananchi watatumia uhuru wao wa kuchagua viongozi wanaowahitaji.

Naibu katibu mkuu huyo, anabainisha kuwa ile tabia ya watu waliokuwa wanatumia vitendo vya rushwa, mapingamizi au nguvu ili kupita bila kupingwa sasa hivi havitakuwa na maana tena.

“Ikitokea mapingamizi yamewekwa lazima msimamizi wa uchaguzi ahakikishe upate zaidi ya nusu za kura utakazopigiwa na wananchi. Kama hujapata kura hizo, uchaguzi utafutwa na kurudiwa upya, jambo litakaloleta gharama kubwa kwa Serikali.

“Sasa hivi watu watakwenda katika uchaguzi kwa ushindani halisi, kama wewe hukubaliki katika jamii huwezi kujitosa katika mchakato husika,” anasema Bashange.


Kwa nini alifungua kesi?

Kwa mujibu wa Bashange, aliona kuna uvunjaji wa Katiba katika vifungu cha 45 (2) katika sheria ya uchaguzi sura 343. Pia kifungu cha 13 (7) katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa, sura 262.

Anasema kwa mujibu wa Katiba ibara ya 5, moja ya haki ya Mtanzania aliyefikisha miaka 18 ni kupiga kura na katika Ibara 21 (1) inaonyesha namna wananchi wanavyoweza kushiriki katika chaguzi.

“Ibara ya 67 ya Katiba imeorodhesha viongozi wanaopatikana kwa njia ya uchaguzi kuanzia Bunge ambao ni wale waliochaguliwa katika majimbo, 10 wanaoteuliwa na Rais na viti maalumu. Hakuna anayepita bila kupingwa.

“Nikaona vifungu hivi vinakinzana na Katiba Ibara ya 26 (1), kila mtu anatakiwa kuheshimu Katiba na sheria za nchi. Pia katika ibara ya 26 (2) inaeleza mtu anayeona hili halifanyiki anawajibika kuchukua hatua kuhakikisha Katiba inahifadhiwa na sheria za nchi,” anasema.

Kutokana na hilo, Bashange aliamua kukimbilia mahakamani kufungua kesi kuueleza mhimili huo kuhusu vifungu hivyo kukinzana na Katiba, akiomba ivibatilishe ili iweze kuvifuta.


Changamoto zilizomkabili

Bashange anasema kesi hiyo, aliifungua mwaka 2021, lakini alikumbana na changamoto mbalimbali, ikiwemo Serikali kutumia nguvu kubwa kuhakikisha kesi inaondolewa bila kusikilizwa.

“Walitumia nguvu kubwa kuhakikisha wanaweka mapingamizi ili kesi ife katika hatua za mwanzo, kabla ya kusikilizwa. Kwa sababu ikifika hatua ya kusikilizwa muda mwingine hoja zao (Serikali) zinakuwa hazina mashiko.

“Mwaka wa kwanza ulikuwa ni mapingamizi karibu manne katika kesi, kwa vile ilikuwa ya Kikatiba yenye maslahi makubwa kwa Taifa nilifanikiwa kusimama imara kwa sababu nyuma yangu niliwakilisha kundi kubwa la wananchi walioonewa,” anasema.


Marekebisho ya sheria

Bashange anasema bado ni vikwazo katika demokrasia ya vyama vingi, ingawa tayari suala hilo limeshaanza kufanya kazi katika kikosi kazi na ACT-Wazalendo kilipeleka mapendekezo yake.

“Ikitokea hazijafanyiwa kufanyiwa marekebisho na Serikali tutachukua hatua pia kwa njia ya mahakamani,” anasema Bashange.