Mbowe kuongoza mkutano wa hadhara kumkaribisha Wenje

Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe.

Dar es Salaam. Viongozi wakuu wa Chadema wakiongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho Taifa Freeman Mbowe, wanatarajia kuhutubia katika mkutano wa hadhara utakaofanyika Machi 14, katika viwanja vya Obwere Rorya.

Mkutano huo ulioandaliwa kwa ajili ya kumkaribisha aliyekuwa mgombea ubunge Jimbo la Rorya katika Uchaguzi Mkuu 2020 Ezekia Wenje, utahudhuriwa pia ni viongozi mbalimbali wakiwemo wabunge na wabunge na Gavana kutoka Kenya.

Wenje ambaye ni mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Victoria, aliondoka nchini na kwenda kuishi uhamishoni baada ya uchaguzi mkuu 2020, akihofia usalama wake.

Taarifa kutoka ndani ya chama imeeleza kuwa mbali na Mbowe viongozi wengine watakaohudhuria ni Katibu Mkuu John Mnyika na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu.

Kwa upande wa viongozi kutoka Kenya watakaoshiriki ni Gavana wa Kaunti ya Homaby, Cladys Wanga, Mbunge wa Rarieda, Otiende Amolo na Mbunge wa Suba, Kusini Caroli Amond.

Aidha katika taarifa hiyo pia imeeleza kuwa Machi 15, Mbowe ataendelea na mikutano ya hadhara ambapo atafanya mkutano mwingine Jimbo la Serengreti, akiambatana na viongozi mbalimbali.

Mikutano hiyo ni mwendelezo wa mikutano ya hadhara, inayofanywa na vyama mbalimbali tangu Rais Samia Suluhu Hassan alipoondoa zuio la mikutano kwa vyama vya siasa.