Mbowe: Viongozi wote nchini wachaguliwe na wananchi

Muktasari:

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema mabadiliko ya Katiba ni lazima ili kubadilisha mfumo wa utawala utakaoruhusu viongozi wote kuchaguliwa na wananchi.


Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema mabadiliko ya Katiba ni lazima ili kubadilisha mfumo wa utawala utakaoruhusu viongozi wote kuchaguliwa na wananchi.

Alisema lengo ni kuwa na viongozi wanaojali wananchi ili kupeleka madaraka katika Serikali ya wananchi na wawe huru kuamua hatima ya maisha yao.

“Katika nchi za wenzetu kama Kenya hakuna kiongozi wa Serikali asiyetokana na kura za wananchi, iwe gavana anachaguliwa na wananchi. Ndio maana tunasema katika mabadiliko ya msingi ya sera zetu, lazima viongozi wote watokane na kura za wananchi,” alisema Mbowe ambaye ni kiongozi wa zamani wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni (KUB).

Mbowe alisema hayo jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Sumbawanga mkoani Rukwa ikiwa ni mwendelezo wa mikutano hiyo, baada ya kusimama kwa siku kadhaa tangu ilipozinduliwa Mwanza na Mara mwezi uliopita.

Alisema wakati wa ukoloni Malkia wa Uingereza, alikuwa anateua gavana ili kuongoza Tanganyika na kulinda masilahi ya malkia huyo, lakini hivi sasa kuna wakuu wa mikoa nchi nzima, huku akihoji wanawakilisha masilahi ya nani.

“Wakuu wa wilaya wanasimamia masilahi ya nani? Haya mambo ya ajabu, tuna mifumo ya utaratibu wa uchaguzi, wanachaguliwa viongozi lakini hawana mamlaka, lakini wale wanaoteuliwa na Rais wana mamlaka,” alisema.

Mbowe alisema Chadema inataka Katiba ibadilishwe ili viongozi wote watakaongoza wananchi watokane na kura za wananchi.

Alisema Chadema inataka Katiba bora itakayohakikisha utawala wa sheria unaheshimika ndani ya Taifa ili kila mwananchi tajiri au masikini awe na uhuru ndani ya nchi.

“Tunataka Taifa la haki katika Mahakama na uchaguzi ili nchi itawaliwe na maandiko yanasema, haki huinua Taifa. Lakini tunataka chama cha kujenga demokrasia ili wananchi wachague viongozi wanaowahitaji,” alisema Mbowe.

Alisema Chadema itafanya operesheni nchi nzima usiku na mchana kwa sababu wamepania kuleta uhuru wa kweli.

Katibu Mkuu wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), Catherine Ruge alisema bado kuna changamoto katika upatikanaji wa mbolea ya ruzuku kwa kuwa haipatikani kwa wakati kama Serikali inavyotangaza.

Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa, Mchungaji Peter Msigwa alisema miaka 16 iliyopita kanda hiyo ilikuwa inatoa asilimia 75 ya mahindi, akisema mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe, Songwe na Rukwa ndio kapu la kuilisha Tanzania.