Prime
KONA YA MALOTO: Kauli za viongozi ni hatari kwa Muungano
Viongozi wawili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, hivi karibuni walitoa kauli zilizozua gumzo hasi, kisha wakatokeza kuzikanusha. Ni Waziri wa Afya, Zanzibar, Saada Mkuya, na Naibu Waziri wa Vijana, Ajira na Uwezeshaji Zanzibar, Hassan Khamis Hafidh “Diaspora”.
Kauli ya Mkuya kuhusu watu ambao si Wazanzibari hawawezi kugharamiwa matibabu Zanzibar, pia alichosema Diaspora kwamba ajira nyingi Zanzibar kwenye sekta binafsi, hasa zenye kuhusisha kada ya utalii, zimechukuliwa na wageni. Diaspora aliliahidi Baraza la Wawakilishi, Juni 6, 2026, kuwa anakwenda kuongoza mapinduzi ili ajira zenye kushikiliwa na wasio Wanzanzibari, zichukuliwe na Wazanzibari.
Kauli za Mkuya na Diaspora, moja kwa moja zilitafsiriwa kuwa ni za ubaguzi kwa watu wa Tanzania Bara. Matokeo yake, kila mmoja alilazimika kukanusha kauli yake ya mwanzo. Pamoja na ukanushaji huo, ukweli unabaki kuwa matamshi ya awali hayakutolewa vizuri.
Tanzania ni muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Kauli yoyote yenye kuhusu upande mmoja, lazima ipimwe na kuchujwa kabla ya kutolewa. Vinginevyo, itakwenda kuzua taharuki. Na kwa ulimwengu wa mitandao ya kijamii, hali ni mbaya zaidi.
Mathalan, watu wasio Wazanzibari hawatagharamiwa matibabu, maana yake unasema Watanganyika hawastahili matibabu. Ni kweli, suala la afya siyo Muungano. Je, Mtanganyika anayeishi na kufanya kazi Zanzibar, hastahili huduma. Haishi Tanganyika, anaishi Zanzibar.
Unaposema unaanza mapinduzi ya ajira, ili ajira zilizoshikwa na wasio Wazanzibari ziwe za Wanzibari, kauli hiyo ina maana sawa kuwa Watanganyika waliojiriwa sekta binafsi Zanzibar, watanyang’anywa na kupewa Wazanzibari. Ni matamshi tu, uzuri lugha ni Kiswahili na kinaeleweka vema.
Naamini kuna namna ya kushughulikia changamoto ambazo zinajiri, bila kutoa matamshi yenye kuibua hisia hasi kuuelekea Muungano. Nchi ina Serikali mbili, kwa nini hazikutani na kujadiliana, badala ya kutoa matamshi yenye kuonesha kuna vita baridi baina ya Watanganyika na Wazanzibari?
Mwenyekiti mstaafu wa chama cha ADC, Hamad Rashid Mohamed, katika mjadala wa Miaka 60 ya Muungano, Suza, Aprili 20, 2024, alisema, Watanzania Bara 300,000 wanaishi Zanzibar, halafu Wazanzibari milioni 1.2 wapo Bara. Wazanzibari wanamiliki ardhi kubwa Tanzania Bara, fursa ambayo hawawezi kuipata Zanzibar.
Hamad ni Mzanzibari, anatambua jinsi ambavyo Wazanzibari wanavyonufaika na Muungano. Wakati akitoa takwimu hizo, alisema pia ardhi ambayo anaimiliki Tanzania Bara, ingekuwa ndoto kwake kuipata Zanzibar. Je, viongozi wengine hawaoni? Hasa Mkuya ambaye amepata kuwa Waziri wa Fedha, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Watanzania ni ndugu asilia. Hata kabla ya Muungano, Watanganyika na Wazanzibari walikuwa na uhusiano mkubwa. Mwingiliano wa ndoa na ujamaa mwingine wa kijamii. Kabla ya uhuru wa Tanganyika na Zanzibar, watu walihama upande mmoja kwenda wa pili. Walioana na kujenga familia.
