Lusinde akemea ushabiki wa siasa

Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa (NEC), Livingston Lusinde akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika leo Jumapili Mei 28, 2023 katika viwanja vya Stendi kuu ya mabasi mjini Moshi.

Muktasari:

  • Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (NEC), Livingston Lusinde amewataka wananchi kuacha ushabiki wa kisiasa na kuwa wapenzi wa kisiasa ili kuweza kuchambua mambo kwa kina na kuyaona maendeleo yanayofanywa na Serikali.

Moshi. Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (NEC), Livingston Lusinde amewataka wananchi kuacha ushabiki wa kisiasa na kuwa wapenzi wa kisiasa ili kuweza kuchambua mambo kwa kina na kuyaona maendeleo yanayofanywa na Serikali.

 Lusinde ambaye ni Mbunge wa Mvumi, mkoani Dodoma ameyasema hayo, wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara, ulioandaliwa na Mbunge wa Moshi mjini, Priscus Tarimo na kufanyika katika viwanja vya stendi kuu ya mabasi mjini Moshi.

Amesema ushabiki wa kisiasa unafanya watu washindwe kutafakari mambo ya maendeleo kwa kina na kueleza ukweli wa yale ambayo yamekuwa yakifanywa katika maeneo mbalimbali nchini katika kuwaletea wananchi maendeleo.

"Ndugu zangu hasa vijana, ushabiki unampunguzia mtu uwezo wa kutafakari mambo kwa kina na kuna mambo hayahitaji ushabiki, mfano kwenye mpira unapokuwa shabiki unakuwa unapinga hata kama unaona goli lililofungwa ni nzuri utasema lilipita au ulitumika uchawi, lakini kama wewe ni mpenzi wa mpira utaueleza ukweli na kupongeza kazi nzuri ya wachezaji," amesema.

"Na ningependa kwenye siasa za Tanzania, ikiwezekana mwenyezi Mungu atujalie tuondoe ushabiki tuweke upenzi ili tuweze kuyachambua mambo kwa kina, kwani ukiweka ushabiki utakosoa lakini ukiwa mpenzi wa siasa utachambua, hapa CCM wamesema kweli, hapa Chadema wamesema kweli na hapa ACT Wazalendo wamesema kweli, hapa wamedanganya na hapa wamesema uwongo kwa sababu unatumia vizuri akili," amesema.


Ameongeza kuwa "Ukiondoa ushabiki kwenye siasa utayaona maendeleo, utaona kazi wanazofanya madiwani, Mbunge na viongozi wengine, niwapongeze Moshi kwa mara ya kwanza mliacha ushabiki na kuchagua kiongozi na leo mnaona kazi kubwa ambayo inafanywa na mbunge wenu Priscus Tarimo," amesema.

Ameongeza kuwa chama hicho hawana mpango wa kuliachia Jimbo la Moshi Mjini na kuwataka wananchi kuacha ushabiki wa kisiasa na kuendekea kukiamini chama hicho.

“Hapa Moshi nimetumwa na chama kueleza ya kuwa hili jimbo hatuachii ng’o, Meya hii halmashauri hatuachii, sisi tuna kazi za kufanya hapa, haiwezekani kuachia," amesema.

Aidha amesema Rais Samia Suluhu amewaagiza wao Wajumbe wa NEC kila watakapokwenda waziambie mamlaka za maji pamoja na watu wote wanaosimamia maji, maji siyo biashara bali ni huduma.

"Ndugu zangu maji ni ibada, maji ni maisha huwezi kuamka leo maji 2000 kesho 2,500, haiwezekani, kwani huduma ya maji sasa imegeuka kuwa biashara, Wizara ya Maji inatakiwa iangalie bei za maji na kuondoa watu kupandishiwa gharama hovyo".

Akizungumza kwenye mkutano huo, Mbunge wa Moshi Mjini, Priscus Tarimo amesema katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia wamepata fedha nyingi za maendeleo ambapo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi, wamepokea zaidi ya Sh6bilioni kwa ajili ya kukamilisha jengo la huduma za mama na mtoto.

“Lakini pia katika bajeti ijayo, tumepitisha Sh3 bilioni kwa ajili ya kujenga wodi za kisasa za ghorofa katika hospitali hiyo, ili ifanane na hospitali za mikoa zenye hadhi na kinachofuata ni kusimamia huduma, lakini pia kulikuwa na kilio cha muda mrefu cha hospitali ya wilaya, na sasa ujenzi umeanza pale ng’ambo, pia tunajenga kituo cha afya cha Msandaka.”

Akizungumzia sekta ya Elimu alisema pamoja na mambo mengi yaliyofanyika, wamejenga shule mpya ya sekondari katika eneo la Msandaka kwa gharama ya Sh570 milioni, na halmashauri imetenga Sh150 milioni kwa ajili ya mabweni ya shule hiyo ambapo pia wanakusudia kuyaweka kwa ajili ya kidato cha kwanza hadi cha nne katika Shule ya Sekondari Mawenzi.

“Tayari tumepata Sh5 bilioni kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa stendi ya kisasa ya mabasi ya Ngangamfumuni na kwenye uwanja wa ndege Moshi zimetoka Sh12 bilioni na kazi inaendelea,” amesema.

Akizungumzia tatizo la ajira alisema jitihada mbalimbali zinaendelea ikiwemo kufufua viwanda vilivyokufa pamoja na kupambania mipaka ya Manispaa ya Moshi kuongezwa ili kupata maeneo ya uwekezaji.

“Tatizo la ajira siyo tu kwamba ninapambana nalo kwa kufufua viwanda vilivyokufa, linafungamana moja kwa moja na ajenda ya kupanua Manispaa ya Moshi kuongeza mipaka, maana kwa sasa hakuna hata pa kujenga viwanda na maeneo mengine ya uwekezaji,” amesema.

“Leo dampo la Moshi mjini lipo Halmashauri ya Moshi, lakini pia eneo la makaburi limejaa, hivyo ninavyosema tunapambania Moshi mipaka iongezwe tunazo sababu za msingi, naomba Mnec kwenye vikao vyenu vikubwa ueleze kwetu siyo kuwa jiji kwa fahari  tunauhitaji kwa sababu ya mambo hayo na uwekezaji, pia maeneo tunayotaka kuyaingiza mjini yameendelea kujengwa kiholela,” amesema.

Kwa upande wake Meya wa Manispaa ya Moshi Zuberi Kidumo alisema katika kipindi cha miaka miwili ya Rais Samia, Manispaa hiyo wamepokea zaidi ya Sh21 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.