Sababu nne Chadema kuendelea kuimarika

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ataja misingi minne ikiwemo ya haki na uhuru wa watu akisema ndiyo inayoifanya chama hicho kuwa imara na kutotetereka.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe chama hicho, kimejengwa kwa msingi wa mambo manne ikiwemo misingi ya haki na uhuru wa watu, akisema ni vigumu kukiua au kukidhoofisha.

Mbowe ambaye ni mbunge wa zamani wa Hai mkoani Kilimanjaro, ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Agosti 28,2023 wakati akihutubia katika mkutano wa hadhara wilayani Kishapu mkoani Shinyanga.

Kabla ya kutoa kauli hiyo, Mbowe amedai utawala uliopita, ulijaribu kuviua vyama vya upinzani kiwemo Chadema, lakini ilishindikana kwa namna chama hicho, kilivyojipanga na kuenea katika kila kijiji cha Taifa hili.

“Chadema tuna misingi ya haki kwa wakulima, wafanyabiashara, wafanyakazi wa umma walimu, mahakamani na katika mchakato wa uchaguzi. Taifa lenye haki ndio Taifa la Mungu.

“Msingi mwingine Chadema tunaamini katika uhuru wa watu, tunataka kuhakikisha uhuru na maisha mwananchi yawe katika mikono yao siyo mikononi mwa Rais ambaye anakuwa na madaraka makubwa kama ilivyosasa ana mamlaka ya kumteua kila,” amesema Mbowe.

Katika mkutano huo, Mbowe alikumbushia machungu ya miaka saba ya zuio la mikutano ya hadhara, akisema ilikuwa migumu ndiyo maana hivi sasa chama hicho kinapigania umuhimu wa kuwa na Katiba mpya itakayozuia changamoto kama hizo.

Mwaka 2016, aliyekuwa Rais wa awamu ya tano John Magufuli (hayati), alipiga marufuku mikutano ya hadhara, huku akitoa fursa kwa wabunge na madiwani kufanya mikutano kwenye maeneo yao na wengine wakitakiwa kusubiri wakati wa uchaguzi.

Zuio hilo lilidumu hadi Januari 3, 2023 wakati Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi wa vyama 19 vya siasa, Ikulu jijini Dar es Salaam, alipotangaza kuliondoa zuio hilo.

Katika mkutano huo, Rais Samia amesema; “uwepo wangu leo hapa mahali nimekuja  kufanya ruhusa ya mikutano hii, nimekuja kutangaza kuondoa zuio la kuzuia mikutano ya hadhara na ninasema kwamba, sasa linaondoka,” amesema.