Utamaduni wa Mtanganyika, hasa Pwani, unashabihiana mno na Mzanzibari. Pengine ukiacha siasa, hii ni sababu muhimu ya kudumu kwa Muungano kwa miaka 62 na bila shaka utaendelea kwa karne nyingi zijazo, kama viongozi wataacha maneno yenye kuhatarisha umoja wa kihistoria uliopo.
Sensa ya watu na makazi mwaka 2022, ilitoa picha kuwa katika watu milioni 61, ni milioni tatu tu ndiyo walioshuhudia Muungano. Maana yake, watu milioni 58, wamezaliwa Tanzania ikiwa imeshaundwa. Watu hao hawajui ladha ya Zanzibar wala Tanganyika. Wanachojua pekee ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hata hao milioni tatu, wengi walikuwa watoto. Wameanza kupata akili ya kuchanganua mambo tayari nchi ikiitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hivyo, ladha ya Tanganyika bila Zanzibar, au Zanzibar pasipo uwepo wa Tanganyika, haiakisi kundi kubwa la Watanzania wa sasa.
Mtanganyika au Mzanzibari aliyezaliwa mwaka 1960, alikuwa na umri wa miaka minne wakati Muungano unafanyika. Watu hao katika hali halisi hawana hisia za kweli za upande mmoja wa Muungano, bali wanajua zaidi kuhusu Tanzania. Hao ni wangapi ndani ya milioni tatu?
Weka kadirio, miaka 10 ijayo. Je, Watanzania wangapi kati ya milioni tatu waliopo sasa, waliozaliwa kabla ya Muungano, watakuwa hai sensa ijayo? Ni rahisi kukadiria kwamba kati ya sensa mbili au tatu zijazo, hakutakuwa na Mtanzania mwenye hisia za Utanganyika au Uzanzibari kwa kuzaliwa na kuishi, bali Utanzania.
Undugu wa Watanganyika na Wazanzibari una historia inayorudi nyuma kwa zaidi ya miaka milioni moja. Wataalamu wa ikolojia, katika maeneo ya Unguja Ukuu, Kae Pwani na Kae Bona, upande wa Unguja, vilevile Mtambwe Mkuu na Mkumbuu, Pemba, walipata kuonesha visiwa hivyo kukaliwa na watu miaka milioni moja iliyopita. Watu hao inasadikika kuwa walitoka Tanzania Bara.
Kitabu cha “Perilus of the Erythraen Sea” – “Safari ya Mwambao wa Bahari”, kilichoandikwa na Wagiriki wa Kale, kilionesha hivyo. Hiyo ndiyo sababu ya uwepo wa dhana kwamba watu wa Zanzibar, kwa sehemu kubwa walitokea Tanzania Bara. Waliingia visiwani kuanzisha maisha. Wareno na Waarabu walifuata baadaye. Wagunduzi wa visiwa vya Zanzibar ni watu kutoka Bara.
Historia hiyo inajenga muktadha wa uwepo wa undugu asilia. Inagusa maisha ya Rais wa Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi. Mei 8, 1925, Mwinyi alizaliwa Kivule, Mkuranga, Pwani, Tanganyika. Alipofikisha umri wa miaka minne, baba yake, Hassan Mwinyi, alimpeleka Mangapwani, Unguja, Zanzibar, akasome Quran.
Mangapwani, nyumbani kwa Swedi Mgeni, rafiki wa baba mzazi wa Mwinyi, ndiyo kwenye kitovu cha mchakato. Kusoma, kulelewa, kuanza kazi, hadi kupanda ngazi hatua kwa hatua kufikia kuwa Rais wa Tatu Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, juu zaidi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Huo ni ushahidi kuwa undugu wa Watanzania upo kabla ya Muungano. Rais wa Kwanza wa Zabzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, alipomteua Mwinyi mara ya kwanza kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, baadaye Mkurugenzi Msaidizi wa Chama cha Wakulima wa Karafuu (CGA), kilichokuwa moyo wa Uchumi wa Zanzibar, wala hakumuuliza asili yake, kwani Mwinyi alifanana na Wazanzibari wengine. Utamaduni unashabihiana.
Watanganyika na Wazanzibari ni ndugu. Undugu huu unapaswa kuenziwa na kulindwa. Viongozi, hasa wa kisiasa, wanapaswa kuchunga sana kauli zao.