Rais Samia akikosolewa isiwe dhambi, akisifiwa isiwe kero

Aprili 8, 2013 alifariki dunia Waziri Mkuu wa zamani wa United Kingdom (UK), Margaret Thatcher. Vyombo vingi vya habari vilimpamba. Vingine vilimponda tu kuwa alikuwa mtu mwovu. Kila chombo kilichagua upande wake wa kusimamia.

Taaluma ya habari UK ilikosolewa kwa vyombo vya vingi kukusanya habari na kuripoti kwa kujenga mitazamo badala ya kupasua katikati ya ukweli bila hisia.

Gazeti la The Northern Echo lilipata heshima kubwa kwa kuandika kichwa cha habari; Alipendwa, alichukiwa, kamwe hatasahaulika.

The Northern Echo lilipata heshima kwa sababu lilipita katikati. Kwamba Thatcher alipendwa na alichukiwa, kamwe hatasaulika. Ni gazeti lililoamua kuandika habari kwa ulinganifu. Huwezi kusema “fulani alikuwa mwovu” au “alikuwa mwema tu”. Binadamu hakamiliki.

Ukienda Uganda, mpaka leo utakuta kuna watu wanamzungumzia vizuri Idi Amin Dada. Dunia ina picha mbaya kuhusu Amin. Na kwa hakika, Watanzania hawapaswi kumpenda Amin kwa hasara kubwa ambayo aliwasababishia katika Vita ya Kagera.

Ndivyo ilivyo kwa Mobutu Sese Seko, mpaka leo kuna Wakongo wanamlilia. Kadhalika Adolf Hitler kwa baadhi ya Wajerumani na Joseph Stalin Urusi. Ni vigumu kuchukiwa na wote. Haiwezekani ukawa na mabaya tu lisiwepo jema.

Kutoka Thatcher, Amin hadi Mobutu na Hitler, kisha malizia Stalin. Unapaswa kushika hili; binadamu anabaki kuwa binadamu na hajawahi kuwa na ukamilifu. Zaidi, hakuna binadamu mwenye kipeo cha pili hata huitwa robo au nusu ya malaika.

Mwalimu Julius Nyerere ni Baba wa Taifa la Tanzania. Kwa vipimo vingi, dhahiri hakuna Mtanzania ambaye amepata kupendwa na kuheshimiwa kwenye ardhi ya Tanganyika na Zanzibar kuliko Mwalimu. Hata hivyo, kuna ambao hawampendi na hawakupata kumwelewa.

Inapaswa kufahamika kuwa kamwe hutapendwa na wote. Isipokuwa upo mzani. Mathalan, makosa machache ya Mwalimu Nyerere ambayo husemwa na wasiomkubali au kutomwelewa, yamezidiwa na mema mengi aliyoyatenda. Ndiyo maana ni Baba wa Taifa na sio malaika wa Taifa.

Mfano huo, unatusogeza kwa Rais Samia Suluhu Hassan. Tangu ameshika madaraka, matendo yake ya kiuongozi wengi wanayafurahia, kuna wasioyapenda na hawamwelewi kabisa. Hayupo binadamu wa kupendwa na wote.

Machi 17, 2021, taifa lilipotangaziwa kifo cha Rais wa Tano, Dk John Magufuli, kuna vyombo vilikuwa ‘subjective’ mpaka kumwita “shujaa wa Afrika”. Wengine waliingia maktaba kutafuta nyaraka zenye kuthibitisha uhalali wa kumwita Magufuli shujaa wa Afrika na hawakuona.

Hata kelele za sasa za “never again” - “kamwe isijirudie”, zinamhusu Magufuli. Kwamba vitendo vyake vya kiuongozi vilikiuka mno haki za binadamu na wanataka asitokee tena kiongozi aina yake kuiongoza nchi. Wakati huohuo, kuna wanaoamini kwamba nchi tangu imepata uhuru, Magufuli amewazidi marais wote kwa ubora.


Tujadili kwa usawa

Anayesema Magufuli ni bora kuliko wengine wote anatumia vigezo gani? Kuna anayesema ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere (JNHPP), bila kujali kuwa Rais Samia, amefanikisha kwa sehemu kubwa JNHPP kuliko Magufuli.

