Mbowe aeleza ukimya mazungumzo Serikali, CCM, asema…

Rais Samia Suluhu Hassan akiongoza kikao cha majadiliano kilichohusisha viongozi wa CCM, Chadema na Serikali Ikulu Chamwino Jijini Dodoma. Picha na Maktaba

Muktasari:

Mbowe amesema anasikitishwa na watu wanaomtuhumu kwamba amelamba asali kutokana ukimya wake kuhusu mazungumzo kati ya chama hicho na Serikali yaliyoanza Mei 20 mwaka katika Ikulu ya Chamwino Jijini Dodoma.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amesema anasikitishwa na watu wanaomtuhumu amelamba asali kutokana na ukimya wake kuhusu mwenendo wa mazungumzo kati ya Serikali, Chama cha Mapinduzi (CCM) na chama hicho.

Kauli imekuja ikiwa imepita wiki chache tangu Makamu mwenyekiti wa Chadema, bara Tundu Lissu kueleza chama hicho, kitaamua kama kiendelee mazungumzo na CCM au la ifikapo mwezi huu kwa madai mambo mengi wanayolalamikia hayatekelezwi.


Majadiliano kati ya Chadema na viongozi wa Serikali na CCM yalianza Mei 20, 2022 Ikulu ya Chamwino Dodoma, kwa Rais Samia Suluhu Hassan akiambatana na viongozi waandamizi waliokutana na ujumbe wa viongozi wa Chadema, ulioongozwa na Mbowe.


Hata hivyo, baadhi ya Wanachadema kwa nyakati tofauti wamekuwa wakisikika na kuandika katika mitandao ya kijamii wakida kwamba hawaridhishwi na mwenendo wa majadiliano hasa la masual ya mikutano ya hadhara na wabunge 19 ambayo hayapatiwa ufumbuzi na kushauri Chadema kujiondoa.


“Nimekuwa mfuatiliaji wa mijadala katika mitandao, hisia za viongozi wenzangu ndani ya chama na Watanzania wasio Wanachadema. Wengi wakiamini maridhiano haya ni kupoteza muda Ukatokea msamiati kwamba Mbowe amelamba asali inaniudhi…


“Mbona Mbowe azungumzi, amekuwa kimya sasa leo nataka nizungumzie hili na kuweka rekodi sawa. Mbowe kalamba asali lakini inabidi nikubali kwamba kama kulamba asali ni kuitetea Tanzania basi nitaendelea kuitetea,” amesema Mbowe.


Mbowe ambaye ni kiongozi wa zamani wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni (KUB), ameleeleza hayo usiku wa kuamkia Desemba 11, 2022 wakati akizungumza na wanadaispora wa Marekani Jijini Washington D.C. Mbowe yupo Marekani kwa ziara maalumu ya kikazi.


Mbowe ambaye ni mwenyekiti mwenza wa Umoja wa Vyama vya Demokrasia Afrika (DUA), amefafanua kwamba chama anachokiongoza amekiruhusu kusema na hataki Chadema ionekana akizungumza mwenyekiti basi viongozi wengine wakae kimya.


“Anaweza kutoka makamu wangu Lissu (Tundu), akasema na ukimsikiliza unaweza kusema Mbowe na Lissu wana ugomvi, lakini kumbukeni yule alipigwa risasi 16. Hawa ni viongozi wenzangu wana uchungu na waliofungwa jela na kuhamishwa nchi, wanaishi ughaibuni kwa nguvu sio kwa kupenda,” amesema


“Niliwahi kumwambia Rais Samia kwamba namsaidia kumkinga na mizinga na mishale ya Chadema ili kurekebisha kesho yetu iwe bora zaidi,” amesema Mbowe.


Hata hivyo, Mbowe amesema Chadema haitajitoa katika mazungumzo hayo, akisema baadhi ya mambo yanakwenda vizuri hasa mchakato wa kufufua Katiba Mpya.


“Wakati tunaanza mazungumzo, Rais na CCM hawakutaka kusikia Katiba mpya, lakini tuliwapelekea hoja yenye ngazi nne kuhusu ulazima Serikali na CCM kuona umuhimu wa Taifa kuhitaji Katiba mpya.


“Ilituchukua miezi kuwambembeleza CCM kubadilisha msimamo kwamba Katiba hadi baada ya mwaka 2025 na kukubali kujadili, halafu mtu anakwambia maridhiano hayana faida mnanichanganya,”amesema Mbowe.


Mbowe amesema CCM walikubali kuhusu mchakato wa Katiba kupitia vikao vyao vya juu vikiongozwa na mwenyekiti wao Rais Samia. Kiongozi huyo ameshangaa wanaosema hakuna mafanikio katika mchakato huo.


“Mnataka mafanikio ya aina gani kaka na dada zangu? Tumevuka hatua ya kwanza ya muhimu kuliko zote, kwamba sasa tunajadili Katiba, lakini kuna mtu anakwambia mikutano ya hadhara haijaruhusiwa, Mbowe toka katika mazungumzo au hadi leo Serikali haijawaondoa wabunge 19 inatosha tujitoe hapana, tupo katika maridhiano sio kwa sababu ya Chadema au CCM bali kwa Taifa.


"Haiwezekani eti mkutano ya hadhara imekatiliwa basi tuache yote ikiwemo Katiba, hata tukose mengi yote lakini tuweze kujadili Katiba mimi nitasimama kwenye hili. Sio kwamba CCM ni watu, hawajahi kuwa wema kwangu na chama changu, lakini unabakia ni sehemu ya jamii ya Watanzania iwe mbaya au nzuri,”amesema Mbowe.