Mshindi CCM: Nimeokota dodo kwenye mpilipili

Mwenyekiti mpya wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa, Fadhil Maganya akiwashukuru wajumbe wa mkutano Mkuu wa Jumuiya hiyo kwa kumchagua. Picha Ramadhan Hassan

Muktasari:

Mwenyekiti mpya wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Fadhil Maganya amesema hakutegemea kupata ushindi ni sawa na 'ameokota dodo katika mti wa mpilipili.'

Dodoma. Mwenyekiti mpya wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Fadhil Maganya amesema hakutegemea kupata ushindi ni sawa na 'ameokota dodo katika mti wa mpilipili.'

  

Maganya aliibuka kidedea katika uchaguzi wa Jumuiya ya Wazazi uliofanyika jana jijini Dodoma na kupata kura 578 kati ya 835 akiwashinda wagombea wengine saba akiwemo Mwenyekiti aliyepita Dk Edmund Mndolwa.


Akizungumza baada ya kuchaguliwa, Mwenyekiti huyo katika uchaguzi uliomalizika usiku wa kuamkia leo Ijumaa, Novemba 245, 2022 amesema wajumbe wamemheshimisha kwa kumpigia kura kwani hakutegemea kupata ushindi.


"Ndugu wajumbe mimi nimewiwa,nimehemewa,kwa namna ambavyo nimepigiwa kura mmenipa heshima kwa kweli mmefanya maajabu na wajumbe wa wazazi mmevunja rekodi.


"Wanasema wajumbe hawafai lakini leo mmefaa mmetengeneza historia.Ndugu zangu nitakuwa mchovu wa fadhila kama nisiposema nimeokota dodo katika mti wa mpilipili sikutegemea,mimi sina jina lakini nimeshinda," amesema Mwenyekiti huyo.


Mwenyekiti huyo amesema ushindi huo sio wake bali ni wajumbe walimpigia kura na viongozi wote.


"Kura mlizonipa mpaka zikajaa kwakweli zinanisukima mimi kulipa deni na lazima niwalipe mimi kwanza nikishukuru Chama Cha Mapinduzi na Mwenyekiti wetu nani alikuwa ananifahamu mimi," amesema.


Amesema uchaguzi huo umetengeneza historia kwani yeye amepata uenyekiti kwa hisani ya wajumbe kwa kuamua kumchagua kwani hajawahi kufanya kazi popote.


Amewataka wanachama wa CCM kumtumia kwani hajawahi kutumika mahali popote yupo fresh.


"Mimi sijawahi kutumika mahala popote sio Serikali wala katika Chama cha Mapinduzi nimekuja nikiwa fresh,"amesema Mwenyekiti huyo huku wajumbe wakishangilia.


Aidha, amesema atawashangaza kwani anataka kuinyanyua Jumuiya kwa kiwango cha juu.


Amesema atatoa ushirikiano kwa Mwenyekiti wa Chama Samia Suluhu Hassan kuhakikisha mambo yanaenda vizuri.


"Namwambia Mama kwamba atapata ushirikiano nitampa sapoti na ataendelea kuupiga mwingi anaetaka kufa na afe,"amesema.