Mwingine atataja reli ya Standard Gauge (SGR), hawezi kuelewa kitu kwamba Samia aliikuta imekamilika kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro, lakini sasa inakwenda Kigoma.

Wapo walimpenda Magufuli kwa sababu aliuahidi umma kuwa “waliokuwa wanaishi kama malaika, wataishi kama shetani”. Kwa Mtanzania asiyebebwa na ushabiki wa upande, aliona matamshi hayo ya Rais, yalijaa kisasi.

Kesi nyingi za uhujumu uchumi zikapelekwa mahakamani pasipo upelelezi kukamilika. Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka ya Umma (DPP), ikawa idara mpya ya mapato. Watuhumiwa wakatakiwa kulipa fedha kwa mpango wa makubaliano ya msamaha wa jinai (plea burgain).

Mtindo huo wa DPP kukusanya fedha za watuhumiwa, ulikosolewa kwamba ulikiuka utawala wa sheria kwa kuwaingiza watu kwenye kona ambayo, walijikuta hawana namna ya kupata uhuru bila ya kuununua. Wapo Watanzania walipenda hali hiyo.

Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, mara kwa mara alirejea kutaka ofisi ya DPP ichunguzwe kutokana na makusanyo ya plea burgain.

Kisha, Rais Samia akafichua kwamba kuna fedha zilifichwa kwenye akaunti China. Kuna wanaoona suala la plea burgain linaibuliwa kuchafua heshima ya uongozi wa Magufuli.

Binadamu anapokuwa na upande au kuendeshwa na hisia hukosa usawa. Ukweli ataupinga na uongo ataukumbatia. Huchagua yale yenye kumliwaza na kuyapiga teke yanayomkwaza. Bahati mbaya dunia imejaa binadamu wa aina hii.

Katika saikolojia kuna ugonjwa unaitwa “stockholm syndrome”, wenye tafsiri ya watu ambao ni mateka kifikra. Wagonjwa wa stockholm syndrome, hujikuta wanawapenda watu katili na wanaotesa watu, ikiwemo wao wenyewe.

Mathalan, tukio la Tundu Lissu kupigwa risasi Septemba 7, 2017, ulikuwa unyama ambao kila Mtanzania alipaswa kuupiga vita. Hata hivyo, kulikuwa na Watanzania waliotokeza hadharani na kuombea Lissu afe. Yupo aliita waandishi wa habari na kutishia kumfuata Ubelgiji kummalizia.

Mitazamo huharibu usawa. Dunia haijabadilika tangu Amin, alipowashurutisha Wazungu wambebe mithili ya chifu wa zamani, na kama ambavyo Wakoloni walibebwa na Waafrika kwa shuruti, hususan nyakati za mwanzo za uvamizi wa Bara la Afrika.

Yupo mtu haambiwi kitu kuhusu Amin kwa sababu alibebwa na Wazungu. Wengine walikosoa kitendo hicho kwa sababu kilikosa utu. Wakoloni walokosea na vitendo vyao vililaaniwa.

Amin alichofanya ni kulipiza kisasi kwa watu ambao si wao walitenda. Kosa la Mzungu wa kale, alilipa wa vizazi vya baadaye. Makosa mawili hayasahihishi muktadha.


Si wote wanampenda Samia

Unaposema kwenye uongozi wake, pamoja na kusifiwa kwa kufanya mageuzi makubwa, lakini si wote wanampenda Samia, yupo mtu kichwani anamwaza Dk Bashiru Ally, alipoondolewa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi, na kupelekwa bungeni kuhudumia kama mbunge wa benchi la nyuma.

Mwingine anamwaza Lengai ole Sabaya ambaye yupo mahabusu hivi sasa, huku akiandamwa na kesi lukuki za unyang’anyi wa kutumia nguvu. Makosa anayodaiwa kuyafanya kipindi alipokuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai.

William Lukuvi, Profesa Palamagamba Kabudi, Medard Kalemani, Profesa Kitila Mkumbo na Geofrey Mwambe, walikutwa Baraza la Mawaziri, lakini Samia aliwatoa. Wapo watu ambao kwa hisia zao wanaamini kwamba mawaziri hao wa zamani hawamwelewi rais huyo wa sasa.

