Mahakama ilivyoulinda ubatili kwenye Katiba kuhusu mgombea binafsi

Kwa wasomaji wapya, leo naendelea na makala elimishi kuhusu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (JMT) kwa jicho la mtunga Katiba, alidhamiria nini wakati anaweka kifungu fulani.

Wiki iliyopita niliishia jinsi Mchungaji Christopher Mtikila (RIP) alivyofungua kesi ya kikatiba kupinga shurti la mgombea uongozi kudhaminiwa na chama cha siasa, akapewa ushindi na Mahakama Kuu kutamka kifungu hicho ni batili.

Mchungaji Mtikila, mwaka 1993, alifungua kesi Namba 5 ya mwaka 1993, alifanya juhudi kubwa kukipinga kifungu hiki na Mahakama Kuu kupitia kwa Jaji Lugakingira, (Mungu amuweke mahala pema peponi), ikatamka wazi kwamba kipengele hicho ni batili na kinakiuka Katiba ya JMT ya mwaka 1977, hivyo kifutwe na kutoa haki kwa kila Mtanzania kushiriki kugombea uongozi.

Serikali ilikata rufaa na wakati huohuo ikapeleka bungeni kwa hati ya dharura, sheria namba 34 ya mwaka 1994, kufanya marekebisho ya 8 ya Katiba ya JMT na kukichomeka kipengele hicho batili cha mgombea kudhaminiwa na chama cha siasa, ndani ya Katiba, hivyo kuibatilisha ile hukumu ya Jaji Lugakingira. Hapa ndipo ubatili wa kuinajisi katiba yetu ulipoanzia, Serikali yetu kuchomekea ubatili ndani ya Katiba yetu kiubatili.

Mchungaji Mtikila, licha ya kuwa ni mwanasiasa, mwenyekiti wa chama cha DP, lakini alikuwa ni mtu wa Mungu kiukweli, kwa sababu hakukubali Katiba yetu inajisiwe, hivyo akafungua kesi nyingine namba 10 ya mwaka 2009 kupinga marekebisho hayo ya 8 ya Katiba na kuyaita ni ubatili.

Katika kesi hiyo, Mchungaji Mtikila aliomba mambo mawili makuu; Mosi, Mahakama Kuu itamke ibara 39 na 67 za Katiba zilizorekebishwa na marekebisho ya 8 kwa sheria namba 34 ya mwaka 1994, ni batili na kinyume cha Katiba.

Pili, kutamka wazi kuwa kila Mtanzania ana haki ya kugombea kwa mujibu wa ibara ya 21 ya Katiba, bila kulazimishwa kudhaminiwa na chama cha siasa, hivyo mtu anaweza kugombea kama mgombea binafsi.

Mahakama Kuu chini ya majaji watatu (Half Bench), Jaji Amiri Manento, Jaji Salim Masati na Jaji Thomas Mihayo, wakayakubali mambo yote ya Mchungaji Mtikila na kumpa ushindi tena kwa kutamka marekebisho hayo ya 8 ya Katiba ya JMT ni batili, ibara za 39 na 67 ni batili, zifutwe toka kwenye vitabu vya sheria.

Lakini Serikali yetu, ikakata tena rufaa na safari hii ni Mahakama ya Rufaa ikakaa Full Bench (majaji saba), chini ya Jaji Mkuu mwenyewe, Jaji Agustino Ramadhani, akisaidiwa na majaji, Jaji Eusebio Munuo, Jaji January Msoffe, Jaji Natalia Kimaro, Jaji Salum Mbarouk, Jaji Benard Luanda na Jaji Mjasir ambapo Juni 17, 2010 ikatoa hukumu ya ajabu kabisa kuwahi kutokea Tanzania.

Tena Mahakama haikuwa peke yake, bali iliwaita mabingwa wabobezi wa sheria na Katiba kuisaidia, hawa wanaitwa marafiki wa Mahakama, kwa kiingereza ni “friends of the Court”, kisheria wanaitwa Amicus Curiae, hivyo ma Amicus Curiae hawa walikuwa ni Othman Masoud Othman, Profesa Palamagamba Kabudi na Profesa Jwan Mwaikusa (Mungu aiweke roho yake mahala pema peponi).

Mahakama ya Rufaa uliamua kitu cha ajabu sana.

Dhima ya mtunga katiba aliposema Katiba ni sheria mama na sheria nyingine yoyote inayokwenda kinyume cha Katiba ni batili, mtunga Katiba alidhamiria hakuna mamlaka yoyote ndani ya JMT, inaruhusiwa kutunga sheria yoyote inayokwenda kinyume cha Katiba na ikitokea sheria hiyo ikatungwa, mtunga Katiba alidhamiria sheria hiyo ni batili.

Anayebatilisha sheria batili inayokwenda kinyume cha Katiba ya JMT kwa dhima ya mtunga Katiba, ni Katiba yenyewe na sio Mahakama Kuu ya Tanzania. Jukumu la Mahakama Kuu kwenye ukuu wa Katiba, ni kujiridhisha tu na kuthibitisha kuwa sheria fulani inakwenda kinyume cha Katiba.

Hivyo, uamuzi wa Mahakama Kuu ni kuuthibisha na kuutangaza ubatili wa kwenda kinyume cha Katiba, na sio kuibatilisha. Anayebatilisha sheria batili inayokwenda kinyume cha Katiba ni katiba yenyewe na sio Mahakama Kuu.

Serikali, Bunge na Mahakama zina wajibu wa kuheshimiana, Mahakama ikitoa hukumu, Bunge na serikali zinapaswa kwanza kutekeleza hukumu husika, ndipo taratibu za kukata rufaa ziendelee, lakini kwa mujibu wa Katiba ya JMT, dhima ya mtunga Katiba ni sheria yoyote batili, sio sheria, kwa lugha ya kisheria ni “void ab initio”, yaani haipo.

Toka Mahakama Kuu ilipotoa uamuzi wa ubatili huo, ubatili huo unakuwa umebatilika palepale, hivyo serikali haikupaswa kukata rufaa, lakini serikali yetu ilikata rufaa na wakati huohuo serikali ilipeleka bungeni kwa hati ya dharura, sheria namba 34 ya mwaka 1994, kufanya marekebisho ya 8 ya Katiba ya JMT na kukichomeka kipengele hicho cha mgombea kudhaminiwa na chama cha siasa, ndani ya Katiba.

Hivyo, hiyo ilibatilisha ile hukumu ya Jaji Lugakingira. Hapa ndipo ubatili wa kuinajisi Katiba yetu ulipoanzia. Serikali ililinda ubatili.