Kinana aitupia dongo Chadema

Muktasari:

  • Asema walikwenda katika vikao vya maridhiano na CCM wakiwa na ajenda binafsi, ahoji sababu za maandamano wakati Bunge likikusanya maoni, Mnyika amjibu akisema ni kauli za kupotosha umma.

Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana amezungumza kwa mara ya kwanza kuhusu sababu za kukwama kwa mazungumzo ya maridhiano baina ya chama chake na Chadema.

Mazungumzo hayo yaliyofanyika kwa mwaka mmoja, yalianza Mei 2022 katika kikao kilichowakutanisha viongozi kadhaa wa CCM wakiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan na viongozi wa Chadema wakiongozwa na Mwenyekiti Freeman Mbowe.

Hata hivyo, tangu Juni, mwaka jana hadi sasa, hakuna kikao chochote kilichofanyika baina ya vyama hivyo, huku kila upande ukiutuhumu mwingine kwa kusababisha kuvunjika kwa mazungumzo hayo.

Kinana akizungumza na wanachama wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam leo Februari 4, 2024, ameelezea mkwamo wa mazungumzo hayo na kujadili hoja moja baada ya nyingine zilizowasilishwa na Chadema kwenye mazungumzo baina ya vyama hivyo.

Baadhi ya hoja hizo ni kufutiwa kesi za wanachama zaidi ya 400 wa Chadema, viongozi waliokimbilia nje ya nchi kuhakikishiwa usalama, mikutano ya hadhara kuruhusiwa, chama chao kupewa malimbikizo ya ruzuku kwa miaka mitatu, akisema walilipwa Sh2.7 bilioni na wabunge 19 wa Chadema kutolewa bungeni.

Kinana amesema kati ya hoja 11 zilizowasilishwa na Chadema, tisa zilifanyiwa kazi na amekilaumu chama hicho kwa kile alichosema ubinafsi kwa kutaka kutumia jukwaa hilo kueleza matatizo yao binafsi wanayotaka yafanyiwe kazi.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alipotafutwa na gazeti hili, amekanusha madai ya Kinana kuhusu ubinafsi wa chama chake naye akailamu CCM kwa kukwamisha mazungumzo hayo.


Sababu alizozitaja Kinana

Akizungumzia kukwama kwa mazungumzo baina ya vyama vyao, Kinana amesema kumesababishwa na mambo mawili – Chadema kutukana viongozi wa CCM majukwaani na kupeleka manung’uniko yao kwenye kila kikao.

“Tuliwasihi wenzetu, kwamba mikutano ya hadhara imeanza, tafadhali tusitumie hii mikutano kukashifiana, kutukanana, kudhalilishana na hasa kumdhalilisha kiongozi wa nchi. Hatukuomba jambo kubwa, isemeni Serikali, semeni mapungufu ya CCM,” amesema.

Amesema walijitahidi kuvumilia lakini wameshindwa kutokana na Chadema na viongozi wake kuendelea kukashifu viongozi.

Amesisitiza wangependa kuendelea na mazungumzo lakini kwa hali hiyo hawataweza.

“Sasa mnakwendaje kwenye mazungumzo, jana mmedhalilishwa, kiongozi wenu katukanwa, asubuhi mnakutana mnazungumza. Tulifanya hivyo mara ya kwanza, ya pili, ya tatu, ya nne, mwisho tukasema hapa tutaonekana watu wa hovyo,” amesema.

Kinana amesema, “tungependa tuendelee na mazungumzo lakini hatuwezi kuendelea na mazungumzo jioni tumedhalilishwa, kiongozi wetu ameshutumiwa na kudharauliwa, halafu asubuhi tunakutana, tunakunywa chai na kuzungumza, haiwezekani.”

Kuhusu sababu ya pili ya mazungumzo kukwama, amesema ni Chadema kupeleka manung’uniko yao binafsi kwenye kila kikao wanachokaa, ili Serikali ione namna inavyoweza kuyatatua na namna mambo yalivyokuwa yanaenda, wakaona hiyo ndiyo sehemu ya kupatia kila kitu wanachokitaka.

“Wakasema tunakataka Katiba mpya, sisi tukasema mbona Katiba si jambo la CCM na Chadema? Ni jambo la Watanzania wote, vyama vyote, jamii yote, makundi yote, haliwezi kuwa letu,” alisema na kuongeza:

“Wakasema mnaonekana ninyi hamjitambui, kwa vipi? Wakasema hapa kuna vyama viwili; CCM na Chadema tu.”

Amesema Chadema walitaka Rais na Serikali wasihusike kwenye mchakato wa kuandika Katiba mpya.

Hata hivyo, amesema Serikali na CCM waliridhia kuanza mchakato huo kwa kuwa ni hitaji la Watanzania wengi, si la Chadema peke yao.