Ninapojenga mtazamo wa watu kutomwelewa Rais Samia, sitazami masilahi au upendeleo wa mtu mmoja-mmoja. Hoja inajengwa kwa kupitia aina ya uongozi wake, matokeo anayoyatengeneza na mapokeo ya watu.

Hivi sasa, siasa zipo shwari, malalamiko ya muda mrefu ya dhuluma kwenye mchakato wa haki jinai, Rais Samia ameyaundia tume. Wafanyabiashara wanakiri mazingira ni nafuu kuliko zamani. Hata hivyo, wapo walitamani chuki za siasa ziendelee, uonevu kwenye jinai ubaki vilevile na wafanyabiashara wapitie mateso.

Si binadamu wote, milango yao ya fahamu ina zawadi ya “moral compass”, yaani uwezo wa kupokea kwa usahihi, kuchanganua vema na kutenda inavyotakiwa. Wapo ambao hawana kabisa au moral compass zao zimeshaelemewa na rushwa ya fikra. Hawawezi kujenga mtazamo bora.

Wafanyabiashara wenye maduka ya kubadilishia fedha walinyang’anywa mpaka mitaji yao, Rais Samia amewarejeshea fedha zao. Hapohapo, kuna wanaokebehi hilo na wanaahidi kwamba sarafu za kigeni hasa dola zitapaa na Shilingi itaanguka. Wanaamini Magufuli alikuwa sahihi.

Wapo wasiomwelewa Rais Samia kwa sababu wanaona maisha ni magumu. Bei za bidhaa zimepaa. Hawakubaliani na ukweli kwamba uchumi wa dunia upo vibaya. Mfumuko wa bei unaitesa Ulaya yote na hata Marekani.

Rais Samia ameshatimiza miaka miwili madarakani. Hivyo, si wote wenye kufurahia urais wake. Mitazamo ni tofauti. Hata alipoahidi kuwa nchi itapata Katiba mpya, kuna ambao walihoji; Katiba ndio itashusha bei za bidhaa? Kufanya maridhiano na wapinzani kumemaliza tatizo la maji mpaka vijijini?

Tanzania ipo kwenye maelewano na jumuiya za kimataifa. Hakuna matukio ya kufungiana mipaka na majirani wala kuchoma vifaranga. Kuna wasiolikubali hata hilo. Wapo waliomkosoa Rais Samia kwa kuvaa tu ushungi. Isisahaulike, kuna yule hatakupenda, akiulizwa sababu atajibu; basi tu simpendi.

Mwingine kila siku anasonya Samia kuwa Rais kwa sababu ni mwanamke. Mtazamo wake umelemazwa kwamba nchi kuongozwa na mwanamke ni makosa makubwa hata kama yeye mwenyewe ana jinsia ya kike.

Yupo asiyetaka Samia akosolewe kwa chochote kwa kuwa ni mwanamke. Basi tu nafsi yake inasuuzika nchi kuwa ina Rais mwanamke.

Kinachopaswa kuangaliwa ni usahihi wa kumsifu na kumkosoa. Asitokee mwenye kumchukia au kumpenda kwa sababu ya dini yake, hiyo ni dhambi kubwa mbele ya misingi iliyoliasisi na kulilea taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mathalan, kumkosoa Rais Samia kwa kuvaa ushungi na kumlazimisha akae kichwa wazi, ulikuwa mtazamo wa hovyo sawa na udini. Vilevile ni haramu kumpenda Rais Samia au kumchukia kwa sababu ni Mzanzibari. Tanzania ni moja na kila Mtanzania ana haki ya kuongoza nchi kama matakwa ya Katiba yametimizwa.

Wapo wanamkosoa Rais Samia kuwa anakumbatia mataifa ya Magharibi. Wanaamini nchi hizo ni wanyonyaji. Wengine wanapenda kuwa na ushirikiano mwema na jumuiya za kimataifa kwa sababu Tanzania sio kijiji. Kuna wasiopenda Rais kusafiri na wanaopenda anavyopasua mawingu kwa ajili ya kusaka fursa za kiuchumi.

Ifahamike kuwa Watanzania sio hayo makundi mawili, ya wenye kumkubali na kutomkubali Rais Samia, bali wengine hawajui kama wanampenda au hawampendi, wapo katikati. Ni hali ya binadamu. Muhimu ni usahihi wa kile anachokisimamia.