KONA YA FYATU: Sasa Maza ni Profesa Emeritus, si doktari

Kwa vile sifa zinatoka kila kona kuwa amefanya makuu na makubwa mengi hata kama hajawahi kushika chaki wala kufundisha hata chekechea, maza sasa ni Prof Emeritus. Huu ndiyo urathi wa jiwe. Isitoshe, si vibaya kumtia moyo kipenzi maza yetu.
Naona yule anasonya cheo gani hiki ambacho siyo udoktari wa heshima. Wajua maana yake? Ni profesa mstaafu. Alifundisha na kustaafu chuo gani? Tafadhalli sana. Usiniulize. Mimi ni kama fyatu Paulo na makasisi. Fuata nikwambiayo siyo nifanyayo fyatu wangu. Mafyatu wameniomba nimuombe maza akubali kupewa hadhi hii. Usiniulize toka chuo gani? Kwani, lazima chuo?
Nani anashindwa kufyatua chuo feki na kufyatua vitu kama hivi? Wanaotaka kunifyatua kwa kuja na ubunifu huu, wajiulize. Mbona mafyatu wengine wanapomtunuku hamuhoji bali kuimba kwaya doktari doktari utadhani vyura na chawa? Sasa, mtake msitake, mtaanza kuimba prof emeritus hata kama wengine hamuwezi kuitamka.
Wala sisi hatutakuwa wa kwanza. Mbona M7 na mke wake walipewa udoktari wa heshima kwa pamoja ukiacha mbali Grace Jongwe wa kule Zimba za Mabwe aliyejitia kuusomea kwa miezi sita akaishia kuumbuka alipobanduliwa Jongwe? Alhaj, Profesa, Dk ustaadh, mhashamu Idi Amin aliwahi kusema kuwa watawaliwa wanapaswa kuwapenda watawala wao.
Nami nasema lazima waliwa wawapende na kuwasifia wanaowala, sorry, wanaowatawala. Kama wengine wamewapa shahada hizi na vyeo vitukufu, kama wachunaji wamejipachika utume, unabii, uaskofu, na upuuzi, sorry, utapeli, sorry, utukufu mwingine, kwanini iwe kosa kwetu au kwa maza kusifiana na kutunukiana na kuunga?
Raha jipe mwenyewe au mpeane. Kuna kosa gani, mfano, kumpa dingi kipenzi cha maza uprofesa ili afanane ni waivu wake? Isingekuwa katiba yetu kutoliona hili, ningependa bwana nkubwa aitwe rahish kwa vile bi nkubwa ni rahis. Wakwe na watoto wao ningependa waitwe marahisho ili kuweka ulali katika ulaji wa kifamilia. Ikiwapendeza, chata lake, familia, mawaziri, marafiki, na hata mafyatu wapewe udoktari wa heshima. Kwani, lazima kuunga mkono juhudi bila kuwa chawa wala kunguni? Si inapendeza kwa kila mnene kuwa na cheo na shahada nene?
Mbali na ‘kuunga mkono jihitihada’, tunataka kuwakomesha mawazi-ri wanaotunyanyasa na kutukoga kwa udoktari tena uchwara na siyo kama huu mtukufu wa kupewa na kusifiwa kama njia ya kuunga mkono jitihada.
Kama wengine waliitwa Mungu bila kuchukia wala kuwaonya waliofanya hivyo, hamuoni kuwa hii inapendeza na kuvutia?
Kwa sababu kusifia nayo ni sera, kwa nini mafyatu wasiiunge mkono? Kama hata chawa wanaongea na kuimba sifa, sisi ni nani? Ni mwanakwaya gani aliwahi kuuliza mantiki ya wimbo auimbao? Ni abiria gani aliwahi kuuliza sifa za dereva?
Fuata nyuki urambe asali. Kama alivyovunga fyatu mgoshi Yusif Makambale kuwa mama amewapa asali warambe, nani hataki asali hata kama asali yenyewe mafyatu hatuioni? Sie tunakula kwa imani au macho wakati akina mgoshi wakiramba asali kupitia vitegemezi vyao vilivyopewa ulaji mnene na mnono katika mfumo wa kifamilia zenye majina manene.
Mafyatu tunaanza na prof emeritus. Kama haitatosha, kama yule profedheha Kabundi wa magamba alivyomuita mwendaze aliiyemuumba maza Mungu, tutamuita muungu mwenyepenzi na mwenzi kipenzi cha mafyatu hata kama hatupendwi. Katika nchezo wa karata tatu, lazima ufyatuke na kufyatua ili urambishwe asali. Japo wengi watashangaa kwa nini mafyatu wazima tena wasomi tunafyatua kitu siyo kituko kama hiki. Kwani hao waliomwita mwendazake ni watoto au maamuma?
Kwa taarifa yenu, kuna aina mbili za uumbaji. Upo ule wa mwenyewe Subhana na ule wa ngurumbili ambao kwa kisambaa huitwa political creation or cloning. Hapa, mafyatu tegemezi wasioweza kujisimamia, hujikomba ili kuumbwa au kuibuliwa na wenye maulaji ili wapate tonge na kujaza mifuko yao isiyoshiba wala kushukuru. Hii haijalishi mhusika ni mbukuzi, mtu mzima, mwanaume au mwanamke.
Ni tabia binafsi itokanayo na kutojiamini au kuishiwa mbinu na ubunifu wa kula bata. Huu ni uchangudoa wa kisiasa unaoonekana kuanza kukubalika hata kushabikiwa. Je, nini madhara yake? Kupata wanene wasio na sifa na wanaotumikia matumbo yao badala ya mafyatu. Pia, inawezekana wahusika wakajikuta uso kwa uso na popobawa au poposhungi.
Sisi tumeamua kumpa uprof emeritus si kwa sababu ya kujikomba au kutafuta ulaji. La hasha. Tunafanya hivyo ili kutimiza mila. Naona yule anacheka. Sisi siyo wachumia tumbo. Ni wanafalsafa ambao ukiwaelewa, utajua nini tunamaanisha.
Utakubali kuwa tunachomaanisha ni tofauti kabisa kwa sababu hatuwezi kuumbwa wala kupewa ulaji. Nani awape fyatu ulaji wamfyatue? You know what I mean. Lengo letu ni kumsuta, sorry, kumvuta ili aende chuo akajikunje na kupewa hii kitu ambacho tunamzawadia kama motisha.
Turejee kwa wanaojikomba aka machawa, tokana na uchangu wa kisiasa, wahusika wanaweza kutumiwa hata na maadui toka ughaibuni kutufanyia kitu kibaya kama vile kutununua, kutugeuza vitu, mbali na kutubinafsisha na mali zetu kuanzia bandari hadi washirika wetu wa bedroom. Are you there? Patamu hapo.
Kabla ya kubinafsisha mshirika wangu wa bedroom, nitahanikiza waanze na wao. Kwa warume, mtajijuu. Kwa manzi, haina shobo. Muulize bi nkubwa anavyoshare na wenzake.
Kwanini nami nisipe uprofesa emeritus?