Prime
Lyimo achaguliwa mwenyekiti TLP, 21 wafutwa uanachama, wamkataa

Richard Lyimo (aliyevaa taji) baada ya kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa TLP Taifa
Muktasari:
- Lyimo achaguliwa mwenyekiti mpya TLP, wanachama 21 waliotimuliwa wakana kumtambua na wenzake wote waliochaguliwa huku wakidai wapo tayari kwenda mahakamani kudai haki, Naibu msajili awakingia kifua waliochaguliwa
Dar es Salaam. Wakati Chama cha Tanzania Labour Party (TLP) kikipata uongozi mpya, ikiwemo Mwenyekiti wa chama hicho, Richard Lyimo, sintofahamu imezuka kwa baadhi ya makada kudai hawaitambui safu hiyo.
Lyimo, aliyekuwa Katibu Mkuu, alichaguliwa kwa kunyooshewa vidole badala ya kupigiwa kura na wajumbe 84 wa chama hicho kushika wadhifa huo kwa miaka mitano ijayo. Kwa muda mrefu, Hamad Mkadamu alikuwa anakaimu nafasi hiyo baada ya Augustino Mrema kufariki dunia Agosti 21, 2022.
Viongozi wengine waliochaguliwa kupitia uchaguzi huo ni Johari Hamis (Makamu Mwenyekiti- Bara), na Hamad Mkadamu (Makamu Mwenyekiti –Zanzibar). Katibu Mkuu na manaibu wao watapatikana baadaye wiki ijayo.
Chama hicho, hadi kufikia hatua ya kufanya mkutano mkuu huo kwa mujibu wa katiba yao, kilikumbwa na changamoto, ambapo baadhi ya makada waliwahi kufanya mikutano mitatu ya kumpata mrithi wa Mrema, ikiwemo ule wa Julai 29, 2024, katika Ukumbi wa Ubungo Plaza, lakini yote ilikataliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa madai kuwa ilikosa sifa.
Katika mkutano wa leo, Jumapili, Februari 2, 2025, uliohudhuriwa na Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, ulitumia dakika 290, ukianza saa 4:30 asubuhi hadi saa 7:20 mchana. Wanaompinga Lyimo ni makada waliotimuliwa uanachama kupitia mkutano huo kwa madai kuwa ulikuwa batili na wagombea walipaswa kupitishwa na Halmashauri Kuu ya chama hicho.

Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TLP Taifa
Tofauti na vyama vingine kama Chadema na CCM, ambavyo viliendesha mikutano yao kwa siku mbili, TLP ilikamilisha uchaguzi wake ndani ya siku moja.
Wanaomuunga mkono Lyimo wanadai mkutano huo ni halali kwa kutoa sababu mbili, kwanza, umezingatia taratibu na katiba ya chama hicho na pili, hata Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kama mlezi, imeshiriki katika mchakato huo.
Wakati mvutano wa pande hizo mbili ukiendelea, Nyahoza amesema mkutano huo umezingatia vigezo, taratibu, na Katiba ya chama hicho, huku akisisitiza kuwa ofisi yake imeridhishwa na mchakato mzima na jinsi demokrasia ilivyotendeka.
“TLP mkutano wao umezingatia taratibu zote kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa na Kanuni za Usajili na Ufuatiliaji wa Vyama vya Siasa ya mwaka 2019. Chama cha siasa kinapotaka kufanya mkutano mkuu ni lazima kitoe taarifa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, na walifanya hivyo,” amesema.
Nyahoza, aliyegeuka mpiga picha wa baadhi ya matukio katika ukumbi wa uchaguzi huo, amesema kuwa chama kinapotoa taarifa, ofisi yake hujiridhisha kwa kuangalia kama wameitisha mkutano kwa kufuata utaratibu, ambapo anayeitisha anatakiwa kuwa anayetambuliwa kwa mujibu wa katiba ya chama hicho.

