Mazingira yanamuunga mkono Mbowe kukataa kuungana na vyama vya siasa

Ukifungua juzuu zote za sayansi ya siasa, zinatoa mwongozo kuhusu muungano wa vyama. Wakati ambao hushawishi kuungana na kujenga agenda ya pamoja.

Mosi, vyama huungana ili kuunganisha nguvu kwa ajili ya uchaguzi. Tanzania, uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni mwakani. Joto la uchaguzi halijafika mahali pa kuunguza vyama kiasi cha kushawishi kusaka nguvu ya pembeni.

Pili, vyama huungana kwa ajili ya kuunda serikali baada ya uchaguzi. Kwamba uchaguzi umepita, matokeo yanalazimisha vyama kuungana kuunda Serikali ili kutimiza matakwa ya kikatiba. CCM ina kila kitu mbele ya dola. Haihitaji ushirikiano.

Zanzibar, CCM na ACT-Wazalendo, wanaunda serikali. Sio ushirikiano wa vyama, bali mwafaka wa kikatiba, unaotaka mgawanyo wa madaraka kulingana na asilimia za kura kwenye uchaguzi. CCM na ACT walifuzu vigezo vya kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Upande wa Jamhuri ya Muungano, CCM wanajidai kwa mamlaka yao yaliyotimia. Hawahitaji kuungwa mkono na chama chochote ili kuendesha serikali wala kufanikisha kupitisha agenda zao bungeni. Wanajitosheleza.

Isitoshe, mara nyingi muungano baada ya uchaguzi huzihusu zaidi nchi zenye kufuata serikali za kibunge (parliamentary democracy), kwamba vyama vinaungana kwa lengo kupata idadi nzuri ya wabunge ili kupata uhalali wa kuongoza serikali.

Tanzania imeshika mfumo wa nusu urais (semi presidential system). Rais akishinda, anateua waziri mkuu miongoni mwa wabunge wa kuchaguliwa kutoka kwenye chama kinachoongoza kwa idadi bungeni.

Tatu, upo ushirikiano ambao vyama vya upinzani huungana na chama kinachoongoza dola, lengo likiwa kuiunga mkono serikali iliyo madarakani. Je, vyama vya upinzani vipo tayari kugeuka kwaya ya mapambio ya CCM kwa sasa?

Katika zama hizi, mwanasiasa wa upinzani akimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kutengeneza mazingira bora ya kufanya siasa nchini anaitwa chawa, au amelambishwa sukari, je, wapinzani wapo tayari kuziishi presha za kuitwa majina mabaya?

Tabia za kisiasa nchini hazitoi upendeleo wa kimazingira kwa vyama kuungana ili kuiunga mkono Serikali. Kufanya hivyo, itakuwa sawa na kujiua. Siasa za nchi huvipa uhalali vyama vya upinzani pale vinapokuwa vinaibua hoja na kusimamia agenda kinzani dhidi ya Serikali na chama tawala.

Nne, upo ushirikiano wa vyama kwa ajili ya uchaguzi wa marudio. Katiba ya nchi inataka mshindi wa urais atangazwe baada ya kupata asilimia 50 jumlisha moja ya kura. Wagombea wawili wa juu hakuna aliyevuka 50. Inabidi kurudia uchaguzi kumpata ambaye atafikisha 50 jumlisha moja.

Hapo wagombea wawili wa juu na vyama vyao, huunganisha nguvu na wagombea walioshindwa ili kusaka kura za kuwezesha ushindi katika uchaguzi wa duru ya pili (runoff). Katiba ya Tanzania haisemi 50 jumlisha moja. Inataka aliyeongoza kwa kura atangazwe. Zaidi nchi haipo kwenye uchaguzi.

Tano, vyama vya siasa vinaweza kuungana kwa ajili ya kushirikiana kusukuma agenda ya pamoja. Mathalan, ilitokea mwaka 2014, ulipoundwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa). Msukumo ulikuwa kutetea rasimu iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Sita, vyama vya upinzani vinaweza kuungana kwa ajili ya kuipinga serikali inayotaka kuipeleka nchi vitani. Katika muktadha huu, vyama pia vinaweza kuungana kwa ajili kupinga sera ambazo vinaona zinaipeleka nchi shimoni.

Saba, muungano wa upinzani unaweza kuchochewa na uchagizaji wa mabadiliko ya sheria za uchaguzi. Maana vyote vina masilahi na uchaguzi.
Mwaka jana, vyama 17 vya upinzani Cambodia, vilifanya mazungumzo ya kuungana ili kushinikiza serikali kubadili sheria za uchaguzi. Inawezekana pia kuungana ili kushinikiza kupatikana kwa tume huru ya uchaguzi.

Kauli ya Freeman Mbowe
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, amesema kuwa hivi sasa chama chake kitaendesha mapambano ya kidemokrasia kwa kuunganisha wanachama na sio kuungana na vyama vingine.
Kauli hiyo imekosol…