Kanuni za upinzani fyatu usiofyata bali kufyatua

Baada ya kugundua kuwa upinzani kayani haufanikiwi kufyatuka na kulifyatua hadi kulinyaka dola, nimekuja na njia ya kuupiga tafu lau uondoke kwenye ufyatu wa kukamia na kuyafyatua maulaji ya dezo ya kaya hii ya mafyatu fyatuliwa.

Kwa kituo na utuo bila ngoa, nakuja na kanuni za upinzani wenye siha kisiasa bila usaha na visasi. Hivyo, wote mnaojiita wapinzani, soma hii kitu kwa makini. Zifuatazo ni kanuni za upinzani wenye siha kisiasa ambazo zitaacha historia ya kuuwezesha upinzani kunyakua ulaji tena haraka na kirahisi:

Mosi, ili ufanikishe upinzani wako, lazima upinge kila kitu kifyatufyatu na kifyatuzi.

a) Kama chata twawala wakila wewe unawaaminisha mafyatu kuwa, wakikupa dola, utakuwa ukifunga kila siku. Mfano, wafunge kamba kuwa hutatumia mashangingi na mashankupe wala maboeing na mapipa mengine kusafiri na kutanua.

Muhimu, wahakikishie kuwa utapiga marufuku ununuzi wa mashangingi. Badala yake useme utanunua bajaj kwa ajili ya kusafirisha wanene wote. Ili kuokoa njuluku, kila mnene atajifunza kuendesha bajaji. Hakuna mnene atakayekuwa na dereva, mfagizi, fyatu wa bustani, ngwea za dezo, walinzi na wasaidizi wanaolipiwa kwa njuluku ya kodi za mafyatu. Waaminishe kuwa hutavaa suti, badala yake utavaa mgolole. Mashangingi na suti vinachafua mazingira.

Uhakikishie kuwa utafyatua miujiza ya kisiasa. Mfano, waaminishe unawapenda hadi kutumia bajaj bila kujali hatari ya kugongwa na madereva wasiojali. Hii iite sera ya kujitoa kafara kwa ajili ya kaya kwa sababu unaipenda kuliko uhai wako. Kwa wanaojua bajaj zinavyonyonga, watakuamini kweli unaipenda kaya hata kama baadaye utaiponda hadi kutoa uhai wako kwa ajili yake.

Kadhalika, waaminishe kuwa hutakula kwenye mahoteli ya kitalii, bali utakuwa unakula kwa maza ntilie ili kukuza uchumi wa ndani. Piga marukufu semina, warsha na ujumbazi mwingine.

b) Piga marufuku ruzuku. Kwa nini kila kitu kiwe kibaya ila ruzuku? Unaruzukiwa nini wakati unachofanya ni kupinga na kuanzisha vurugu? Waaminishe mafyatu kuwa ruzuku vinayopewa vyama vya siasa itakwenda kwa wafanyakazi na wakulima. Hii itasaidia kujua umefyatuka na hupendi njuluku.

Hapa, ongeza kuwa hutokuwa na mabaunsa aka bodyguards. Unaogopa nini wakati huli wa kuiba cha fyatu yeyote hadi ulindwe kama mfungwa hatari?
Kadhalika, uwaaminishe mafyatu kuwa umchumi ambaye hutawalipa njuluku washikaji zako hasa waume au wake za wanene eti kwa sababu mnachangia ‘bedrooms’ (chumba cha kulala). Yours is boardroom but not bedroom politics ( Chumba chako ni cha mikutano si siasa za chumbani).

Uwaaminishe kuwa vitegemezi vyako havitapelekwa kusoma, kujiangalia au kutibiwa majuu kwa vile utafufua na kuimarisha huduma za afya. Muhimu, waaminishe kuwa hutakuwa na misafara sumbufu ya kufunga barabara wala wasanii wa kukusifia wakati wanapaswa kukufyatukia na kukufyatua hata kukuzomea kama alivyosema Chalalamika. Waambie mafyatu uko radhi kukosolewa na kutoa zawadi kwa wakosoaji ambao watakulaumu si kusifia ujinga, upoyoyo au uzwazwa.

c) Upinge kila kitu na kwa kelele kuu. Mfano, bibie akitaka kwenda majuu kudanda, ufyatuke kuwa anazurura na kupoteza njuluku za mafyatu. Asipofanya ziara kama mwendaze, piga kelele kuwa ni mshamba anayeogopa kwenda majuu kuzoza kimombo au kukwea pipa. Akileta wawekezaji, unawaita wachukuaji. Akinunua madege, mwambie anapoteza njuluku kwani, mafyatu hawayataki madege bali uhuru usio na mipaka.

Akijenga barabara, madaraja, vyanzo vya kuzalisha umeme, viwanja vya ndege, reli ya kisasi, mwambie mafyatu hawataki vitu bali utu. Tangaza hutotumia madege wala miundombinu. Uulize bila aibu wala woga hata ukichekwa kwa ufyatu wako kuwa tangu lini miundo ikawa mbinu kama siyo mbinu ya kuibia mafyatu? Umeme ukikatika kutokana na ukame, unapiga kelele kuwa rahisi amemkosea Mungu. Maji yakiadimika, unafyatuka kuwa rahisi anaoga sana. Akiongea kitasha, unaongea kimanga. Waishiwa wakiongea kiswanglish, unaongea Kimasai, Kisambaa na Kibarbaig au siyo?

d) Kama chata twawala kikianzisha sera ya uchawa unaipinga kwa kuanzisha sera ya usafi ya kuondoa ukunguni, upanya na uroboto.
Mwisho, lazima uwe bingwa wa kufyatuka na kufyatua. Kila jambo lazima bila unyong’onyo uanzishe payo, na ngebe yosayosa hata chawa, kunguni, na viroboto wakusikie na kuelewa. Uwe mkali kama koyokoyo ukihakikisha kila wanachofanya wapinzani wako ni upoyoyo, uongo na hakifai hata kama chafaa kuwaonyesha wewe ni fyatu au siyo? Jikumbushe kibonzo cha zamani cha Bayoyo.

Acha niache nisijipinge mwenyewe!