Richard Lyimo akishangilia ushindi wake pamoja na wanachama wa TLP
“Tunafanya hivyo kudhibiti vyama vya siasa kwa sababu vina watu wa aina nyingi. Kuna wanaoweza kuitisha mkutano huku wakijua jukumu hilo si lao. Kwa hiyo, tumejiridhisha kuwa mkutano huu umekidhi vigezo, na mchakato mzima wa kupata viongozi tumeridhika nao. Imetumika demokrasia ya wazi,” amesema Nyahoza.
Kuhusu wanaolalamikia mkutano huo, ikiwemo waliofukuzwa uanachama, kama wana hoja wawasilishe ofisini kwake kwa kuzingatia utaratibu atayasikiliza na kuyatolea majibu.
Wanaodai mkutano ulikuwa batili
Wanaodai hawautambui mkutano uliowachagua viongozi hao ni wale 21 waliofukuzwa kwa kauli moja na wajumbe wa mkutano huo kwa madai kuwa walihusika na kupanga njama ya kuandaa mikutano miwili kinyume na taratibu za chama hicho.
Miongoni mwa waliofukuzwa ni Dominata Rwechangura, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, na Ivan Maganza, aliyekuwa Mwenyekiti wa Vijana Taifa.
Wengine ni Mariam Kassim, Riziki Nganga, Stanley Ndumagoba, Mary Mwaipopo, Mohamed Mwinyi, Laurian Kazimiri, Nataria Shirima, Kinanzaro Mwanga, Godfrey Stivin, Rashid Amiri, Twaha Hassan, Tunu Kizigo, Damaly Richard, Hamad Alawi, Mohamed Hemed, Mariam Hamis, Mussa Fundi, Mwajuma Mussa, na Osward Nyoni.
Damaly amesema mkutano huo ni batili kwa sababu wajumbe wa mikoani, ambao ni sehemu ya Halmashauri Kuu ya chama hicho, hawakupewa taarifa, ilhali wao wana jukumu la kupitisha wagombea.
“Sasa Lyimo na wenzake walipitishwa na halmashauri ipi? Tumepanga kwenda mahakamani kuzuia uchaguzi huo kwani wajumbe wengi, hasa tunaoishi mikoani, hatukushiriki. Wamekusanya watu kutoka Dar es Salaam na kufanya mkutano,” amesema.
Maganza naye amesema uchaguzi huo hawautambui kwa sababu uchaguzi wa kumpata kiongozi wa chama ni lazima utangazwe hadharani siku 20 kabla ya kufanyika kwake, jambo ambalo halikufanyika.
“Jambo hili lina ukakasi, na kusema kweli hatuwatambui viongozi hao, kwani hata wajumbe walioshiriki si halali. Kuhusu kufukuzwa uanachama, tutafuatilia hatua za kudai haki zetu,” amesema.
Wanaomuunga mkono Lyimo
Wanamuunga mkono Lyimo wanadai mkutano huo umezingatia demokrasia na taratibu, tofauti na mikutano mitatu iliyofanyika awali ya kutaka kuziba nafasi ya Mrema, ambayo ilikuwa batili.
“Tusiwasikilize wanaongea sasa. Jambo kubwa tunapaswa kuungana na kujiandaa kwa uchaguzi mkuu ili tushike dola. Tuzibe masikio na tusiwasikilize wanaotaka kutugombanisha,” amesema Ester Pamagila.
Kuhusu waliotimuliwa, Lyimo amesema chama chochote kinaongozwa kwa mujibu wa taratibu na miiko yake. Mikutano waliyofanya ilikuwa batili, kwani walivunja sheria.
“Mkutano wowote ili ufanyike unatakiwa kuitishwa na Mwenyekiti, na Katibu Mkuu anatakiwa kufahamu wajumbe wanaopaswa kushiriki. Sasa mikutano yao ilikuwa batili, hata wajumbe walichukuliwa mtaani na kujaza ukumbi,” amesema.
Jicho la chama rafiki
Katibu Mkuu wa Chama cha Wakulima (AFP), Rashid Rai, amesema uchaguzi huo umekwenda vizuri, huku akisisitiza kuwa mara nyingi chaguzi za vyama zinafanywa kwa mujibu wa katiba zao.
“Kila chama kina katiba yake ya namna ya kupata viongozi. Kama waalikwa, kazi yetu ni kutazama na kusema uchaguzi ulikuwa mzuri kwa sababu hatujaona tofauti za kimawazo wala viashiria vya kasoro. Tofauti na chaguzi mbili tulizoalikwa, ambazo zilikuwa na vurugu,” amesema.
Mfumo wa uchaguzi
Wagombea wengi katika uchaguzi huo walipitishwa kwa kunyooshewa vidole kutokana na kukosa ushindani. Katiba ya chama hicho, toleo la mwaka 2009, inatoa ruhusa hiyo.
Katika hotuba yake, Lyimo amesema anakwenda kujipanga kuhakikisha katika uchaguzi ujao wanashinda nafasi za udiwani, ubunge, na urais.