Mnyika amjibu Kinana

Akijibu hoja za Kinana kuhusu sababu za kuvunjika kwa mazungumzo hayo, Mnyika amesema maridhiano hayo hayajakwamishwa kwa kauli za viongozi wa Chadema kama alivyodai Kinana, bali ni kwa sababu CCM imekataa kufanya marekebisho ya Katiba.

“Mazungumzo tunayofanya yamekwamishwa na CCM sababu kuu ni mbili; Kwanza, CCM hawakutaka marekebisho yafanyike kwenye Katiba ya mwaka 1977 katika maeneo yanayohusu uchaguzi, ambayo yangewezesha kuwa na uchaguzi huru na haki,” amesema.

Mnyika ametoa mfano wa matokeo ya Rais kuhojiwa mahakamani, muundo wa Tume Huru ya Uchaguzi, mgombea binafsi na uamuzi wa tume kuweza kuhojiwa au kupingwa mahakamani kama mtu hakuridhika na maamuzi, kuwa vyote hivyo vilikataliwa.

Ametaja sababu ya pili ya kukwama mazungumzo kuwa ni CCM kukataa kuendelezwa kwa mchakato wa Katiba kwa ratiba inayoanza sasa na katika muundo na vyombo vitakavyowezesha kujenga muafaka wa kitaifa.

“Si kweli kwamba CCM ilikataa Katiba mpya kwa kigezo kwamba Chadema ilitaka ijadiliwe na CCM peke yake. Hayo maelezo aliyosema Kinana hayana ukweli, Chadema tulipeleka mapendekezo kwao ya kupeleka muswada wa mabadiliko ya Katiba na ratiba itakavyokuwa,” amefafanua.

Amesema jambo lingine alilopaswa kulizungumza Kinana hadi mazungumzo yanakwama Juni, 2022 kuna hoja ambazo hazikuzungumzwa kabisa.


Miswada iliyopitishwa

Akizungumzia miswada iliyopitishwa na Bunge mwishoni mwa wiki iliyopita, Kinana amesema ilipelekwa bungeni kwa lengo la kuboresha mazingira ya uchaguzi kwa mwaka 2024 na 2025, lakini Chadema waligoma, wanataka mabadiliko yaanzie kwenye Katiba.

Sheria hizo ambazo sasa zinasubiri saini ya Rais Samia Suluhu Hassan ili zianze kutumika, ni Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani; Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Sheria ya Vyama vya Siasa zote za mwaka 2023.

Kinana amesema kabla ya kuwasilisha miswada ya sheria hizo bungeni, Chadema na wadau wengine walikuja na maoni kwamba CCM wamekuwa na utamaduni wa kupeleka mambo makubwa bungeni kwa hati ya dharura.

Walisema ‘sheria zinazohusiana na uchaguzi mtakazozipeleka bungeni ni lazima zipitie mchakato wa kawaida’ na tumeridhia miswada tulipeleka kwa njia ya kawaida Novemba mwaka jana, miswada ilianza kusomwa bungeni,” amesema Kinana.

Kinana amesema Chadema pia walihitaji miswada hiyo iondolewe bungeni huku wakijua wamewatuma viongozi wao wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha) na Baraza la Wanawake (Bawacha) kutoa maoni mbele ya kamati.

“Unasema tuondoe miswada bungeni halafu papohapo mnakuja kutoa maoni, sasa tukiitoa mtakuja kutoa maoni wapi? ‘Toa miswada bungeni’ lakini papohapo mnaanza kuandamana, hatujui tushike lipi, ni mkakanganyiko,” amesema.

Akizungumzia sheria iliyopitishwa, Kinana amesema ni nzuri kuliko zote zilizokuwepo tangu kuanzishwa kwa nchi, kwa madai kuwa inakidhi mahitaji na matakwa ya Taifa.

“Sheria waliyoitunga juzi ni bora kuliko iliyowafikisha huko lakini bado wanasema haifai, lakini ile ya mwaka 2015 wanasema inafaa,” amesema Kinana.

Katika hilo, Mnyika (pichani) amepinga akisema katika miswada iliyopitishwa, bado matokeo ya urais hayataweza kuhojiwa mahakamani, hakutakuwa na Tume Huru ya Uchaguzi (kwa ibara ya 74 ndiyo imeweka muundo, uteuzi, kinga na uendeshaji usio huru wa uchaguzi)

Hata hivyo Kinana, amesema wakati mwingine kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi si kigezo cha kushinda uchaguzi, (Chadema) wanapaswa kujua hilo bali kujipanga na kuwa na sera nzuri kwa kuongea na Watanzania.

Amesema sheria ya mwaka 1995 ambayo wanaoponda, ndiyo iliyowafanya wapinzani wakawa na wabunge 115 na madiwani zaidi ya 1,000 mwaka 2015.